UTAJIJUA MWENYEWE

UKIWA mzima wewe, huwezi elewa kitu,
Utajiona mwenyewe, mbele ya watu ni mtu,
Na hata watu wenyewe, tadhani waona mtu,
Mambo yakibadilika, utajijua mwenyewe.
Nilikuwa na rafiki, karibu na kule kwetu,
Hakuwa mtu wa kiki, bali ni mtu wa watu,
Kwa mtu habadiliki, anachojali ni utu,
Mambo yakibadilika, utajijua mwenyewe.
Pesa kwake mfukoni, za kununulia vitu,
Hakuwa mtu shidani, wa kupungukiwa kitu,
Saidia masikini, alifanya kote kwetu,
Mambo yakibadilika, utajijua mwenyewe.
Balaa likamjia, kwa ajali ya matatu,
Vile alivyoumia, kilichobakia utu,
Akitaka kwenda njia, lazima bebwe na mtu,
Mambo yakibadilika, utajijua mwenyewe.
Marafiki wa zamani, wale walikuja kwetu,
Ngetegemea jamani, waonyeshe wao utu,
Kuja hosipitalini, au karibu na kwetu,
Mambo yakibadilika, utajijua mwenyewe.
Zaidi aliumia, kusikia wale watu,
Meno wakimsagia, sababu mekuwa butu,
Yote alowafanyia, wanayaona si kitu,
Mambo yakibadilika, utajijua mwenyewe.
Simu akiwapigia, kupokea wako butu,
Lake akiwaambia, wanasingizia kitu,
Subiri ntakupigia, wala hawapigi katu,
Mambo yakibadilika, utajijua mwenyewe.
Tunachojifunza hapa, usiwaamini watu,
Kama Mungu amekupa, mali siyo za upatu,
Ikifika uko kapa, kwako humuoni mtu,
Mambo yakibadilika, utajijua mwenyewe.
Mwenye upendo wa kweli, ndiye huyu Mungu wetu,
Kwetu haijali hali, anayabeba ya kwetu,
Yu nasi kila mahali, ndiye kimbilio letu,
Mambo yakibadlika, utajijua mwenyewe.
Tegemea mwanadamu, ulaaniwe we mtu,
Ni kujitoa fahaamu, ukimwacha Mungu wetu,
Rudia uwe timamu, tegemea Mungu wetu,
Mambo yakibadilika, utajijua mwenyewe.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment