WANAFUNZI WA MAHITAJI MAALUM SIMIYU WAPATA MISAADA
Na Samwel Mwanga, Simiyu
WANAFUNZI wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Sima A iliyopo katika Hamlashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu wamepatiwa misaada mbalimbali kwa matumizi ya shule.
Misaada hiyo imetolewa Julai 13,2025 imetolewa na waendesha baiskeli kutoka Dar Es Salaam kuelekea wilaya ya Butiama mkoa wa Mara kwa lengo ni kusaidia wanafunzi hao kuweza kusoma katika mazingira yaliyo rafiki.
Waendesha baiskeli hao walikabidhi viti mwendo,magongo ya kutembelea, magodoro 40, vitanda 20 pamoja na kusaidia ujenzi wa matundu 10 ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi hao pia wamepanda miti 100 katika eneo la shule hiyo kwa lengo la kuhifadhi mazingira.
Akizungumza baada ya kupokea misaada hiyo, Afisa Elimu Maalum wa Mji wa Bariadi, Rutherford Magayame alikiri kuwa msaada huo umetolewa kwa wakati mwafaka, akisema utasaidia kuboresha mazingira ya ujifunzaji.
Afisa Elimu Maalum,Halmashauri ya mji wa Bariadi,Rutherford Magayane(kulia)akipokea vifaa mbalimbali kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Sima A mjini Bariadi.“Tunatoa shukrani za dhati kwa moyo wa upendo,walimu wenye taaluma ya kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwemo viziwi na wasioona ni wachache hivyo tutatumia vifaa hivi kupunguza changamoto nyingi kwa watoto wetu na kuongeza ari ya kujifunza,”amesema.
Awali Gabriel Lando ambaye ni kiongozi wa waendesha baiskeli hao wakiwa wanatoka mataifa mbalimbali ya nchi za Afrika Mashariki na Kati wakiwemo Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Tanzania amesema kuwa safari yao siyo kwa ajili ya michezo pekee bali ni kuchochea mabadiliko ya kijamii katika sekta ya elimu,afya na mazingira.
Baadhi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Sima A mjini Bariadi wakipanda miti na baadhi ya waendesha baiskeli kwenye eneo la shule hiyo.“Tunaendeleza ile kampeni yetu kuboresha amani,umoja na mshikamano kwa kuchochea shughuli za maendeleo katika sekta ya elimu,afya na mazingira pia ni kuenzi urithi wa Mwalimu Nyerere kupitia vitendo vya mabadiliko katika jamii,tunataka wanafunzi wenye mahitaji maalum wapate fursa sawa ya elimu,”amesema.
Msafara huo umewezeshwa na Vodacom Tanzania na Benki ya Stanbic, akizungumza Meneja wa Vodacom,kanda ya Ziwa, Stratton Mchau amesema kuwa wataendelea kudhamini safari hizo za kwenda Butiama kumuenzi Baba wa Taifa, Mwl Nyerere katika kuchochea na kuleta mabadiliko katika jamii.
Meneja wa Vodacom Kanda ya ziwa,Stratton Mchau (mwenye kipaza sauti)akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi misaada mbalimbali kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule ya Msingi Sima A mjini Bariadi.“Kwa mwaka huu Vodacom Fondation tunategemea kuzitembelea shule 30,kupanda miti zaidi ya 50,000 na zaidi wa watu 700,000 watagushwa kwa namna moja au nyingine,”amesema.
Waendesha baiskeli hao wanatarajiwa kuhitimisha safari yao Butiama kwa shughuli maalum ya kumuenzi Mwalimu Nyerere ambaye alisimamia misingi ya haki, elimu kwa wote na usawa katika jamii.
Post a Comment