TANESCO YABAINI KITUO CHA ENERGY OIL KINATUMIA UMEME KWA NJIA YA PANYA

Na Gustaphu Haule, Pwani
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Pwani limebaini kituo cha kuuzia mafuta ya petroli na dizeli cha Energy Oil kilichopo Kata ya Kongowe Manispaa ya Kibaha kuwa kinatumia umeme kwa njia ya Panya.
TANESCO wamekibaini kituo hicho katika oparesheni maalum ya kukagua mita za umeme kwa wateja wake iliyofanyika Agosti 20, 2025 katika maeneo hayo.
Akizungumza na Waandishi wa habari waliokuwepo katika oparesheni hiyo Mhandisi wa udhibiti mapato wa TANESCO mkoa wa Pwani Godfrey Nathan , amesema kuwa kitendo kilichofanywa na kituo hicho cha mafuta ni kinyume cha taratibu na Sheria za umeme .
Maafisa wa Tanesco, Waandishi wa habari wakiwa na afisa usalama wa kituo cha mafuta cha Energy Oil (Kulia) wakipiga Kambi kumsubiri meneja wa kituo hicho baada aliyekimbia baada ya kugundulika kituo chake kinatumia umeme kwa njia ya Panya.
Nathan amesema kuwa Agosti 20, 2025 walikuwa wanaendelea na zoezi la ukaguzi wa mita za umeme za wateja wao ikiwa ni utaratibu wa kawaida kama ulivyoelekezwa na shirika kuhakikisha mita za wateja zinatakiwa kukaguliwa mara kwa mara kuhakikisha utendaji wake ni fanisi na mapato hayapotei.
Amesema walipofika katika kituo cha mafuta cha Energy Oil kilichopo Kongowe wamekuta kuna uchepushaji wa umeme umefanyika katika mita yao huku kitendo sio sawa kwakuwa anakuwa anatumia umeme bila malipo na hivyo kulisababishia Shirika hasara.
Nathan ameongeza kuwa wakati wanafungua mita hiyo walikuwa pamoja na meneja wa kituo hicho lakini mara baada ya kufungua meneja huyo aliwaaga anakwenda Msikitini lakini hakuonekana mpaka muda wa kuondoka.
Amesema wakati anaondoka meneja huyo aliwaachia namba ya simu ya mkononi lakini kila walipojaribu kumpigia ili atoe ufafanuzi kwa Waandishi wa habari juu ya jambo hilo hakupokea na wala hakuonekana tena.
Amesema kuwa uchepushaji wa umeme sio jambo sahihi kwakuwa ni kinyume cha sheria na kuwa wote wanaojihusisha na vitendo hivyo waache mara moja .
Amesema TANESCO Mkoa wa Pwani bado inaendelea na oparesheni hiyo ya kukagua mita za umeme na endapo mtu yeyote atabainika atachukuliwa hatua na taratibu nyingine za kisheria ikiwemo kulipa gharama zote alizolisababishia Shirika.
Fundi wa upande wa udhibiti mapato TANESCO mkoa wa Pwani Damas Kimaro,amesema baada ya kufungua mita hiyo waliona umeme unatumika bila kupita kwenye mita.
Mmoja wa fundi umeme kutoka Tanesco Mkoa wa Pwani akiwaelekeza Waandishi wa habari namna mita hiyo ilivyochepushwa umeme na kituo cha Energy Oil.
Kimaro amesema baada ya kuona hali hiyo hatua ya kwanza ilikuwa ni kukata umeme na kisha kuendelea na taratibu zote za kisheria na kwamba watampigia hesabu na gharama zote ambazo shirika limepata hasara.
Amesema kituo hicho kilikuwa kinatumia uniti 4000 kwa mwezi na amekuwa akilipa kiasi cha Tsh. Milioni 4 kwa mwezi lakini kuanzia Mei mwaka huu matumizi hayo yakashuka mpaka kutumia Uniti 200 kwa mwezi sawa na Tsh.68000.
"TANESCO huwa inawasoma wateja wake wote kupitia mfumo maalum na huwa tunajua matumizi ya kila mteja kwa mwezi lakini tunapoona yameshuka huwa tunajiuliza na hatimaye kuchukua hatua ya kufuatilia na ndio maana hata kituo hiki tulipoona matumizi yameshuka kwa kasi ikabidi tuje tujridhishe na tulipokagua mita tukagundua amechepusha umeme,"amesema Kimaro
Nae msimamizi wa kitengo cha udhibiti mapato TANESCO mkoa wa Pwani John Nassari,amesema mteja anavyofanya kitendo cha kuchepusha umeme madhara yake ni makubwa kwa mteja mwenyewe na hata yule anayetumika kufanya hivyo.
Msimamizi wa kitengo cha udhibiti mapato TANESCO mkoa wa Pwani John Nassari akiwa eneo la kituo cha mafuta cha Energy Oil katika oparesheni ya ukaguzi wa mita za wateja wao.
Amesema kuwa madhara yake yanaweza yakasababisha mlipuko mkubwa ambao kwa namna moja au nyingine ukaleta madhara kwa jamii ya kuunguza nyumba zao na hata kuteketeza kwa kituo chenyewe
"Hiki ni kituo cha mafuta na kipo jirani na makazi ya watu na endapo pakatokea na mlipuko wowote madhara yake yanaweza kuwa makubwa kwani moto unaweza kusambaa haraka kutokana na nguvu ya Petroli na mafuta mengine na hivyo kuathiri makazi ya watu,"amesema
Meneja wa kituo hicho ambaye hakuweza kufahamika jina lake alikimbia eneo hilo baada ya TANESCO kugundua tatizo la uchepushaji umeme katika mita yake na hata alipojaribu kupigiwa kwa kutumia namba yake ya simu hakuweza kupokea.
Hata hivyo, afisa usalama wa kituo hicho ambaye alikuwa akishuhudia fundi wa TANESCO akikata umeme katika eneo hakuonyesha ushirikiano zaidi ya kusema msemaji wa kituo hicho amesafiri kwenda nje ya nchi hadi hapo atakaporudi.

~2.jpg)



Post a Comment