KIBOKO

SI kile cha kuchapia, huyu Kiboko mnyama,
Tabiaze nakwambia, hatabiriki mnyama,
Na kama akikujia, kimbia isiwe noma,
Tembelea mbuga zetu, jionee utajiri.
Kwa ukubwa twasikia, wanyama wakisimama,
Kiboko wa tatu pia, nchi kavu kwa wanyama,
Tembo anatangulia, Faru mbili asimama,
Tembelea mbuga zetu, jionee utajiri.
Uzito unafikia, Kiboko akisimama,
Moja na nusu sikia, tani jike zinakoma,
Dume hapo huanzia, na zaidi kimpima,
Tembelea mbuga zetu, jionee utajiri.
Viboko wajikalia, kwenye kundi kama chama,
Kumi waweza anzia, hadi thete wasimama,
Majini wajiishia, usiku wasaka ngama,
Tembelea mbuga zetu, jionee utajiri.
Aweza kujikalia, kwenye maji bila noma,
Dakika zinafikia, tano hali amezama,
Juu hujipumulia, kwa juu akiachama,
Tembelea mbuga zetu, jionee utajiri.
Mimea jitafutia, hawaruki kama kima,
Wao huongoza njia, majani kwao ni mema,
Kilometa hufikia, kumi wakisaka ngama,
Tembelea mbuga zetu, jionee utajiri.
Mimba wanashikilia, myezi nane kama mama,
Pale anajizalia, hicho kitoto cha mama,
Kilo huweza fikia, hamsini kama duma,
Tembelea mbuga zetu, jionee utajiri.
Ila wakijizalia, vidume kwa dume noma,
Laweza vishambulia, visiweze kusimama,
Liweze kushikilia, utawala usokoma,
Tembelea mbuga zetu, jionee utajiri.
Hivyo akijizalia, vidume kazi kwa mama,
Kwa mbali kuvifichia, dume lisije vifuma,
Mbali likaviulia, libaki limesimama,
Tembelea mbuga zetu, jionee utajiri.
Kiboko kimsikia, kwa wanyama huyu noma,
Vigumu mtabiria, kwake nini kinavuma,
Sitake kukaribia, pale aliposimama,
Tembelea mbuga zetu, jionee utajiri.
Mabwawa na mito pia, maziwa makazi mama,
Hali inayotishia, maisha huyu mnyama,
Wale wanaovizia, makazi yanayokoma,
Tembelea mbuga zetu, jionee utajiri.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment