ZINGATIA USHAURI
KUWA na afya ya mwili, kunaboresha akili,
Kama ni dhofli hali, unavuruga akili,
Hebu tumia akili, ijenge afya ya mwili,
Zingatia ushauri, ufanye mambo sahihi.
Taaluma nzuri kweli, hutufungua akili,
Unene huwa dalili, kuleta magonjwa mwili,
Suala muhimu hili, vizuri kulijadili,
Zingatia ushauri, ufanye mambo sahihi.
Kimo chako ni halali, umeumbwa ni kamili,
Mahesabu ya akili, una uzito halali,
Wewe unasoma kweli, ila mkaidi kweli,
Zingatia ushauri, ufanye mambo sahihi.
Waambiwa huo mwili, punguza kilo kamili,
Wewe ni mbishi kweli, chakula kwako asali,
Unaziona dalili, unachokachoka kweli,
Zingatia ushauri, ufanye mambo sahihi.
Chakula ni sumu kali, katika kujenga mwili,
Vyakula vingine kweli, vitamu ndani ya mwili,
Lakini ni sumu kali, kwa unene kuabili,
Zingatia ushauri, ufanye mambo sahihi.
BMI kamili, iweke kwenye akili,
Ukaze wako msuli, usisubiri dalili,
Kwa matendo na kauli, iboreshe yako hali,
Zingatia ushauri, ufanye mambo sahihi.
Sisubiri uwe chali, kwa kupata gonjwa kali,
Nakusihi tafadhali, suala la muhimu hili,
Uthamini wako mwili, iwe nzuri yako hali,
Zingatia ushauri, ufanye mambo sahihi.
Tena nakwambia hili, sijaliona mahali,
Kiweka vizuri mwili, ukivaa nguo kali,
Wapendeza kweli kweli, wawa kamili kamili,
Zingatia ushauri, ufanye mambo sahihi.
Kuutunza wako mwili, ni kupenda yako hali,
Kusema chakula sili, jambo kawaida hili,
Si kila mara asali, inafaa kwenye mwili,
Zingatia ushauri, ufanye mambo sahihi.
Amua kutunza mwili, ni kujinyima kwa kweli,
Mazoezi ya msuli, kuacha lile na hili,
Fanya kama unasali, kwa kuzingatia kweli,
Zingatia ushauri, ufanye mambo sahihi.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment