HEADER AD

HEADER AD

JAMII YATAKIWA KUPIMA VINASABA VYA UGONJWA WA SELIMUNDU


Na Gustaphu Haule, Pwani 

SERIKALI kupitia Wizara ya afya  Kitengo cha Selimundu (Sickle cell) imesema kuwa ugonjwa wa Selimundu sio ugonjwa wa kurogwa kama ambavyo jamii inachukulia lakini  ugonjwa huo ni wakurithi kutoka kwa mzazi mmoja kwenda kwa mzazi mwingine.

Imesema ili kujiepusha na ugonjwa huo ni vyema kabla ya kuingia katika mahusiano jamii inapaswa kuchukua hatua ya kwenda kupima vinasaba vya ugonjwa na endapo watakuwa salama wanaweza kuoana na hatimaye kujenga familia salama isiyo na ugonjwa wa Sikoseli.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya damu kutoka katika hospitali ya Amana iliyopo Jijini Dar es Salaam Jamila Makame,ametoa kauli hiyo katika semina ya siku moja kwa  baadhi ya Waandishi wa Mkoa wa Pwani iliyolenga masuala ya ugonjwa wa Sikoseli .

Semina hiyo iliyofanyika Agosti 12,2025 katika kituo cha afya Mkoani kilichopo Manispaa ya Kibaha iliwajumuisha baadhi ya Waandishi wa habari ambapo Dr.Makame amesema Selimundu ni ugonjwa wa kurithi ambao chanzo chake ni vinasaba kutoka kwa wazazi wa pande mbili.

      Baadhi ya Waandishi wa habari wa Mkoa wa Pwani wakiwa katika picha ya pamoja na madaktari bingwa wa magonjwa ya damu akiwemo Jamila Makame wa kwanza kushoto mara baada ya semina ya siku moja kuhusu masuala ya ugonjwa wa Selimundu.

Makame,amesema kuwa kuna vinasaba vya aina tatu tofauti na ili uweze kutambua kundi la vinasaba hivyo lazima hatua ya haraka ichukuliwe ikiwa pamoja na kupima na kusema kuwa vipo vinasaba vitatu vya Sikoseli ambavyo ni  AA ,AS na SS.

Amesema ukipimwa ukikutwa una (AA) ujue upo kawaida lakini ukipimwa ukikutwa una (AS) maana yake umebeba vinasaba vya Selimundu lakini ukipimwa ukikutwa na (SS )ni wazi kuwa unagonjwa wa Sikoseli.

"Ili kuepuka na kizazi cha ugonjwa wa Sikoseli ni vyema vijana wakachukua hatua ya kupima yeye na mwenza wake na endapo wakajua kama wapo salama basi wanaweza kufunga ndoa lakini kama watakutwa inakuwa njia rahisi ya kujiepusha na ugonjwa huo,", amesema Dr. Makame.

Amesema takwimu za Selimundu duniani ni kuwa watoto 300,000 -400,000 huzaliwa na ugonjwa wa Selimundu kila mwaka lakini Tanzania ni nchi ya nne duniani kwakuwa na ugonjwa wa Sikoseli na kwa Afrika inashika nafasi ya tatu kwani kila mwaka watoto 14000 huzaliwa wakiwa na ugonjwa huo.

Amesema dalili za ugonjwa huo ni maumivu ya viungo,upungufu wa damu,manjano kwenye macho na ngozi ,kuvimba miguu na mikono,vidonda sugu pamoja na kuvimba bandama.

Ameongeza kuwa madhara ya ugonjwa huo ni makubwa ikiwemo kudumaa kwa ukuaji wa mtoto,ulemavu wa kudumu ,vifo vya mapema huku akisema mama wajawazito wapo katika hatari zaidi.

Daktari bingwa wa watoto na magonjwa ya damu wa mkoa wa Pwani Pius Muzzazzi amesema kuwa mkoa wa Pwani ni moja ya Mkoa wenye jamii kubwa ambayo inahudhuria kliniki kupata huduma ya matibabu.

Amesema Mkoa wa Pwani jumla ya watu wanaohudhuria Kliniki ya ugonjwa kuwa ni 6,145,ambapo Mkuranga ni 1,444, Manispaa ya Kibaha 1,290, Bagamoyo 1,078,Rufiji 582,Kibiti 541, Kisarawe 510, Chalinze 340, Kibaha Vijijini 205 na Mafia 155.

Ameishukuru Serikali kwa kuimarisha huduma ya matibabu Kwa wagonjwa wa Sikoseli kwakuwa sahihi hivi huduma hiyo inapatikana katika vituo vyote vya afya ,hospitali za Wilaya na hata Mkoa ambapo ameishauri jamii kujitokeza kupima ili kutambua afya zao.

Mratibu wa huduma ya Selimundu kutoka Wizara ya afya Asteria Mpoto,amesema kuwa lengo la kutoa semina hiyo kwa Waandishi wa habari ni kutaka kufikisha elimu sahihi kwa jamii kuhusiana na ugonjwa wa Selimundu ikiwemo kuelewa maana ya Selimundu kutoa taarifa sahihi kwa jamii na kuhamasisha jamii kutambua afya zao.

      Mratibu wa huduma za Selimundu kutoka Wizara ya afya  Asteria Mpoto akieleza umuhimu wa Waandishi wa habari katika kuhamasisha jamii juu ya kujitokeza kupima vinasaba vya Selimundu.

Mpoto amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kutaka kufuta mila potofu zilizopo katika jamii ambayo imekuwa ikiamini ugonjwa wa Selimundu ni ugonjwa unaotokana  na imani ya kishirikina lakini pia kutanua wigo wa elimu kwa jamii ili wajitokeze kupima ugonjwa huo na hatimaye wapate tiba.

Amewaomba Waandishi wa habari kwenda kutoa elimu kwa jamii juu ya ugonjwa huo na wameamua kuwatumia Waandishi wa habari kwakuwa wanaweza kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja kupitia vyombo vyao.

Amesema  semina hiyo wameanza kutoa katika Mkoa wa Tanga,Pwani na baada ya hapo wataenda katika Mkoa wa Dar es Salaam ,Manyara, Arusha na Rukwa ambapo wakiwa katika Mkoa husika ukutanisha makundi mbalimbali ya kijamii kwa ajili ya kuwapa elimu hiyo.

Mkuu wa mkoa wa Pwani amesema walianza kutoa semina hiyo Agosti 11, 2025 kwa viongozi wa dini ya kiislam na Kikristo na kisha Agosti 12 kutoa elimu kwa Waandishi wa habari na Agosti 13 wamewafikia kundi la walimu wa Shule mbalimbali.

      Baadhi ya Waandishi wa habari wa Mkoa wa Pwani wakiwa katika semina ya siku moja kuhusu masuala ya ugonjwa wa Selimundu iliyofanyika Agosti 12,2025 katika kituo cha afya Mkoani kilichopo Manispaa ya Kibaha.

No comments