HEADER AD

HEADER AD

SERIKALI YATANGAZA KUPANDISHWA HADHI HALMASHAURI MJI WA BAGAMOYO

Na Gustaphu Haule, Pwani 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa, ametangaza rasmi kupandishwa hadhi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo na kuwa Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo.

Mchengerwa ametoa tamko hilo Agosti 22,2025 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Nia Njema, Wilayani Bagamoyo.

      Waziri wa Tamisemi Mohamed Mchengerwa akizungumza katika mkutano wa hadhara na Wananchi wa Bagamoyo katika viwanja vya Nianjema ,mkutano huo umefanyika Agosti 22,2025.

Mchengerwa amesema tangazo hilo linatokana na maelekezo rasmi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameridhia mabadiliko hayo muhimu kwa maendeleo ya wananchi wa Bagamoyo.

“Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza Halmashauri ya Bagamoyo ipandishwe hadhi kuwa Halmashauri ya Mji, ninyi sasa ni mji kamili na maandalizi ya mipango ya Mji yataanza mara moja,” amesema Mchengerwa.

Kwa kutekeleza agizo hilo, Waziri Mchengerwa amewaagiza wataalamu wa mipango kutoka Tamisemi kufika Bagamoyo na kuanza maandalizi ya kitaalamu ya upangaji wa mji huo.

    Wananchi wa Bagamoyo wakiwa katika mkutano wa hadhara wa Waziri wa Tamisemi uliofanyika Agosti 22,2025.

 Pia amemuagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi kuandaa tangazo rasmi katika Gazeti la Serikali kwa ajili ya kuthibitisha kisheria kupandishwa hadhi kwa Bagamoyo.

Katika hatua nyingine Mchengerwa amesema kuwa Serikali imetenga fedha kiasi cha Sh.bilioni 1 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya pamoja na miundombinu yake katika maeneo ya Bagamoyo.

Ametoa agizo kwa katibu mkuu wa Tamisemi kuhakikisha sh. milioni 700 zinapelekwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika eneo la Kisutu, pamoja na sh. Milion 300 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati mpya katika eneo la Kitame.

Pia ameielekeza Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kufanya mapitio ya kina ya mtandao wa barabara za Mji wa Bagamoyo ili kuandaa mpango wa kuongeza barabara za lami kwa ajili ya kuboresha usafiri, biashara na ustawi wa wakazi wa Mji huo mpya.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, aliwasilisha shukrani kwa niaba ya wananchi wa Bagamoyo kwa hatua mbalimbali za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

      Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza na Waandishi wa Bagamoyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Agosti 22,2025 katika viwanja vya Nianjema.

“Sisi wakazi wa Bagamoyo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia kwa kutufungulia fursa mpya za maendeleo kwani ameridhia kujenga Bandari ya Bagamoyo, reli ya SGR kutoka Bagamoyo hadi Kwala kwa ajili ya mizigo, pamoja na kituo cha kupoza umeme cha megawati 22 kilichopo Chalinze,” amesema Kunenge.

Hata hivyo, Kunenge ameongeza kuwa Serikali imeanza pia ujenzi wa barabara ya Makofia–Mlandizi kwa njia mbili hatua inayolenga kuboresha miundombinu ya usafiri katika mkoa huo na kukuza uchumi wa wananchi.

No comments