KINYONGA NA KONOKONO
NENDA mbele rudi nyuma, huo ndio mwendo wetu,
Vyuma huwa tunakaza, na kulegeza kivyetu,
Shamba letu tunalima, mazao twafyeka yetu,
Kinyonga na konokono, nao wanafika kwao.
Nyumba imeshasimama, hayo ni makazi yetu,
Unaibomoa nzima, zibaki tofali zetu,
Ni wapi tutasimama, kupata kivuli chetu?
Kinyonga na konokono, nao wanafika kwao.
Halija alinselema, mchakamchaka wetu,
Nyuma unatusukuma, eti kali mbio zetu,
Sasa tumeshasimama, zazorota afya zetu,
Kinyonga na konokono, nao wanafika kwao.
Jirani ninamsoma, anayepitia kwetu,
Anasimamisha boma, ramani katoa kwetu,
Sisi bado lelemama, twakuna Ubongo wetu,
Kinyonga na konokono, nao wanafika kwao.
Ujana povu lavuma, wanasema ndio zetu,
Wainuka na kukwama, kwa ile mipango yetu,
Wanafanya ya lazima, tumboni wapate kitu,
Kinyonga na konokono, nao wanafika kwao.
Wazee nao wagoma, wanataka mambo yetu,
Ona wababa wazima, warandia dada zetu,
Nao hao kinamama, wafuga vijana wetu,
Kinyonga na konokono, nao wanafika kwao.
Huyu taa alizima, kisema faida yetu,
Mwingine huyu asema, iwashwe kwa mwanga wetu,
Twageuka mbele nyuma, huo ndio mwendo wetu,
Kinyonga na konokono, nao wanafika kwao.
Tunazo Tabia njema, zizo sawa mila zetu,
Naona tunazisoma, na kuiga za wenzetu,
Wengine watu wazima, wazisagia za kwetu,
Kinyonga na konokono, nao wanafika kwao.
Unabii ni karama, wengine wala si yetu,
Mazingira tukisoma, twashika videvu vyetu,
Tuendako ni kisima, hatukijazi mwakwetu,
Kinyonga na konokono, nao wanafika wao.
Akili kama yagoma, kurudi nyumbani kwetu,
Tumelowea mazima, ugenini kusokwetu,
Wenzetu ona wavuma, kwa matunda yale yetu,
Kinyonga na konokono, nao wanafika kwao.
Na Lwaga Mwambande ( KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment