HEADER AD

HEADER AD

CHARLES MWERA WA ACT WAZALENDO AREJESHA FOMU KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA TARIME VIJIJINI


>> Asema akiwa mbunge atahakikisha anaisimamia serikali ili kuwaletea maendeleo wananchi

>> Charles Mwera na mgombea wa CCM Mwita Waitara wanatoka Kata moja ya Itiryo

DIMA Online, Tarime

MWENYEKITI wa Chama cha ACT Wazalendo mkoa wa Mara, Charles Mwera Nyanguru amechukua na kurejesha fomu ya kugombea ubunge Jimbo la Tarime Vijijini .

Mgombea huyo amerejesha fomu Agosti, 27, 2025 katika ofisi ya msimamizi mkuu wa uchaguzi Jimbo la Tarime vijijini iliyopo halmashauri ya wilaya ya Tarime. 

Charles Mwera aliwahi kuwa mbunge wa Jimbo la Tarime kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na atachuana na Mwita Mwikwabe Waitara mgombea ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi ( CCM) ambaye anatetea nafasi yake ya ubunge kwa miaka mingine mitano.

Charles amesema kuwa hamuogopi Waitara katika siasa kwani ana uzoefu wa kutosha kwakuwa amekuwa mwanasiasa kwa miaka mingi kupitia vyama mbalimbali vya kisiasa na amewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Tarime mwaka 2008 baada ya kifo cha aliyewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Tarime Chacha Zakayo Wangwe.

     Mgombea ubunge Jimbo la Tarime vijijini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mwita Waitara alisalimiana na mgombea ubunge chama cha upinzani cha ACT Wazalendo Charles Mwera (kulia) wakati walipokutana ofisi ya halmashauri ya Wilaya ya Tarime kurejesha fomu.

Amewaomba wananchi kumwamini na kutokuwa na shaka nae kwani akipata ridhaa ya kuwa mbunge atahakikisha anaisimamia serikali ili iweze kuwaletea maendeleo wananchi .

" Nina uzoefu katika siasa na uongozi kwani nimewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Tarime na nimewahi kuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime hivyo sina shaka yoyote" amesema Charles.

Ameongeza kuwa Jimbo la Tarime vijijini bado lina changamoto nyingi ambazo zinahitaji kusemewa na kutatuliwa na mamlaka ikiwemo changamoto za huduma ya afya, umeme na miundombinu ya barabara.

       Viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo wakiwa wamemsindikiza Charles Mwera (wa kwanza kulia ) mgombea Ubunge Jimbo la Tarime vijijini.

Amesema akipata ridhaa ya kuwa mbunge atahakikisha anasimamia mapato ya halmashauri zikiwemo fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ziweze kufanya kazi ipasavyo bila hujuma.

" Simuhofii Waiatara maana ninaamini wananchi wananifahamu vyema na wanakumbuka mazuri yangu , ninaomba wananchi mniunge mkono mnipe ridhaa ili nikawawakilishe bungeni katika kuzisemea changamoto zilizopo jimboni ili ziweze kutatuliwa kwa wakati " amesema Charles Mwera .

Charles Mwera ameipongeza ofisi ya Msimamizi mkuu wa uchaguzi katika Jimbo hilo akiwemo msimamizi mkuu wa uchaguzi na afisa uchaguzi kumwelekeza vyema bila hiyana pale alipohitaji kupata uelewa.

   Msimamizi mkuu wa uchaguzi Jimbo la Tarime vijijini Simon Langoi ( Kulia) akimwelekeza Charles Mwera mgombea ubunge Jimbo la Tarime Vijijini kupitia ACT Wazalendo .

" Naipongeza ofisi ya msimamizi mkuu wa uchaguzi Jimbo la Tarime Vijijini wamenitendea haki pale nilipohitaji ufafanuzi na uelewa walinielimisha wamenielekeza kwa moyo mmoja na nimerejesha fomu yangu, sasa nasubiri uteuzi kutoka Tume huru ya uchaguzi .

" Ninaamini Tume itatenda haki kwakuwa ni Tume huru itarejesha jina langu maana vigezo vyote ninavyo na nimevizingatia katika ujazaji wa fomu " amesema Charles.

Katibu wa Chama cha ACT Wazalendo Jimbo la Tarime Vijijini Gesero Marwa Makore amesema kwamba chama hicho kimejipanga vyema na kitapita kila kata kuweza kuwanadi wagombea wake.

          Katibu wa Chama cha ACT Wazalendo Jimbo la Tarime Vijijini Gesero Marwa Makore.

Amewaomba wananchi kuwaunga mkono ili kuwapa ushindi wagombea wa ACT waweze kusimamia maslahi ya wananchi ikiwemo kuhakikisha huduma za kijamii zinaboreshwa.

" ACT tukishinda tunaahidi kusimamia vizuri mapato yanayotokana na rasilimali ili wananchi wa kawaida waweze kunufaika na mapato hayo.

" Wananchi wasisahau kutupatia kura kwasababu tumeleta wagombea wanaokubalika , Charle Mwera amewahi kuwa mbunge na Mwenyekiti wa halmashauri na maendeleo yalionekana , tumpe nafasi tena akatusemee kwa maendeleo ya wananchi wa Jimbo la Tarime vijijini" amesema Katibu .

Msimamizi mkuu wa uchaguzi Jimbo la Tarime vijijini Simon Langoi amesema zoezi la uchukuaji fomu na urejeshaji limekwenda vizuri hakuna malalamiko na kwamba hadi sasa waliochukua na kurejesha fomu kugombea ubunge Jimbo la Tarime Vijijini ni Mwita Waitara wa CCM na Charles Mwera wa ACT Wazalendo.

        Afisa Uchaguzi Jimbo la Tarime vijijini akimpokea mgombea ubunge chama cha ACT Wazalendo, Charles Mwera wakati alipowasili halmashauri ya wilaya ya Tarime kurejesha fomu.





No comments