UZEE HAUKIMBIWI

UZEE haukimbiwi, Ujana historia,
Kukwepa huruhusiwi, ni lazima kupitia,
Si michezo ya Shimiwi, ya kwamba hutaingia,
Jiandae silemae, uzee unakujia.
Mwenyewe hutajiona, ila ndio wakujia,
Wenzako unawaona, pale walipofikia,
Na wao wanakuona, umri wakupitia,
Jiandae silemae, uzee unakujia.
Umejaliwa watoto, ujukuu waingia,
Furahia ni mvuto, ubani unakujia,
Hapo hakuna Mateto, ukubwa umefikia,
Jiandae silemae, uzee unakujia.
Unajipitia njia, barakoa watumia,
Watu wakuamkia, hata usiodhania,
Kwa macho waangalia, uzee ushafikia,
Jiandae silemae, uzee unakujia.
Njiani kijipitia, jina wanakupatia,
Babu tunalisikia, uzee ushaingia,
Wengine kiwatania, wasema ushaishia,
Jiandae silemae, uzee unakujia.
Acha ukiulizia, vipi hapo wafikie,
Nywele ukifukizia, ili ndevu kufichia,
Hizi na zile tumia, mbinu zitakuishia,
Jiandae silemae, uzee unakujia.
Watoto mejizalia, huko mnakutania,
Viti ulivyokalia, sasa wavishikilia,
Muda umeshawadia, acha vizia vizia,
Jiandae silemae, uzee unakujia.
Vijana wanakujia, busara kujipatia,
Siyo wajichagulia, miaka imetulia,
Yale uliyopitia, waweze kujifunzia,
Jiandae silemae, uzee unakujia.
Uzee kuufikia, ni neema ya Jalia,
Wachache wanafikia, ndio tunajivunia,
Hasa kama wasalia, vema wakiutumia,
Jiandae silemae, uzee unakujia.
Nami nimeshafikia, uzee nafurahia,
Mungu kumtumikia, ya dunia masalia,
Najibidisha sikia, nafsi weze tulia,
Jiandae silemae, uzee unakujia.
Na Lwaga Mwambande ( KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment