NIPE KAULI NJEMA

UNIPE kauli njema, katika mdomo wangu,
Nakuomba ya karima, kwa hekima mola wangu,
Mbele yako nasimama, nakuomba Mungu wangu,
Unipe kauli njema katika mdomo wangu,
Unikinge na shetani, uniingize peponi,
Uniepushe motoni, nifurahi kaburini,
Nakuomba kwa yakini, maisha yangu thamini,
Unipe kauli njema katika mdomo wangu,
Niyatamke mazuri, ya wewe kukupendeza,
Hakika na yenye heri, na mema kuendeleza,
Ninakuomba kahari, nipe ya kunipendeza,
Unipe kauli njema katika mdomo wangu,
Unipe maisha mema, duniani na Akhera,
Unijalie neema, unipe pia busara,
Unipe amali njema, pia na makazi bora,
Unipe kauli njema katika mdomo wangu.
Niepushe na dhuluma, unipe vyenye thamani,
Unikinge na lawama, nakuomba Rahamani
Unipe na mwisho mwema, Mungu wangu wa mbinguni,
Unipe kauli njema katika mdomo wangu
Mwishoni nimefikia, ipokei yangu dua,
Mengi nimeelezea, na wala siyo kwa ria,
Nimekuomba kwa nia, malipo natarajia,
Unipe kauli njema katika mdomo wangu.
Sirdody, 0675654955, AU 0762396923
Kijijichasoya@gmail.com
Post a Comment