HEADER AD

HEADER AD

ONA UNYASI SHITUKA


NYOKA anabaki nyoka, ileile sumu yake,

Ngozi itabadilika, wala siyo sumu yake,

Usinziaye amka, usife kwa sumu yake,

Vile alikuumiza, ona unyasi shituka.


Kama nyoka gamba lake, ndivyo anafanya yake,

Lifanya vituko vyake, hata wewe wakucheke,

Ikawa furaha yake, kukufanya upigike,

Vile alikuumiza, ona unyasi shituka.


Ulilia ukachoka, sababu ya mambo yake,

Hata mwili kupunguka, kwa mashambulizi yake,

Lifanya ukaanguka, kwa mbinu chafu zake,

Vile alikuumiza, ona unyasi shituka.


Sasa umeimarika, na kufanya usomeke,

Aja kule ametoka, kwamba tena akuteke,

Kwamba kasahaulika, alivyofanya uchoke,

Vile alikuumiza, ona unyasi shituka.


Huyo nyoka yuleyule, hatatoa gamba lake,

Sumu yake ilele, wala usidanganyike,

Akija muweke pale, usitake akushike,

Vile alikuumiza, ona unyasi shituka.


Kupiga mara ya kwanza, halali uadhirike,

Ugeni ulikuponza, kufanya ukamatike,

Sasa umeshajifunza, kwa janja asikushike,

Vile alikuumiza, ona unyasi shituka.


Kama ukiwa mzembe, ufanye usogeleke,

Waweza fanya tuimbe, mpeleke mpeleke,

Atafika akukombe, na mauti yakufike,

Vile alikuumiza, ona unyasi shituka.


Ulishang’atwa na nyoka, unyasi sitikisike,

Bila wewe kushituka, akung’ate uteseke,

Huko ni kuerevuka, ni kiunzi ukivuke,

Vile alikuumiza, ona unyasi shituka.


Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments