HEADER AD

HEADER AD

HOFU YETU IWE YAO

WATU tunacheka nao, Tunafanya kazi nao,

Watu tunaishi nao, Tuko nyumba moja nao,

Watu tunalala nao, Chumba na kitanda nao,

Lakini mioyo yao, Inawaza mambo yao.


Kukuua lengo lao, Ufukuzwe raha yao,

Ufulie cheko lao, Filisika hamu yao,

Aibika raha yao, ukifa amani yao,

Sababu mioyo yao, Inawaza mambo yao.


Kuchafua nchi yao, Hiyo ndiyo raha yao, 

Faida iwe ya kwako, itune mifuko yao,

Wakati taifa lao, aibu yake si yao,

Sababu mioyo yao, inawaza mambo yao.


Kuua watu wa kwao, Hiyo ni furaha yao, 

Wasikitishe wa kwao, Sababu ya njia zao, 

Wazilete shida kwao, kwayo mienendo yao,

Sababu mioyo yao, inawaza mambo yao.


Wameshikwa gonjwa hao, siyo wa kupona hao,

Hata na mioyo yao, inayawaza ya kwao,

Ya wengine siyo yao, kwao hayana makao,

Sababu mioyo yao, inawaza mambo yao.

 

Kuwabadilisha hao, tuvae viatu vyao,

Kuomba rehema kwao, Mungu wetu awe wao,

Hofu yetu iwe yao, Waziache njia zao,

Sababu mioyo yao, inawaza mambo yao.


Yale ya kwao mazao, Toka kwa miungu yao,

Yachomwe yatoke kwao, Mioyo jiwe ya kwao,

Wala isibaki nao, kwani ni hasara kwao,

Sababu mioyo yao, inawaza mambo yao.


Mungu aitoe kwao, kusiweko na makao,

Mioyo ya nyama kwao, hiyo ndiyo iwe yao,

Wamjue Mungu wao, Awe kiongozi waom 

Sababu mioyo yao, inawaza mambo yao.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments