WAZAZI WADAIWA ADA ZAIDI YA MILIONI 168 SHULE YA MSINGI MKOANI YENYE MCHEPUO WA KINGEREZA
>> Wasababisha shule hiyo ya serikali kupata wakati mgumu kujiendesha
>> DED asema wazazi hawaoni umuhimu wa kulipa ada kwakuwa wanafunzi hawafukuzwi shule
>> Ada ya mwaka ni Tsh 400,000
Na Gustaphu Haule, Pwani
SHULE ya msingi mkoani yenye mchepuo wa kiingereza iliyopo kata ya Tumbi katika Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani ipo katika wakati mgumu wa kutekeleza majukumu yake kutokana na baadhi ya wazazi kushindwa kulipa ada kwa wakati.
Shule hiyo ya serikali ilianzishwa mwaka 2018 ili kuwawezesha wanafunzi kupata masomo sawa na shule za Kiingereza za binafsi ( Private) lakini changamoto iliyopo hivi sasa ni wazazi kushindwa kulipa ada ambayo ni Sh.400,000 kwa mwaka.
Amesema ada hiyo ni mgawanyo wa mihula miwili ambapo kila baada ya miezi sita mzazi anatakiwa kulipa Tsh.200,000 lakini bado wazazi wanashindwa kulipa jambo ambalo linapelekea uendeshaji wa shule hiyo kuwa mgumu.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Adelhelma Shawa akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake juzi amesema kuwa mpaka kufikia Julai 11,2025 shule hiyo inawadai Wazazi kiasi cha Tsh. 168,956,000.
Shawa amesema kati ya deni hilo lipo la miaka ya nyuma ambalo ni Tsh. 51,563,000 ambalo baadhi ya wazazi wamekuwa wakipunguza kwa kasi ndogo huku wengine wakiendelea kuruhusu watoto wao kwenda shule bila kupunguza deni.
Amesema kuwa ,wamekuwa wakichukua hatua ya mara kwa mara ikiwemo ya kuwaandikia barua wazazi ya kuwataka walipe madeni wanayodaiwa na wakati mwingine kufanya kikao cha pamoja na wazazi hao lakini utekelezaji wake umekuwa mdogo.
"Nimekuwa nikiwaita wazazi kwa ajili ya kufanya kikao na huwa tunajadiliana vizuri na mzazi uweka makubaliano ya kimaandishi kuwa siku fulani atalipa ada lakini akishatoka hapa Shuleni ndio mazima wala hatumuoni tena,"alisema Shawa.
Hata hivyo, Shawa amewaomba wazazi wenye watoto ambao wanadaiwa ada kujitokeza na kulipa madeni yao ili kusudi waweze kuendesha shule hiyo sambamba na kuhakikisha watoto wanapata haki ya elimu kwa kusoma katika mazingira mazuri.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa ameeleza kuwa hakuna mwanafunzi ambae amefukuzwa kwa kushindwa kulipa ada jambo ambalo limewafanya wazazi kutoona umuhimu wa kulipa ada kwa wakati.
"Ukienda shule za binafsi wanafunzi hawaruhusiwi kuingia darasani kama hawajalipa ada lakini hapo mkoani kwasababu ni shule ya serikali wapo ambao hawajigusi kabisa kulipa ada kwakuwa watoto hawafukuzwi "amesema.
Dkt.Shemwelekwa amesema wazazi waliopeleka watoto wao kusoma katika shule hiyo wanatakiwa kutambua kwamba shule haipokei ruzuku kutoka serikalini kwani inajiendesha yenyewe hivyo kutokulipa ada inakwamisha mipango iliyowekwa kutotekelezeka.
Shemwelekwa amesema kuwa shule hiyo inatakiwa kujiendesha yenyewe kama zinavyokuwa shule nyingine binafsi na mpango uliopo hivi sasa ni kuwaondoa walimu wote wa Serikali ili kusudi Shule iajiri walimu wake wenyewe.
"Shule inatakiwa kujiendesha yenyewe na kwasasa mpango uliopo ni kuwaondoa walimu wa Serikali ili shule iajiri walimu wake ,kwahiyo kama wazazi hawataki kulipa ada hiyo shule itajiendeshaje na walimu watalipwa nini? alihoji Mkurugenzi Shemwelekwa
Amewasisitiza wazazi kutambua majukumu yao na kuthamini malengo ya shule hiyo ambayo inatakiwa kujiendesha yenyewe kupitia ada za wanafunzi na kwamba shule nyingine za binafsi ada yake zinaanzia Milioni mbili na kwenda juu lakini Shule ya Mkoani ni Sh.400,000 kwa mwaka .
Mmoja wa wazazi mwenye mtoto anayesoma shule hiyo Omari Salehe amesema uwepo wa shule hiyo ni msaada kwao kwakuwa mtoto anasoma kwa gharama ndogo ikilinganishwa na shule nyingine za binafsi.
Post a Comment