KUKU ANABAKI KUKU

KUKU anabaki kuku, mwewe ni adui yake,
Hata awe na vikuku, mwewe si saizi yake,
Yeye chini ni shauku, mwewe anapaa zake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.
Kama refa yuko chini, rafu za mwewe si zake,
Hiyo mana yake nini, mwewe apeta kivyake,
Akiwa juu ya chini, yuko na jamaa yake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.
Nilivyowaona juzi, kuku na bata mwenzake,
Kwa mazoezi wajuzi, kila mtu na mwenzake,
Wasiwasi toka juzi, uwanja wa mechi yake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.
Kuku ni mkubwa kwake, wala sio mlo wake,
Ila vifaranga vyake, hivyo ni halali yake,
Kuku na kelele zake, mwewe vifaranga vyake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.
Kitaka teke la punda, uguse mkia wake,
Anaweza kukuponda, aridhishe roho yake,
Utabaki amekonda, ukiwa pembeni yake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.
Vifaranga vikiliwa, zabaki kelele zake,
Autangaze ukiwa, wausikie wenzake,
Apate kuhurumiwa, kirudi nyumbani kwake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.
Waingia mchezoni, wadai refa ni wake,
Wajidai ulingoni, ama zako ama zake,
Makali ya mkononi, mpini naona kwake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.
Damu meanza kutoka, mwewe anafanya yake,
Kiunzi utakivuka, uweze kufika kwake?
Au wataka sikika, yeye akipeta zake?
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.
Kuku mashindano yako, waweza uaibike,
Umalize pesa zako, wengine watajirike,
Bora ungelinda vyako, vifaranga siwe vyake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.
Pembeni ninasimama, kutazama mwisho wake,
Yule atayesimama, kipigwa filimbi yake,
Ninaombea salama, yakosekane mateke,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.
Natamani kuwa mwewe, kule aliko nifike,
Kuku asiruhusiwe, nile vifaranga vyake,
Nani mgumu ka jiwe, asipende raha zake?
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.
Kama wakabiliana, kila mtu paso pake,
Vita yaweza umana, hakuna mshindi wake,
Hapo wakubaliana, kila mtu ale vyake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.
Refa bila kamisaa, tajifanyia kivyake,
Ni nani atamvaa, kuyapinga yale yake?
Tusubiri nusu saa, apige kipenga chake,
Kushindanisha wawili, refa hatambulikani.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment