HEADER AD

HEADER AD

JACKSON KANGOYE ASEMA DHARAU ZA ESTHER MATIKO ZIMESABABISHA AHAMIE ACT WAZALENDO KUGOMBEA UBUNGE TARIME MJINI



>> Asema Esther Matiko amekuwa mbunge  kwa miaka 15 mfululizo hivyo hana Jipya

>>Asema wananchi wa Tarime wanataka mtu sahihi na si chama, na mtu sahihi ni yeye

>> Asema ni maamuzi magumu kuhama CCM lakini yenye lengo la kuwatumikia wananchi

DIMA Online , Tarime

KATIKA hali isiyo ya kawaida aliyekuwa mtiania wa ubunge Jimbo la Tarime mjini kupitia Chama cha Mapinduzi CCM, Jackson Ryoba Kangoye amekiahama chama cha Mapinduzi (CCM).

Jackson Kangoye ametimkia chama cha upinzani cha ACT Wazalendo ambapo amechukua na kurejesha fomu ya kugombea ubunge Jimbo la Tarime mjini.

Akizungumza na Waandishi wa habari Agosti, 27, 2025 mara baada ya kurejesha fomu ofisi ya msimamizi mkuu wa uchaguzi Jimbo la Tarime mjini, Jackson amesema kwamba ameondoka CCM kutokana na dharau alizozionesha Esther Matiko aliyeteuliwa na CCM Taifa kugombea ubunge Jimbo la Tarime mjini.

         Mgombea ubunge Jimbo la Tarime mjini kupitia Chama cha ACT Wazalendo Jackson Kangoye akiwa viunga vya ofisi ya Halmashauri ya mji Tarime baada ya kuwasilisha fomu yake kwa msimamizi mkuu wa uchaguzi .

" Sijafukuzwa nimeondoka CCM kwa hiari na utashi wangu ,ni baada ya kukaa na kutafakari namna nilivyokitumikia chama na hali iliyopo sasa . Nimehamia ACT Wazalendo kutokana na dharau za Esther Matiko.

" Awali niliahidi kwamba nikishindwa nitamuunga mkono aliyeteuliwa kugombea ubunge lakini sijafanya hivyo baada ya kuona Esther Matiko akitutambia na kutuonesha dharau. Alikuwa akitamba kwamba yeye hata akipata kura asilimia mbili au asilimia 10 jina lake litarudi tu kutoka Taifa.

" Kweli jina lake limerudi , ndipo nikaamini kwamba kumbe haukuwa uchaguzi bali kuna watu tayari walikuwa wameshapangwa ndio maana Esther alikuwa akitamba kwa ujasiri akiwa na uhakika wa jina lake kurudi.

" Kuna wakati unaamua kufanya maamuzi magumu. Haiwezekani mtu umeitumikia CCM kwa miaka mingi alafu mtu anatoka na kuhamia CCM ndani ya muda mfupi na kuchukua fomu alafu anateuliwa kugombea ubunge na kuachwa wagombea ambao wameitumikia CCM kwa miaka mingi" amesema Jackson .

Jackson amesema kwamba mbali na dharau za Esther amehamia ACT Wazalendo kwakuwa watu wa Tarime hawaangalii chama wanaangalia mtu sahihi na mtu sahihi ni yeye .

      Msimamizi mkuu wa uchaguzi Jimbo la Tarime mjini Mbuga Erasto Mbung'a (kulia) akiwa na mgombea ubunge Jimbo la Tarime mjini Jack Kangoye kupitia ACT Wazalendo pamoja na kiongozi wa ACT Jimbo la Tarime mjini (wa kwanza Kulia) . 

" Wakati mwingine unalazimika kuhama kutokana na matakwa ya wajumbe kutosikilizwa. Baada ya mlango wa chama cha Mapinduzi kufungwa ACT Wazalendo wamenifingulia mlango.

" Nimechukua na kurejesha fomu ya kugombea ubunge kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo nikiwa na malengo ya kuwatumikia wananchi " amesema Jackson.

Ameongeza kwamba mgombea wa CCM Esther Matiko ni dhaifu ni mgombea ambaye sio matamanio ya wananchi na wanachama wa CCM na kwamba kwa kipindi Esther alichoongoza kwa miaka 15 mfululizo hana Jipya.

Mgombea ubunge kupitia chama cha ACT Wazalendo Jimbo la Tarime mjini, Jackson Kangoye (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na mgombea ubunge wa chama hicho Jimbo la Tarime vijijini Charles Mwera (kulia) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo mkoa wa Mara.

Amesema endapo akichaguliwa kuwa mbunge atahakikisha anazuia rasilimali za nchi zisitumike vibaya lakini pia kuhakikisha huduma za kijamii zinaongezeka na kuboreshwa, zikiwemo hospitali, shule kwakuwa mahitaji ya kijamii yanazidi kuongeza kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu.

"Sijabahatisha kuchukua haya maamuzi, chama cha ACT Wazalendo kimetoa mgombea anayefaa. Nikiwa mbunge nitahakikisha nawasemea wananchi, nitapiga kelele juu ya matumizi makubwa ya gharama za serikali.

" Matamanio yangu nikuona kodi zinazolipwa na wananchi zinarudi kuwafanyia wananchi maendeleo. Nitahakikisha nasimamia vyema asilimia 10 ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu maana ukichunguza kwa makini fedha hizo haziwafikii walengwa zaidi ya kuzisoma kwenye makaratasi.

Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Jimbo la Tarime mjini Laurent Johanes Marwa amesema kwamba kutokana na sera za chama hicho wana matumaini makubwa ya Jackson kushinda ubunge .

Amesema katika Jimbo hilo wamesimamisha madiwani kata sita kati ya nane na amewaomba wananchi endapo Jackson akipata ridhaa wamchague kwa kura za kishindo.

       Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Jimbo la Tarime mjini Laurent Johanes Marwa akizungumza 

Wasemavyo wananchi, wanaccm

Baadhi ya wananchi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wameunga mkono hatua ya Jackson kuhama CCM na kusema kwamba kuhama chama ni hiari ya mtu.

Mwanachama mmoja wa CCM mkazi wa mtaa wa Rebu Sokoni amesema " Kwakweli hata mimi nimefurahi kuona Jack ameamua kutafuta mlango mwingine wa kutokea , huyu kijana yuko vizuri kutuwakilisha lakini CCM imekuwa ikimtenga hampatii nafasi .

" Amewahi kushinda kura za maoni lakini jina lake halikurudi likaletwa la mshindi namba mbili ambaye ni Kembaki nakuwa mbunge , na sasa limeletwa jina la mshindi wa tatu Esther Matiko aliyehamia CCM siku chache kisha akachukua fomu ya kugombea ubunge na jina lake limerudi ,walioitumikia CCM kwa muda mrefu wameachwa.

" Sioni ubaya Jackson kuhamia upinzani kwasababu hata katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 20 inatoa haki ya mtu kukutana na watu wengine , kuchanganyika na kujiunga na vyama " amesema mwanachama wa CCM.

Mwanachama mwingine wa CCM amesema " CCM Taifa imetukosea sana kumchukua mtu ambaye alikuwa upinzani na kuhamia CCM ndani ya muda mfupi alafu unamleta agombee ubunge ni kuwavunja moyo wanaccm hasa walioitumikia chama kwa miaka mingi.

" Mimi nilitegemea kwamba kwakuwa Esther amekuwa mbunge kwa miaka 15 basi kama wanaona ni muhimu kuwepo bungeni angepewa nafasi katika vile viti 10 vya Rais na sio kuja kuwapora madaraka wanaccm kindakindaki, kiukweli wanaccm tumeumia sana bora akagombee upinzani tutamuunga mkono " amesema mwanaccm.

Mwanachama mwingine wa CCM mkazi wa Nkongore amesema" Mimi sikuwa na wasiwasi kwasababu Esther alituambia tusiwe na wasiwasi hata kama amekatwa jina CCM Taifa itarejesha jina lake na kweli jina lake limerudi . Tumchague Esther ndio chaguo la Rais Samia" amesema.

Mariam Tura mkazi wa mtaa wa uwanja wa Ndege mwenye ulemavu wa viungo amesema " Nimeumia sana baada ya jina la Kembaki kutorudishwa maana alitujali sana sisi walemavu alitukatia bima za afya, wakina mama wa Rebu sokoni tukanunuliwa miamvuli siku hizi hatuungui jua.

" CCM imeleta mtu wao imemuacha Kembaki , nilikuwa nimekataa sitopiga kura lakini baada ya kusikia Jackson Kangoye amehamia ACT Wazalendo nitampigia kura maana hata yeye ni mtu wa watu amewahi kuwakaribisha nyumbani kwake watu wenye ulemavu na kula nao chakula " amesema Mariam.

James Marwa mkazi wa mjini Tarime amesema " Baada ya wafuasi wa Kembaki kukamatwa kwa tuhuma za rushwa na clip kusambaa zikiwaonesha vijana wa Kembaki wakiwa na silaha za uhalifu sisi tulitegemea jina litakalorudishwa ni la Jackson.

" Lingerudi jina la Jackson tusingeona shida maana Jack aliwahi kushinda kura za maoni na badala yake akaletwa Kembaki , haijarishi Kembaki amepata kura nyingi angetangazwa Jackson ingekuwa sawa tungeona wamelipizana na Kembaki angelidhika maana hata yeye alikuwa mshindi wa pili lakini jina lake lilirudi " amesema.

Chacha Marwa mkazi wa Tarime mjini amesema " Mi naona maamuzi ya CCM Taifa yako sahihi kwasababu kazi ya wajumbe ni kupiga tu kura za maoni na wenye maamuzi wa mwisho ni CCM Taifa.

" Wao wameona Esther anafaa kuwa mbunge ni sawa, tumuunge mkono ili CCM ishinde lakini pia Jackson kuhamia ACT Wazalendo ni hiari yake.

" Mimi sishangai maana yeye sio mtu wa kwanza kuhama CCM hata wengine walihama CCM wakaenda upinzani na wamerejea nyumbani , kwahiyo hata Jackson ipo siku atarejea nyumbani." amesema Chacha.

Rejea 

Jackson alichukua fomu ya kutiania ubunge Jimbo la Tarime mjini kupitia CCM Juni, 29, 2025 nakuwa miongoni mwa watiania wapatao 14 waliochukua fomu .

Kamati kuu ya halmashauri ya CCM Taifa katika kikao chake kilichofanyika tarehe 28, Julai 2025 kiliwateuwa wanachama 7 waliotiania kugombea ubunge Jimbo la Tarime mjini akiwemo Jackson jina lake lililokuwa la kwanza ili kupigiwa kura za maoni na wanachama.

Katika matokeo ya kura za maoni CCM mshindi wa kwanza alikuwa Michael Mwita Kembaki aliibuka mshindi kwa kura 1,572, mshindi wa pili Jackson Ryoba Kangoye aliyepata kura 364, mshindi wa tatu Esther Nicholas Matiko kura 196, mshindi wa nne  Machare Heche Suguta kura 60, Said Kisyeri Chambili kura 31, Mussa Ryoba Deus kura 18 na Robert Mkirya Chacha kura 3.

CCM Taifa ilimteua mshindi wa tatu Esther Matiko kugombea ubunge Jimbo la Tarime vijijini ambapo Juni, 29, 2025 alitangaza kupitia vyombo vya habari kujiunga na chama cha Mapinduzi akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) .

Juni ,28, 2025 hadi Julai , 02, 2025 Chama cha Mapinduzi CCM kilitoa ratiba ya uchukuaji fomu za kugombea ubunge na udiwani. Esther alichukua fomu Julai, 01, 2025 kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM ambapo alikuwa mbunge mstaafu wa viti maalum kupitia CHADEMA.

Ikumbukwe kuwa katika kura za maoni uchaguzi wa mwaka 2020 Jackson Kangoye alikuwa mshindi wa kwanza kwa kuongoza kwa kura za maoni 126, mshindi wa pili Michael Kembaki aliyepata kura 64, Martin Mwita kura 29 na Wakili Onyango kura 11.

Hata hivyo, chama cha Mapinduzi ngazi ya Taifa kilirejesha jina la mshindi wa pili Michael Kembaki kugombea ubunge Jimbo la Tarime mjini ambapo alifanikiwa kuwa mbunge na kuongoza kwa miaka mitano.

Katika uchaguzi wa mwaka huu wa  2025 Esther Matiko ndiye atakayeipeperusha bendera ya CCM kugombea ubunge Jimbo la Tarime mjini akichuana na Jackson Kangoye kwa tiketi ya ACT Wazalendo.



No comments