HIVI KUKU NI KWA NINI

HIVI kuku ni kwa nini, huwezi ukatulia?
Hizo kelele za nini, mbona unajichulia?
Unataka tafrani, hivyo unavyojitia,
Wakati mwingine ndugu, ni bora ukanyamaza.
Kuku ukitaka taga, kelele twazisikia,
Hata ukienda oga, vumbi watutifulia,
Si ufanye kwa kuzuga, yako ukimalizia?
Wakati mwingine ndugu, ni bora ukanyamaza.
Vifaranga kipatia, kelele twazisikia,
Kote unakopitia, nduru tunazisikia,
Hujui unaitia, adui kukuvamia?
Wakati mwingine ndugu, ni bora ukanyamaza.
Ukitoka taga yai, sikio twashikilia,
Kelele kama vile mbwai, wewe tunakusikia,
Wafanya anywapo chai, atake cha kukaangia,
Wakati mwingine ndugu, ni bora ukanyamaza.
Jogoo waliitia, mlo meandalia,
Pale anapokujia, mbio unamkimbia,
Si ungemnyamazia, aende na yake njia?
Wakati mwingine ndugu, ni bora ukanyamaza.
Kimya kimya ukifanya, maisha utapatia,
Hata sehemu kupenya, enenda kwa kunyatia,
Anotaka kukufinya, vigumu kukufikia,
Wakati mwingine ndugu, ni bora ukanyamaza.
Waweza kufikiria, yale unajifanyia,
Bora kuwatangazia, wengine kuwatambia,
Watu wakiangalia, hawawezi kusifia,
Wakati mwingine ndugu, ni bora ukanyamaza.
Kelele unazofanya, unajikaribishia,
Watu wataokusonya, na yako kukuibia,
Ndani kwako watapenya, aibu kukuachia,
Wakati mwingine ndugu, ni bora ukanyamaza.
Wajifanya u angani, hakuna kukufikia,
Kumbe mchwa wako chini, ngazi wakutafunia,
Kelele zako njiani, anguko zimechangia,
Wakati mwingine ndugu, ni bora ukanyamaza
Wapo watu wengu sana, kimya kimya wajilia,
Mambo yao ukiona, huwezi kuaminia,
Wenyewe hutawaona, kelele watupigia,
Wakati mwingine ndugu, ni bora ukanyamaza.
Kuku wangu naamini, yangu umeyasikia,
Na kwamba unathamini, ushauri wenye nia,
Kelele siyo thamani, ni nguo wajivulia,
Wakati mwingine ndugu, ni bora ukanyamaza.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment