HEADER AD

HEADER AD

SPONSA AKISHAKUFA UTAULA WA CHUYA


HATA mfadhili hufa, ukabaki huna kitu,

Si vema kwake ukafa, awe ndiye kila kitu,

Haya ndiyo maarifa, usitegemee mtu,

Sponsa akishakufa, si utaula wa chuya?


Kwa mtoto njema sifa, kumtegemea mtu,

Mzazi mlezi sifa, katika jamii zetu,

Huzuni mzazi kufa, malezi yabaki butu,

Sponsa akishakufa, si utaula wa chuya?

 

Kwako eti ni mshefa, anakupa kila kitu,

Kote unampa sifa, wengine wote si watu,

Unatafuta ulofa, atapoingia kutu?

Sponsa akishakufa, si utaula wa chuya?


Unaoga kwenye ofa, mbele za watu ni mtu,

Hufikirii maafa, yanayowakuta watu,

Wengine kwako malofa, unawapiga viatu,

Sponsa akishakufa, si utaula wa chuya?


Ona ulimpa sifa, kazimika siyo mtu,

Wapi utafanya dhifa, na kutetemesha watu?

Au kukalia sofa, ili uwanange watu?

Sponsa akishakufa, si utaula wa chuya?


Watu huenda masafa, wasilete tena kitu,

Au wakijaa sifa, wakuteme sio mtu,

Au wewe ni refa, umlazimishe mtu?

Sponsa akishakufa, si utaula wa chuya?


Ni Neno la maarifa, linalofaa kwa watu,

Tegemea aso kufa, huko ndiko weka utu,

Kuliko wanaokufa, ubaki na ukurutu,

Sponsa akishakufa, si utaula wa chuya?


Kalaniwa tena lofa, ategemeaye mtu,

Huyu mtu anakufa, kwamba kwake kila kitu,

Kuna siku atasafa, kitoweka huyo mtu,

Sponsa akishakufa, si utaula wa chuya?


Haya ndiyo maarifa, usitegemee mtu,

Mungu afaaye sifa, mshike ubaki mtu,

Huyo hasa ndiye refa, wa maisha yote yetu,

Sponsa akishakufa, si utaula wa chuya?


Masponsa wanakufa, maana nao ni watu,

Hata akina Kayafa, kifo hakijali mtu,

Mbele yetu kuna ofa, mtegemee Mungu tu,

Sponsa akishakufa, si utaula wa chuya?


Na Lwaga Mwambande (KiMPAB

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments