MSHUMAA
MSHUMAA utumike, uwake umalizike,
Vema sana utumike, hata mwanga umulike,
Wengine wafurahike, wenyewe utamatike,
Ewe mshumaa pole, kuwaka ni kujizika.
Giza lije wakutake, wakupate utumike,
Mwanga uje utoweke, ni taka wasikutake,
Na utake usitake, usibakie utoke,
Ewe mshumaa pole, kuwaka ni kujizika.
Bulldoza utumike, barabara ipitike,
Na tena wasikutake, kwenye lori ubebeke,
Wala isikanyagike, wewe ndio uondoke,
Ewe mshumaa pole, kuwaka ni kujizika.
Ni machozi yadondoke, mshumaa mnishike,
Mimi vipi nitumike, halafu nimalizike,
Wengine watajirike, hata vinono vilike?
Ewe mshumaa pole, kuwaka ni kujizika.
Nifanyeje nizimike, mshumaa nisiwake,
Isifike nitumike, na halafu nitoweke,
Nisipate sekeseke, mwanga wangu nijizike?
Ewe mshumaa pole, kuwaka ni kujizika.
Pole za kwako zifike, sikioni zisikike,
Magunia ujivike, msiba na uandike,
Hivi kwanini uwake, na ndio umalizike?
Ewe mshumaa pole, kuwaka ni kujizika.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment