WAGOMBEA UBUNGE ESTHER MATIKO WA CCM NA JACKSON KANGOYE WA ACT WAZALENDO WAWEKEANA PINGAMIZI

>> Esther alimwekea pingamizi Jackson kutoteuliwa kuwa mgombea ubunge akidai hajakidhi matakwa ya kanuni ya ACT Wazalendo
>Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Tarime mjini alitupilia mbali pingamizi la Esther Matiko
>> Jackson naye amwekea Esther pingamizi , atuma nakala ya pingamizi kwa Mkurugenzi INEC, Msajili wa vyama vya siasa, Jaji mkuu mahakama Kuu Tanzania, Mkurugenzi TAKUKURU
DIMA Online, Tarime
MSIMAMIZI wa uchaguzi Jimbo la Tarime mjini Erasto Maternus Mbunga ametupilia mbali pingamizi lililotolewa na Esther Nicholas Matiko mgombea ubunge Jimbo la Tarime mjini, kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kwamba mgombea ubunge Jimbo la Tarime mjini Jackson Kangoye wa Chama cha ACT Wazalendo hana sifa za kuwa mbunge.
Msimamizi huyo wa uchaguzi amelikataa pingamizi lililoandikwa na Esther Matiko na kusema kwamba ni kinyume na Ibara ya 67 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Ameongeza kuwa muweka pingamizi Esther Matiko endapo asiporidhika na majibu ya msimamizi wa uchaguzi anayo haki ya kukata rufaa kwenda Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ndani ya saa 24 tangu kupokelewa kwa barua hiyo na nakala kutumwa kwa Jackson Kangoye.
Msimamizi wa uchaguzi aliandika barua hiyo Agosti, 29, 2025, saa 8: 30 asubuhi.
Isemavyo Katiba Ibara ya 67 (2)
Ibara ya 67 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasema Mtu hatakuwa na sifa za kustahili -
(a) Ikiwa mtu huyo anao au kwa hiari yake amejipatia uraia wa nchi nyingine yoyote ; au
(b) Ikiwa kwa mujibu wa sheria inayotumika katika Jamhuri ya Muungano imethibitishwa rasmi kwamba mtu huyo ana ugonjwa wa akili.
(c) Ikiwa mtu huyo amehukumiwa na mahakama yoyote katika Jamhuri ya Muungano na kupewa adhabu ya kifo au kufungwa gerezani kwa muda unaozidi miezi sita kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote , vyovyote linavyoitwa , linaloambatana na utovu a uaminifu.
(d) Ikiwa katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya uchaguzi mkuu amepata kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo kwa kosa linaloambatana na utovu wa uaminifu au kuvunja sheria ya maadili ya viongozi wa Umma.
(e) Bila ya kuingilia haki na uhuru wa mtu kuwa na maoni yake, kuamini dini atakayo, kushirikiana na wengine na kushiriki shughuli za Umma kwa mujibu wa sheria za nchi , ikiwa mtu huyo si mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa.
(f) Ikiwa mtu huyo ana maslahi yoyote katika mkataba wa serikali wa aina yoyote aliyowekewa miiko maalum kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge, na iwapo amekiuka miiko hiyo.
(g) Ikiwa mtu huyo ameshika madaraka ya afisa mwandamizi katika utumishi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano isipokuwa madaraka ambayo Rais aweza au anatakiwa kukabidhi kwa mbunge kwa mujibu wa katiba hii au sheria iliyotungwa na Bunge .
( h) Ikiwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge inayoshughulikia makosa yanayohusika na uchaguzi wa aina yoyote mtu huyo amezuiliwa kujiandikisha kama mpiga kura au kupiga kura katika uchaguzi wa wabunge.
Pingamizi la Esther Matiko
Agosti, 28, 2025 Esther Matiko ambaye ni mgombea ubunge Jimbo la Tarime mjini kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) aliandika barua kwa msimamizi wa uchaguzi Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi Jimbo la Tarime mjini akiomba Tume kutomteua Jackson Ryoba Kangoye anayegombea ubunge wa Jimbo hilo kupitia chama cha ACT Wazalendo kwamba kakosa sifa za kuwa mgombea ubunge .
Mgombea ubunge Jimbo la Tarime mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) , Esther Matiko .
Katika barua hiyo ya Esther alieleza sababu kwamba Jackson hajakidhi matakwa ya kanuni za kudumu za uendeshaji wa Chama cha ACT Wazalendo, sifa za wagombea, utaratibu wa kutangaza nia .
Pia fomu za kugombea na mapingamizi Ibara ya 9 (a) ya kanuni za uchaguzi ya 2024 inayosema " awe mwanachama wa ACT Wazalendo aliyejiunga si chini ya siku saba (7) kabla ya tarehe ambayo mchakato wa uchaguzi umetangazwa.
" Kwa kanuni tajwa hapo juu Kangoye Jackson Ryoba anakosa sifa ya kuwa mgombea maana mchakato wa uchaguzi unaanzia ndani ya chama, kwa mujibu wa kanuni tajwa hajakidhi takwa la kanuni la kuwa mwanachama wa ACT Wazalendo kabla ya siku 7 kuanza kwa mchakato mpaka tarehe 23, 08, 2025.
" Kangoye alikuwa mwanachama wa chama cha Mapinduzi (CCM) akijadiliwa na kamati kuu ya halmashauri kuu ya chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa kupitisha jina lake kwa mgombea ubunge kupitia CCM ambapo 27/8/2025.
" Jackson akiongea na vyombo vya habari mara baada ya kurudisha fomu kwenye Tume Huru ya uchaguzi alikiri kushiriki michakato yote ya kura za maoni ndani ya CCM nambatanisha video yake " Barua imeeleza.
Esther aliongeza kuwa tangu kumalizika kwa vikao hivyo vya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa ni takribani siku nne (4) tu zimepita 23/8/2025 - 27/8/2025 huku jina lake Jackson likionekana kuwa ni mwanachama wa ACT Wazalendo aliyependekezwa kugombea ubunge Jimbo la Tarime mjini kupitia Chama hicho .
" Kwa pingamizi hili naomba ofisi yako itengue uteuzi wa Jackson kwani amekosa sifa kwa mujibu wa fomu Namba 98 (c) ya Tume Huru ya Taifa .
Jackson amwekea pingamizi Esther
Mgombea ubunge Jimbo la Tarime mjini kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo , Jackson Ryoba Kangoye, amemwekea pingamizi Esther Nicholas Matiko la kutoteuliwa kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Tarime mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwakuwa amepoteza sifa ya kugombea ubunge.
Jackson ameyasema hayo kupitia barua yake ya pingamizi aliyoiandika Agosti, 29, 2025 kwa msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Tarime mjini na kusema kuwa hadi sasa Esther ni mwacahama wa Chama cha Maendeleo (CHADEMA) .
" Mimi, Jackson Ryoba Kangoye, mgombea ubunge Jimbo la Tarime mjini kwa tiketi ya Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), ninawasilisha
pingamizi hili kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Toleo la 2023.
" Sheria ya Uchaguzi, Sura ya 343, na kanuni zake, na sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258, kupinga uteuzi wa Bi. Esther Nicholas Matiko kugombea
nafasi ya ubunge katika Jimbo la Tarime Mjini kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM)" Barua imeeleza.
Jackson amesema kwamba uanachama wa CHADEMA na ubunge wa viti Maalum (2020) katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Esther Nicholas Matiko aligombea nafasi ya ubunge katika Jimbo la Tarime Mjini lakini hakupata ushindi.
Amesema baadaye alikula kiapo cha ubunge mbele ya Spika wa Bunge kuwa mbunge wa Viti Maalum kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Hata hivyo, Viongozi wa Chama chake walikana kupeleka majina ya wabunge 19 wa Viti Maalum kwa ajili ya kuapishwa utokana na kukataa na kususia matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwama 2020.
Amesema kufutwa uanachama na maamuzi ya CHADEMA baada ya kuapishwa, Baraza Kuu la CHADEMA lilitoa maamuzi ya kumfukuza
uanachama kutokana na kukiuka taratibu na kudhoofisha mamlaka ya Chama.
Jackson amesema kwa mujibu wa Ibara ya 71(1)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, “Mbunge hupoteza nafasi yake iwapo atakoma kuwa mwanachama wa chama cha siasa kilichompeleka Bungeni”.
" Hivyo basi, baada ya kufutwa uanachama, Esther Nicholas Matiko hakustahili kuendelea kuwa mbunge. Rufaa na Madai Mahakamani.
Ni kweli kwamba Esther Nicholas Matiko na wenzake 18 walijaribu kukata rufaa ndani ya chama chao na hata kufungua shauri Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kupinga uamuzi wa Baraza Kuu la CHADEMA kuwafuta Uanachana wa CHADEMA " Barua imeeleza.
Sababu za pingamizi
Jackson amesema kwamba Hukumu ya Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam
Tarehe 14/12/2023 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliwapa ushindi wabunge 19 wa viti maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliokuwa
wakipinga uamuzi wa Baraza Kuu la chama hicho la kuwafuta uanachama.
Amesema Jaji katika kesi hiyo, Chrispian Mkeha alisema Esther Nicholas Matiko na wenzake 18, wataendelea kuwa wanachama wa CHADEMA kwa kuwa Baraza Kuu la chama hicho
lilikwenda kinyume na Kanuni ya Kawaida ya kutokupendelea.
Hivyo hukumu ya Mahakama ilithibitisha Esther Nicholas Matiko na wenzake 18
wamefutiwa adhabu ya kufutwa uanachama wa Chadema, hivyo kisheria ni wanachama hai na wanapaswa kuendelea kuwa bungeni kama wabunge wanaotokana na Chadema. Na wakaendelea kuwa Wabunge halali hadi Bunge lilipovunjwa tarehe
03/08/2025.
Uanachama wa Esther Matiko CCM
" Taarifa za uanachama wa Esther Nicholas Matiko zinazopatikana kupitia Aplikesheni ya CCM (CCM App), zinatupa taarifa muhimu kuhusu uanachama wake kama ifuatavyo;
" Taarifa za uanachama Jina: Esther Nicholas Matiko Kadi ya Gamba No: AC 4480503 Tarehe ya Usajiri Gamba: 14/07/2022 Namba ya Kielektroniki: C0003-0182-608-1NB: Kwa taarifa hizi ni rasmi kuwa Esther Nicholas Matiko ni mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) toka tarehe 14/07/2022.
" Na hizi ndio taarifa ambazo ziko
kwenye fomu ya CCM aliyoomba kugombea Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi. Na pia nimeambatanisha picha (screenshot) inayoonyesha taarifa hizi " anasema Jackson kupitia barua yake.
Amesema sheria ya vyama vya Siasa, Sura ya 258 kupitia tangazo la Serikali Na. 710 la tarehe 28/08/2020. Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura 258. Sehemu ya pili A: Uanzishaji wa Vyama Vya Siasa.
Miiko ya Uanachama na Ushiriki katika shughuli za Vyama vya Siasa.
Kipengele cha pili kinasema: “Mtu hatakuwa mwanachama wa Chama cha kisiasa zaidi ya kimoja".
Kipengele cha tatu kinasema: “Mtu mwenye kadi za uanachama wa zaidi ya Chama kimoja cha kisiasa atachukuliwa kuwa amejiuzulu kutoka katika chama chake cha awali”. Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama Vya siasa mtu hawezi kuwa mwanachama wa Chama zaidi ya kimoja cha siasa.
" Vilevile mtu akiwa na Uanachama wa Chama kingine moja kwa moja anakuwa
amejivua uanachama wa Chama cha awali. Na kwa kuwa taarifa za uanachama wa Esther Nicholas Matiko inaonekana ni mwanachama wa CCM Toka 14/07/2022.
" Na itambulike bayana hukumu ya Mahakama ya tarehe 14/12/2023 ilimpa uhalali wa uanachama wake ndani ya CHADEMA ili aendelee kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi tarehe 03/08/2025" Barua imeeleza.
Jackson amesema kuwa Esther Nicholas Matiko alichukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akiwa mwanachama halali wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa mujibu wa Hukumu ya Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, tarehe 14/12/2023.
" Hivyo kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria ya vyama vya siasa na Hukumu ya Mahakama kuu Kanda ya Dar es Salaam hadi anachukua fomu kugombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) .
"Bado Esther Nicholas Matiko alikuwa
mwanachama halali wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na sio mwanachama halali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hivyo amekosa sifa kugombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Tarime Mjini.
" Lakini pia inathibitisha Esther Nicholas Matiko hana uadilifu kwani alikula kiapo
kuitetea na kuilinda na kuiheshimu katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini kinyume chake alienda mahakamani kutetea uanachama wake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), huku akiwa na kadi ya Chama cha Mapinduzi (CCM)" Barua imeeleza .
Jackson amesema kwamba alichofanya Esther ni dharau kubwa kwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dharau kwa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dharau kwa Sheria ya Vyama vya siasa.
" Kitendo hicho cha mgombea huyu wa Ubunge wa Jimbo la Tarime Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Esther Nicholaus Matiko cha kuhitimisha safari ya ubunge wa viti maalum kupitia CHADEMA huku akiwa mwanachama wa CCM ni uvunjifu mkubwa wa Katiba ya Nchi ya 1977, sheria ya vyama vya Siasa, Kanuni , Maadili na Miiko ya
viongozi wa Umma.
" Vile vile kitendo cha kuendelea kupokea mshahara, marupurupu na stahiki mbalimbali yakiwemo mafao ya ubunge aliyopokea baada ya kuhitimisha ubunge wake wa viti maalum kwa miaka mitano baada ya Bunge kuvunjwa rasmi tarehe 03/08/2025.
" Sio sahihi hata kidogo kwani huo ni ubadhirifu wa hali ya juu; na ni matumizi mabovu ya fedha za walipa kodi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kitendo hicho ni rushwa, ubadhirifu na ufisadi mkubwa ambapo haupaswi kuvumiliwa hata kidogo.
" Na katika hili taasisi mbalimbali za nchi zinazohusika na maadili na miiko
ya viongozi wa Umma, Taasisi zinazohusika na kuzuia wizi, na ubadhirifu wa mali za Umma ikiwemo TAKUKURU; wanapaswa kushughulika na mgombea huyu ndugu
Esther Nicholaus Matiko " Barua imeeleza.
Jackson ameiomba Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) itengue uteuzi wa Esther Nicholas Matiko kama mgombea Ubunge wa Jimbo la Tarime Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa kukosa sifa, maadili, miiko na uhalali kushiriki shughuli za Vyama vya Siasa, ikiwa ni pamoja na uchaguzi kwa mujibu wa sheria.
" Nimewasilisha pingamizi hili nikiwa mgombea Ubunge wa Jimbo la Tarime mjini kupitia Chama Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), nikitimiza haki na wajibu wangu wa kikatiba kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa heshima, huru na haki unaozingatia maadili na miiko ya viongozi wa umma.
Jackson ameandika barua hiyo na
Nakala kutuma kwa Mkurugenzi
Tume Huru ya Uchaguzi (INEC)
Kwa Taarifa ya Pingamizi, Msajiri wa Vyama vya Siasa Kwa taarifa na kufuatilia Utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa.
Pia nakala kwa Jaji Mkuu Mahakama Kuu ya Tanzania kwa rejea ya hukumu ya Mahakamu Kuu Kanda ya Dar es Salaam katika kesi Wabunge 19 wa Viti Maalum CHADEMA dhidi ya Baraza Kuu la CHADEMA kupinga kuvuliwa uanachama wao, nakala kwa Mkurugenzi Mkuu
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa uchunguzi na matumizi mabaya ya fedha za Umma.
Post a Comment