KINA MANDELA NI WENGI - 4

>>Chris Hani alivyokuwa kigingi
KINA Mandela ni wengi, pamoja na Chris Hani,
Alivyoupiga mwingi, Sauzi kule Kusini,
Alivyokuwa kigingi, hakufikia mwishoni,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Wakati kwapambazuka, ubaguzi wenda chini,
Chris Hani liibuka, walokuwa kileleni,
Tulidhani angeshika, nafasi uongozini,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Miaka msini na moja, kuchemka hadharani,
Wakaja tena wa kuja, na bunduki mikononi,
Mwili wake wakafuja, akaenda mautini,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Mwaka robaina mbili, alikuja duniani,
Tisina tatu kamili, akauawa jamani,
Alama liacha kweli, nyingi ziko vitabuni,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Akiwa kumi na tano, akaingia chamani,
Tena lishawishi mno, wenzake kutinga ndani,
Na moyo wake patano, kazi ni kwenda vitani,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Hakuipenda michezo, shuleni hata vyuoni,
Kuliko hiyo michezo, litaka ende vitani,
Ubaguzi ni kikwazo, litaka upigwe chini,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Chris Hani lijiunga, Umkhonto we Sizwe ndani,
Huko ndiko walipanga, vile vita msituni,
Ubaguzi walilenga, ya kwamba upigwe chini,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Aliwahi kukamatwa, kajiweka mafichoni,
Jina vile aliitwa, lingine likawa dini,
Lengo kama atafutwa, abaki uraiani,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Alijifunza Urusi, namna kuwa vitani,
Akachukua nafasi, kule Zimbabwe vitani,
Lengo kulipa kisasi, kumaliza ukoloni,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Alifanya mambo mengi, kule Lusaka kambini,
Wanawake wengi wengi, haki alizithamini,
Walipoupiga mwingi, wakarudia nyumbani,
Ukombozi wa Kusini, kina Mandela ni wengi.
Chris Hani alivyokuwa kigingiNa Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment