HEADER AD

HEADER AD

MCHAKATO WA UJENZI WA SHULE YA MSINGI KILIMAHEWA PWANI UTAKAO GHARIMU MILIONI 291.5 WAANZA


Na Gustaphu Haule, Pwani 

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha  imeanza mchakato wa kujenga Shule mpya ya msingi katika Mtaa wa Kilimahewa uliopo Kata ya Tangini itakayogharimu kiasi cha Tsh. Milioni 291.5.fedha ambazo zimetoka katika ufadhili wa miradi ya Boost.

Utambulisho wa mradi huo umefanyika  Julai 17 ,2025 katika kikao maalum kilichofanyika kwenye jengo la Zanahati lililopo katika Mtaa wa Kilimahewa  Kata ya Tangini.

Kikao hicho kiliwashirikisha wadau mbalimbali wa elimu ikiwemo timu ya uongozi wa shule ya sekondari Bundikani iliyoongozwa na mkuu wa Shule hiyo Bernad Muyenjwa,timu ya Manispaa ya Kibaha iliyoongozwa na Kaimu afisa Elimu Msingi Hassan Miyanda.

      Mkuu wa Shule ya Sekondari Bundikani Manispaa ya Kibaha Bernad Muyenjwa akionyesha eneo linalotakiwa kujengwa Shule mpya ya Msingi Katika Mtaa wa Kilimahewa Kata ya Tangini.

Mbali na hao, lakini wengine ni viongozi wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) tawi la Kilimahewa akiwemo mwenyekiti wa tawi hilo Mwanahamisi Msuya pamoja na Katibu wa UWT tawi Hawa Omary huku wengine ni wenyeviti wa serikali za mitaa mitatu ya Machinjioni ,Kilimahewa , mailimoja "B " Mabalozi na baadhi ya wananch.

Awali akizungumza katika kikao hicho mkuu wa shule ya sekondari Bundikani Bernad Muyenjwa amesema kuwa fedha hizo zitajenga madarasa ya awali mawili,vyoo matundu sita,uzio na bembea za watoto.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bundikani Bernad Muyenjwa mwenye Tshirt ya njano akiwaongoza wataalam kutoka Manispaa ya Kibaha kukagua eneo la ujenzi wa Shule mpya ya Msingi katika Mtaa wa Kilimahewa Julai  17,2025.

Muyenjwa amesema pia zitajenga madarasa sita ya msingi ,vyoo matundu 12 ambapo kati ya hayo matundu 10 yatatumika kwa wanafunzi na matundu mawili yatatumika kwa walimu na viongozi mbalimbali (Staff) na jengo la utawala.

Amesema shule hiyo ya msingi itajengwa pembeni mwa shule ya Sekondari Tangini ambapo limetengwa eneo la ekari tano ambalo pia litatumika kwa ujenzi wa kituo cha polisi hapo baadae.

Muyenjwa,amesema pamoja na ujenzi wa shule mpya ya msingi lakini pia upo mpango wa kuongeza kujenga madarasa mengine manne ya sekondari katika shule ya Tangini ambapo amepokea kiasi cha Tsh.Milioni 88 fedha za kutoka katika mapato ya ndani ya Manispaa ya Kibaha.

Muyenjwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuleta miradi ya maendeleo Kata ya Tangini na kwamba kinachotakiwa ni kumuunga mkono Rais kwa kuhakikisha Oktoba wanaenda Kutiki.

      Mkuu wa Shule ya Sekondari Bundikani Manispaa ya Kibaha Bernad Muyenjwa akionyesha eneo linalotakiwa kujengwa Shule mpya ya Msingi Katika Mtaa wa Kilimahewa Kata ya Tangini.

Mratibu wa ujenzi huo Musa Shemaya, amesema kuwa baada ya kutambulisha mradi huo kinafuata ni kutangaza zabuni kupitia mfumo wa Nest na mshindi akipatikana itaandikwa ripoti kwa ajili ya kupeleka kwa Mkurugenzi wa Manispaa Dkt.Rogers Shemwelekwa.

Amesema zabuni hiyo itatangazwa wiki ijayo siku ya jumanne na itachukua siku tatu za kazi na kwamba mwenye vigezo atakayeshinda atapewa kazi hiyo mara moja.

Kaimu afisa Elimu msingi kutoka manispaa ya Kibaha Hassan Miyanda ambaye ndiye aliyetambulisha mradi huo amemshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa ya ujenzi wa madarasa.

     Kaimu afisa Elimu Msingi katika Manispaa ya Kibaha Hassan Miyanda akizungumza na baadhi ya wajumbe katika eneo la ujenzi wa Shule mpya ya Msingi katika Mtaa wa Kilimahewa Kata ya Tangini Julai 17,2025.

Miyanda,amesema kuwa kila Rais anayeingia madarakani huwa anakuja na vipaumbele vyake lakini Rais Samia amekuja na kipaumbele cha elimu ndio maana kila kata na mitaa kunajengwa Shule za msingi na Sekondari.

Amesema Manispaa ya Kibaha imepata mafanikio makubwa kupitia juhudi za Rais Samia na kwamba katika kipindi cha kifupi cha uongozi wake Manispaa ya Kibaha imepata kiasi cha Tsh.Milioni 921.7 za kujenga miundombinu ya shule za msingi.

Miyanda amewasisitiza wajumbe wa kikao hicho kuwa na ushirikiano katika ujenzi wa mradi huo huku akisema jambo la msingi ni kuwa mtu yeyote anatakiwa kukemea pale atakapoona mambo hayaendi sawa katika utekelezaji wa mradi huo 

" Watu wakipita wakiona mfuko wa cement (Saruji) unatoka kwenda bondeni halafu unasema hayakuhusu, hilo hapana kwani tunataka kila mtu awe msimamizi na ukiona jambo linakwenda kinyume unatoa taarifa kwa msimamizi haraka sana ili hatua zichukuliwe "amesema Miyanda 

Amesema ili kudhibiti upotevu wa fedha na malighafi za ujenzi wa shule hiyo Miyanda amesema tayari mpaka sasa wamepeleka barua Takukuru kwa ajili ya ufuatiliaji wa karibu kwani watakuwa wanafuatilia ujenzi huo tangu wanapomwaga mchanga,kokoto na hat ununuzi wa Saruji.

"Tumepeleka barua Takukuru kwa ajili ya ufuatiliaji wa mradi huu,na watakuwa wanafuatilia tangu siku ya kwanza ya kumwaga mchanga na kokoto ili wajue ni tipa ngapi zilikuwa zinatakiwa na zimemwagwa ngapi kwani naamini kwakufanya hivyo hakuna fedha ya mradi huu itakayopotea,"amesema .

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Kilimahewa Benedicto Alphonce ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka miradi mingi katika mtaa wake .

Alphonce amesema kuwa si tu shule ya msingi mpya inayotarajia kujengwa lakini pia tayari mtaa wake umepata sekondari na watoto wanasoma , zahanati ambayo ipo hatua za mwisho kukamilika.

Diwani anayetetea nafasi yake kata ya Tangini Mfaume Kabuga,amesema kuwa katika uongozi wake wa miaka mitano alikuwa anakiu ya kupata shule ya sekondari, zahanati,shule ya msingi na kituo cha Polisi.

Amesema anafurahi kuona miaka mitano imemalizika tayari mafanikio yake ni makubwa kwakuwa Tangini imepata shule ya sekondari, zahanati na shule ya msingi inajengwa na kwamba endapo wananchi wakimchagua kwa mara ya pili atahakikisha anakamilisha kituo cha afya na suala la miundombinu ya barabara.


No comments