UJENZI OFISI YA RC KAGERA KUGHALIMU BILIONI 9

Na Alodia Babara, Bukoba
SERIKALI hapa nchini imeanza ujenzi wa ofisi ya kisasa ya mkuu wa mkoa wa Kagera itakayoghalimu Tsh. Bilioni 9 hadi kukamilika kwake.
Katika hafla fupi ya kumkabidhi Mkandarasi eneo la ujenzi wa ofisi na kusaini mkataba lililofanyika jana, mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa ametaja sifa za jengo hilo baada ya kukamilika kwake kuwa, litadumu zaidi ya miaka 100, litakuwa zuri na litakuwa imara halitaharibiwa na tetemeko.
Mwassa ambaye ndiye mwanzilishi wa wazo la ujenzi wa ofisi hiyo amesema ofisi ya sasa ya mkuu wa mkoa wa Kagera ina miaka zaidi ya sitini ( 60 )na ubora wake umepungua kwa kiasi kikubwa,iliwahi kupitiwa na tetemeko,ziwa linaendelea kusogea na nyumba nyingi za watumishi zimemezwa na maji baada ya ziwa kusogea.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa akizungumza na wananchi walihudhuria hafla fupi ya kumkabidhi mkandarasi eneo la ujenzi na kusaini mkataba.
Amesema kuendelea kuboresha jengo hilo ni kupoteza fedha za serikali na kudai kuwa mchakato ulikuwa mrefu hadi kufikia hatua ya kumkabidhi mkandarasi kazi haikuwa rahisi.
Amesema Kagera inakwenda kuwa miongoni mwa mikoa ya kisasa na kuwa sehemu ya kivutio kwa wageni.
Hata hivyo amesema mkandarasi ameshalipwa asilimia 25 ya fedha kati ya Tsh. Bilioni 4.6 za mradi wa ujenzi wa jengo hilo awamu ya kwanza.
Awali mhandisi Raphael Nyatega kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kagera ,amesema mradi huo wa ujenzi umeanza mwaka wa fedha 2024/2025 na unatarajiwa kukamilika mwaka wa fedha 2025/2026.
Wa kwanza kulia ni mhandisi wa ujenzi ofisi ya mkuu wa mkoa Kagera Raphael Nyatega kulia kwake ni Mhandisi mwelekezi wa mradi Gozbert Kakiziba na anayefuata ni mkandarasi aliyekabidhiwa mradi Haamid Ashraf kutoka kampuni ya Skywords Construction Co.Ltd wakisaini mkataba
Mhandisi Nyatega amesema hatua ya Awali ilikuwa kufanya maandalizi ya mradi kulingana na mahitaji ya ofisi ya mkuu wa Mkoa kazi hiyo imefanyika na wataalam kutoka ofisi ya mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na mshauri elekezi.
Amesema mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa awamu mbili na awamu ya kwanza itakuwa na ofisi kuu kwa maana ofisi ya mkuu wa mkoa na wasaidizi wake,katibu tawala wa mkoa na wasaidizi wake,ukumbi wa mikutano utakao kuwa na uwezo wa watu 350,mgahawa mkubwa wa kisasa,ofisi ya habari maelezo na ofisi ya uwekezaji.
"Awamu hiyo pia itajumuisha ujenzi wa uzio,nyumba ya walinzi na ofisi ya madereva"anasema mhandisi Nyatega.
Anasema usanifu wa jengo hilo umezingatia nafasi ya Mkoa kimkakati katika uwekezaji. Anasema mradi huo wa ujenzi Awamu ya kwanza umesainiwa mkataba wa sh. Bilioni 4.6 na utakamilika kwa muda wa miezi 12 na mkandarasi huyo anasimamiwa na mshauri elekezi.
Ameongeza kuwa awamu ya pili itakuwa ujenzi wa jengo la watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa,itakuwa na ofisi za wakuu wa sehemu,vitengo pamoja na maofisa wote na wasaidizi wa ofisi.
Amesema awamu ya pili bado ipo katika hatua za usanifu inatarajiwa kugharimu Tsh Bilioni 4.4 na mpaka kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kagera unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 9.
Aidha,amesema faida za mradi huo ni pamoja na kuboresha utoaji huduma kwa wananchi katika njia za haraka na za kisasa,kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi,mradi utaweka mfumo wa vitendea kazi wa kisasa ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia,kuwa na eneo la kimkakati la kukaribisha na kuvutia wawekezaji na kuboresha mandhari ya mji wa Bukoba.
Naye mshauri mwelekezi katika mradi huo mbunifu majengo ( Architect ) Gozbert Kakiziba kutoka kampuni ya ( GOZTECTURE GROUP LTD)amesema jengo litakuwa imara halitapata shida ya kupitiwa na tetemeko na litakaa zaidi ya miaka mia moja.
Mhandisi mwelekezi wa mradi Gozbert Kakiziba akionyesha ramani ya mchoro wa ofisi ya mkuu wa mkoa huo irakavyokuwa.
Amemuambia mkandarasi aliyekabidhiwa eneo la mradi kuhakikisha kuwa hakuna kitu chochote kinachofanyika bila idhini ya mshauri elekezi.
Amemueleza kuwa sampo zote zipimwe kabla ya kutumika ili pande zote mbili ziwe salama na anatakiwa kutoa ripoti ya maendeleo ya ujenzi kila mwezi.
"Nikusisitize mkandarasi kutumia vibarua wanaotoka eneo hili la mradi, hasa zingatia wanawake na watu wenye ulemavu kwa shughuli wanazoweza kufanya" amesema mhandisi Kakiziba
Ofisi hiyo inajengwa manispaa ya Bukoba kata ya Rwamishenyi na Mkandarasi aliyekabidhiwa mradi huo ni Haamid Ashraf kutoka kampuni ya ( Skywords Construction Co.ltd )
Post a Comment