HEADER AD

HEADER AD

TUSITWEZE KUOLEWA

Kuolewa si balaa, tusitolee unaa,

Kwa wanawake kwafaa, kwetu mila zimekaa,

Ila wale wenye njaa, wafanya kama vichaa,

Tusitweze kuolewa, kama kupatwa kwa jua.

Kwa jamii ukikaa, neno wanavyolivaa,

Kuna kejeli zajaa, kama zaleta fadhaa,

Ni kama anasinyaa, asubirie balaa,

Tusitweze kuolewa, kama kupatwa kwa jua.

Kinadada wamejaa, wanakatisha mitaa,

Mawazo yamewajaa, kwao lini watakaa,

Wao yabaki tamaa, kwa ndoa wapate kaa,

Tusitweze kuolewa, kama kupatwa kwa jua.

Unaweza kushangaa, wanaume wamekaa,

Wanawake wamejaa, wanaruka na mitaa,

Sasa ni hili balaa, watoto kutapakaa,

Tusitweze kuolewa, kama kupatwa kwa jua.

Ndoa iweze kukaa, watu wawili hukaa,

Upweke waukataa, pamoja waweze kaa,

Familia kuandaa, dunia iweze jaa,

Tusitweze kuolewa, siyo kupatwa kwa jua.

Watu ninawashangaa, maneno yamewajaa,

Matusi yanazagaa, kuolewa ni balaa,

Vizuri haijakaa, tena siyo ya kufaa,

Tusitweze kuolewa, siyo kupatwa kwa jua.

Mkeo hapo akaa, mwafanya yanayofaa,

Ndoa vipi inafaa, au kwako ni balaa?

Kama kwako inafaa, kuolewa kwa kufaa,

Tusitweze kuolewa, siyo kupatwa kwa jua.

Mwanaharakati kaa, mengine yatasinyaa,

Nyumbani yawa balaa, mabishano yanajaa,

Mbona mwaleta balaa, taasisi yachakaa,

Tusitweze kuolewa, siyo kupatwa kwa jua.

Kwenye ndoa nikukaa, heshima iweze jaa,

Mke na mume kukaa, mbele imulike taa,

Mema yapate kujaa, na harusi kuzagaa,

Tusitweze kuolewa, siyo kupatwa kwa jua.

Ndoa heshima kijaa, familia manufaa,

Kama dharau balaa, nyumba itaivagaa,

Bora akili kujaa, ndoa isijechakaa,

Tusitweze kuolewa, siyo kupatwa kwa jua.

Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments