HEADER AD

HEADER AD

MIKONONI MWA MANESI - 1

MIKONONI mwa manesi, wengi wetu tumepita,

Mikononi mwa manesi, uhai tulipopata,

Mikononi mwa manesi, na hawakutupepeta,

Wauguzi na manesi, mbarikiwe na Mungu.


Mikononi mwenu sisi, wengi ndimo tulipita,

Wa jadi pia manesi, sifa hizi wazipata,

Mlitutunza manesi, hadi sasa tunapeta,

Wauguzi na manesi, mbarikiwe na Mungu.


Mikononi mwa manesi, huduma tunazipata, 

Nyingi bila ukakasi, hatuhitaji kusuta,

Mwawajibika manesi, tunapoipatapata,

Wauguzi na manesi, mbarikiwe na Mungu.


Kinamama na manesi, mkono vidole pata,

Hasa kukiwa nafasi, ya watoto kuwapata,

Wapatana na manesi, furaha waweze pata,

Wauguzi na manesi, mbarikiwe na Mungu.


Tunapopata nafasi, huko tunapitapita,

Tukiwaona manesi, tutambue wakipita,

Wametuzalisha sisi, ndio sasa tunapeta,

Wauguzi na manesi, mbarikiwe na Mungu.


Kibidi kuwe nafasi, na Mungu wetu kuteta,

Alinde wetu manesi, huduma tuzidi pata,

Wasiipate mikosi, tukabaki twatepeta,

Wauguzi na manesi, mbarikiwe na Mungu.


Wako wachache manesi, sio wengi hao hata,

Watumiao nafasi, kutuacha tunasota,

Kila tukiita nesi, wao wajivutavuta,

Wauguzi na manesi, mbarikiwe na Mungu.


Nyie wachache manesi, kazi njema mmepata,

Kutuhudumia sisi, afya zikisitasita,

Tunawapenda manesi, maombi yetu mwapata,

Wauguzi na manesi, mbarikiwe na Mungu.


Hivyo jueni manesi, thawabu mtaipata,

Kazi yenu kwetu sisi, kwa Mungu heri mwapata,

Tusaidie manesi, afya tuweze kupata,

Wauguzi na manesi, mbarikiwe na Mungu.


Na haki zenu manesi, twafurahi mkipata,

Hizo zipande kwa kasi, mpate bila matata,

Nyumbani kuwe msosi, mijengo muweze pata,

Wauguzi na manesi, mbarikiwe na Mungu.


Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments