ALLY HAPI AMUOMBEA KURA MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA KIBAHA HAMOUD , MGOMBEA URAIS DKT SAMIA

Na Gustaphu Haule, Pwani
KATIBU mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Taifa Ally Hapi amezindua kampeni ya CCM ya Jimbo la Kibaha Vijijini kwa kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo hilo Hamoud Jumaa pamoja na kumuombea kura mgombea wa Urais wa CCM Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Hapi amezindua kampeni hiyo Septemba 19,2025 iliyofanyika katika viwanja vya Mtongani vilivyopo Mjini Mlandizi katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini kampeni ambazo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama kutoka Wilaya ya Kibaha ,Mkoa na Taifa.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Taifa Ally Hapi ( kushoto)akimnadi mgombea wa ubunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa (Kulia) katika uzinduzi wa kampeni uliofanyika Septemba 19,2025 Mlandizi Kibaha.
Akizungumza na Wananchi pamoja na wanachama wa CCM waliojitokeza katika uzinduzi huo Hapi amesema kuwa ujio wake katika uzinduzi huo ni kufanya mambo mawili ikiwemo kumuombea kura Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mgombea ubunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa.
Hapi amesema kuwa Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan ameivusha nchi katika kipindi kigumu na alipata madaraka nchi ikiwa imefiwa lakini zipo nchi ambazo haziwezi kuvuka katika mtego huo kama haikupata kiongozi mahiri lakini Tanzania iliweza.
Amesema Dkt .Samia tangu achukue madaraka nchi imekuwa na amani ,watoto wanasoma,mambo ya maendeleo yanafanyika na kila mwananchi anafanya shughuli za kiuchumi kwa amani.
Amesema Rais Samia alipoingia madarakani alikuta miradi mikubwa ukiwemo ujenzi wa reli ya Mwendokasi ( SGR) Bwawa la kufua umeme Mwalimu Nyerere,kujenga madaraja makubwa na miradi mingine ya ujenzi wa Shule.
Amesema mradi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere umekamilika kwa asilimia 100 na mradi wa SGR sasa unatumia kusafirisha Watanzania kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na bado unaendelea kujengwa kuelekea mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Amesema kiongozi huyo CCM wamemleta tena na sasa wanamuombea kura kwa Wananchi ili ifikapo Oktoba 29 aweze kupigiwa kura na kwamba wanaposema Dkt.Samia anatosha na anasifa hawasemi kwa maneno kwani kazi kubwa ameifanya na wengi wameona.
Amesema ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025 /2030 inakwenda kujenga Bandari ya Bagamoyo na viwanda mbalimbali vitajengwa kwani Rais Samia amesema viwanda hivyo vitatoa ajira kwa vijana wa mkoa wa Pwani.
Amesema ndani ya siku 100 za Rais Samia mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa kiti cha Urais ameweka mikakati ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya maendeleo.
Amesema jambo la kwanza ni kupeleka umeme Vitongojini,kushughulika na tatizo la ajira kwa kuwawezesha Wananchi mitaji mbalimbali na atatenga Sh.bilioni 200 ili watu wapate mitaji.
Hapi amesema Serikali imejenga Zahanati na vituo vya afya lakini ndani ya siku 100 Dkt. Samia ataanza kutekeleza dhima ya bima ya afya kwa Watanzania wote na wataanza na wajawazito,wazee ,vijana na watoto.
Kuhusu magonjwa ya Kansa,Kisukari na Figo amesema ndani ya siku 100 matibabu ya magonjwa hayo Serikali itayabeba ili kuwapunguzia Wananchi wake ugumu wa maisha.
Ameongeza kuwa suala la kutoa maiti hospitalini nalo ni tatizo kubwa na Wananchi wamekuwa wakikwazika na jambo hilo na inatakiwa maiti izikwe kwa haraka lakini huwa inashindikana kutokana na maiti kuzuiliwa kwa ajili ya madeni lakini ndani ya siku 100 hakuna maiti ya kuzuiliwa hospitali yoyote Tanzania.
Aidha Hapi amesema yapo mambo mengi yatafanyika kupitia ilani hiyo na amewaomba wanaKibaha Oktoba 29 kura ya kwanza hiwe kwa Dkt.Samia na kura ya pili hiwe kwa mgombea wa ubunge Hamoud Jumaa.
Amesema ili Rais Samia afanikiwe anahitaji wabunge wazuri na mgombea mbunge wa Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa ni kiongozi mzuri ambaye anaweza kusaidiana na Rais kuleta maendeleo katika Jimbo la Kibaha Vijijini.
Naye mgombea wa ubunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa amewatoa wasiwasi Wakazi wa Jimbo la Kibaha Vijijini kwa kuwaambia kuwa mambo mazuri yanakwenda kutekelezwa katika jimbo hilo ndani ya miaka mitano ijayo.
Mgombea wa ubunge Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa (CCM) akizungumza na wanachama pamoja na Wananchi wa Jimbo hilo katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika Septemba 19 ,2025 Mjini Mlandizi.
Jumaa amesema kuwa kinachotakiwa ni kuhakikisha ifikapo Oktoba 29 ,2025 siku ya uchaguzi mkuu Wananchi wote wanakwenda kupiga kura kuchagua Rais anayetokana na CCM, Mbunge wa CCM pamoja na madiwani wake .
Hata hivyo,Jumaa amesema yupo tayari kuwatumikia Wananchi wa Jimbo la Kibaha Vijijini na miongoni mwa mambo ambayo anakwenda kuyafanyiakazi akiwa mbunge ni kujenga soko jipya la kufanyia biashara.
Wananchi wa Kibaha Vijijini wakiwa katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa Septemba 19/2025.
Post a Comment