HEADER AD

HEADER AD

TOBO LIKISHAZIBIKA

NDOO iliyotoboka, huwa haijai maji,

Hata kukiwa masika, kamwe haijai maji,

Sababu unayaweka, ndoo haiyahitaji,

Tobo likishazibika, utakidhi mahitaji, 


Kweli una heka heka, kujaza unahitaji,

Ila yanachuruzika, kwa mchanga ni mtaji,

Hata jasho likitoka, ndoo tupu bila maji,

Tobo likishazibika, utakidhi mahitaji. 


Kombe tunalifunika, kuijaza ndoo siji,

Tobo bila kufunika, chini tunamwaga maji,

Kiu haitakatika, ndoo maji tahitaji,

Tobo likishazibika, utakidhi mahitaji. 


Ndoo iliyotoboka, kutaka kujaza maji,

Ni ng'ombe kukamulika, bila yake mahitaji,

Maziwa shida kudaka, hata uwe na mtaji,

Tobo likishazibika, utakidhi mahitaji. 


Mashudu kwa ng'ombe weka, magadi pia na maji,

Jinsi yatakavyotoka, maziwa tunahitaji,

Wazi utafurahika, kwa kazi siyo kipaji,

Tobo likishazibika, utakidhi mahitaji. 


Maji unayoyataka, kwako yawe ni mtaji,

Kitobo kikizibika, yakachuruzika maji,

Ujao utaupata, huo kwako ni mtaji,

Tobo likishazibika, utakidhi mahitaji. 


Fikira zilizochoka, zitazidi jaza maji, 

Akili ikishituka, kuziba ndio mtaji,

Au kama unataka, ndoo mpya tahitaji,

Tobo likishazibika, utakidhi mahitaji. 


Ni raha kutazamika, mtu akijaza maji,

Ndoo iliyotoboka, nayo ikimwaga maji,

Ila tunasikitika, jasho lilivyo bubuji,

Tobo likishazibika, utakidhi  mahitaji.


Ushauri wewe shika, kama unataka maji,

Jiridhishe kwa hakika, kwamba ndoo haivuji,

Mpira wa maji shika, pata unachohitaji,

Tobo likishazibika, utakidhi uhitaji. 


Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments