HEADER AD

HEADER AD

FEDHA TARAKIMU

FEDHA hizo tarakimu, na hazina mwisho hizo,

Kama wewe una hamu, kuzipata pesa hizo,

Kwa furaha ya kudumu, utakonda kwa mawazo,

Usikurubie pesa, hutaipata furaha. 


Pesa tunaifahamu,kwa mambo mengi ni nguzo,

Ukiwa nazo ni tamu, kutatua matatizo,

Lakini ni tarakimu, bila mwisho ila mwanzo,

Usikurubie pesa, hutaipata furaha. 


Hivyo wewe mwanadamu, ikae kwenye mawazo,

Furaha inayodumu, si zile pesa unazo?

Tengeneza tabasamu, kutaka pesa mzozo,

Usikurubie pesa, hutaipata furaha. 


Furaha iliyo tamu, isokuwa na kikwazo,

Ulivyonavyo vitamu, si pesa ulizonazo,

Hazitoshi mwetu humu, tajiletea mzozo,

Usikurubie pesa, hutaipata furaha. 


Kuridhika ni muhimu, hayo ya kwangu mawazo,

Ingawa pesa muhimu, sisake kimatangazo,

Jua hizo tarakimu, zimejaa maingizo,

Usikurubie pesa, hutaipata furaha. 


Tartakimu zinadumu, ni sawa na hizi tozo,

Pesa nazo tarakimu, saka zisiwe tatizo,

Kitu kile ufahamu, hazitakupa tulizo,

Usikurubie pesa, hutaipata furaha. 


Pesa jua tarakimu, kila zilipo ni mwanzo,

Hivyo usiweke hamu, zishike zile unazo,

Kutafuta ukidumu, utakuwa hamnazo,

Usikurubie pesa, hutaipata furaha. 


Pesa hizo tarakimu, tarakimu zina mwanzo,

Mwisho hatuufahamu, wabakia kwenye wazo,

Tusijiweke ugumu, kusaka kwa nguvu hizo,

Usikurubie pesa, hutaipata furaha.


Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments