UKIBEBWA UBEBEKE
UMEFUNGWA wafugika, kuku unanichekesha,
Vile ulivyoridhika, kwamba hayo ni maisha,
Unaona umefika, huna wa kukutingisha,
Hisani hiyo yaisha, ukibebwe ubebeke.
Njaa inapokushika, wewe unaliamsha,
Siyo kwenda kupigika, ni kelele za kutosha,
Chakula kikishafika, kula kulala maisha,
Hisani hiyo yaisha, ukibebwe ubebeke.
Umetulia hakika, kula kulala maisha,
Wenzako wachangamka, wewe ndio wawapisha,
Hutaki kushughulika, hata wakikufundisha,
Hisani hiyo yaisha, ukibebwe ubebeke.
Unaishi Tanganyika, ni ya zamani maisha,
Tanzania imefika, fanya kujichangamsha,
Wasubiria mkeka, huko ndiko unakesha,
Hisani hiyo yaisha, ukibebwe ubebeke.
Wenzako wachangamka, kutengeneza maisha,
Wewe hapo umefika, mshefa anakulisha,
Vipi atapokatika, wapi sura utaosha?
Hisani hiyo yaisha, ukibebwe ubebeke.
Muda wa kuerevuka, utoto umeshakwisha,
Bora ukafahamika, vile wajishughulisha,
Kitu chochote kishika, Mungu baraka tashusha,
Hisani hiyo yaisha, ukibebwe ubebeke.
Maisha yanakatika, hata bila ya tamasha,
Ni vipi yakimfika, huyo anayekulisha,
Ni nani utamshika, kwa mahitaji kutosha?
Hisani hiyo yaisha, ukibebwe ubebeke.
Usikae kuridhika, uzio walozungusha,
Toka nje changamka, pata kitu cha motisha,
Kama hicho wakishika, mbele chaweza kuvusha,
Hisani hiyo yaisha, ukibebwe ubebeke.
Kuku muda kuamka, anza kujishughulisha,
Chakula kikikatika, pata nguvu kujilisha,
Hatua ukizishika, ndugu zako tawakosha,
Hisani hiyo yaisha, ukibebwe ubebeke.
Mimi ninavyodamka, usingizi haujesha,
Ni huko kuhangaika, nipate vya kunitosha,
Nimeondoa mashaka, Mungu ananiwezesha,
Hisani hiyo yaisha, ukibebwe ubebeke.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment