HEADER AD

HEADER AD

CCM PWANI YAWATAKA WATIANIA WALIOONGOZA KURA ZA MAONI KUTOBWETEKA

Na Gustaphu Haule, Pwani

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani kimewataka wagombea wa ubunge na udiwani walioongoza katika mchakato wa kura za maoni kuwa watulivu mpaka hapo utaratibu wa chama utakapokamilika. 

Kimewataka wagombea wa ubunge wa vitimaalum walioongoza kuacha kubweteka na badala yake wapite katika maeneo yao kwa ajili ya kumuombea kura mgombea wa Urais wa CCM Dkt . Samia Suluhu Hassan.

Katibu wa Siasa,uenezi na mafunzo wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) mkoa wa Pwani David Mramba ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Waandishi wa habari Agosti 14, 2025 kwenye ofisi za CCM mkoa zilizopo katika Manispaa ya Kibaha.

        Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM )Mkoa Pwani David Mramba akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu mchakato wa kujadili majina ya wagombea ubunge na udiwani wa mkoa wa Pwani ,kikao hicho kimefanyika Agosti 14, 2025 katika ofisi za CCM mkoa zilizopo katika Manispaa ya Kibaha.

Amesema kuongoza katika uchaguzi wa kura za maoni sio kama tayari umekuwa mbunge kwani chama kina utaratibu wake ambao mpaka hivi sasa unaendelea kufanyikal kupitia vikao vyake mbalimbali.

Amesema majina ya madiwani walioongoza katika uchaguzi wa kura za maoni utaratibu wake ulianzia katika vikao vya kamati ya Siasa vya Kata ,vikao vya Wilaya na vikao vya Mkoa.

Mramba ameongeza kuwa baada ya vikao vya mkoa kumalizika majina hayo yamekwenda katika kikao cha Sekretarieti ya Taifa na huko ndiko kutafanyika maamuzi ya mwisho ya chama na kisha kuletwa majina ambayo yatatangazwa na mkoa.

Kuhusu wagombea ubunge Mramba amesema kuwa mchakato wa mkoa wa kupitia majina hayo  umemalizika Agosti 13,2025 na kisha kupelekea katika ngazi ya Taifa.

       Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani David Mramba akizungumza na Waandishi wa habari katika kikao chake kilichofanyika Agosti 14, 2025 .

Amesema kinachofuatia kwasasa ni kusubiri vikao vya juu vya chama kikiwepo kikao cha Sekretarieti ya Taifa, Kikao cha Kamati Kuu na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ambapo baada ya kukamilika mchakato huo jina la mgombea mmoja litapitishwa na litasomwa na CCM Taifa.

"Tumemaliza mchakato wa kupitia majina yote Agosti 13,2025 lakini kwasasa tunasubiri vikao vya juu ambavyo ndivyo vyenye maamuzi ya mwisho kwahiyo wagombea lazima wawe watulivu kwa ajili ya kusubiri maamuzi ya chama," amesema Mramba.

Ameongeza kuwa wale wote walioongoza katika uchaguzi wa kura za maoni hawapaswi kufanya jambo lolote la kusheherekea wala kutengeneza vikundi vyovyote vya ushabiki kwakuwa kufanya hivyo ni kujiondolea  sifa ya kupendekezwa na kuteuliwa.

Hatahivyo,amewaomba wanachama wanaotumia makundi mbalimbali ya mitandao ya kijamii kuacha kutoa taarifa zisizo sahihi kwakuwa kufanya hivyo ni sawa na kuleta uchochezi na kwamba maamuzi ya mwisho yatatolewa na chama kupitia utaratibu uliowekwa.



No comments