ALAMA BARABARANI
ALAMA za barabarani, kwetu sote ni muhimu,
Kizishika kwa makini, usalama unadumu,
Ajali barabarani, zitakuwa ni adimu,
Tuhakikishe alama, zote zasomeka vema.
Ni nyingi barabarani, alama zinazodumu,
Tunaziona machoni, kuzifwata tunadumu,
Twajifunza darasani, tuweze kuzifahamu,
Tuhakikishe alama, zote zasomeka vema.
Chache ziko akilini, ambazo kwetu muhimu,
Zikiwa barabarani, zaepusha hali ngumu,
Twasafiri kwa amani, magari na wanadamu,
Tuhakikishe alama, zote zasomeka vema.
Mistari ya njiani, hiyo kwetu ni muhimu,
Mwishoni barabarani, katikati inadumu,
Tukiiona machoni, twachukua zetu zamu,
Tuhakikishe alama, zote zasomeka vema.
Alama barabarani, mistari ni muhimu,
Hasa usiku njiani, ikiwepo kwetu hamu,
Kukwepa kwenda mwituni, na ajali za adimu,
Tuhakikishe alama, zote zasomeka vema.
Kikosa barabarani, dereva kazi ni ngumu,
Kutambua hasa nini, nafasi yake yadumu,
Tatamba barabarani, na kuyaleta magumu,
Tuhakikishe alama, zote zasomeka vema.
Myeupe barabarani, mistari ikidumu,
Watumiaji njiani, hawapati kazi ngumu,
Kuitambua machoni, kuchukua yao zamu,
Tuhakikishe alama, zote zasomeka vema.
Wakuu barabarani, kuweka alama dumu,
Tutoeni hatarini, ajali ziwe adimu,
Tusafiri kwa amani, magari na binadamu,
Tuhakikishe alama, zote zasomeka vema.
Mipaka barabarani, vema sana ikidumu,
Walio barabarani, wachukue zao zamu,
Usalama uwe dini, sote tupate kudumu,
Tuhakikishe alama, zote zasomeka vema.
Sote tukiwa makini, usalama utadumu,
Ajali barabarani, tazidi kuwa adimu,
Kukiwa na mtihani, sote tutauhitimu,
Tuhakikishe alama, zote zasomeka vema.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment