KUTAFUTANA MUHIMU

MUME na mke sikia, hili lipate ingia,
Ndoa mmeshaingia, na humo mnasalia,
Mwenzako kumwangalia, Mungu anafurahia,
Kama mwaheshimiana, kutafutana muhimu.
Mwenzako kenda safari, wewe nyuma wasalia,
Kumtafuta vizuri, kuijua yake njia,
Kunyamaza ni sifuri, heshima hujafikia,
Kama mwaheshimiana, kutafutana muhimu.
Mwenzangu mefika wapi, ndivyo tunaulizia,
Na mwenzako awa hapi, unavyomfwatilia,
Usimuone makapi, yako unajifanyia,
Kama mwaheshimiana, kutafutana muhimu.
Vipi amekuuliza, hadi hapo kufikia,
Au keshakubeza, yake anaangalia,
Hilo jambo la kuwaza, na kazi kulifanyia,
Kama mwaheshimiana, kutafutana muhimu.
Jinsi mwaheshimiana, mambo ya kuangalia,
Na vile mnapendana, hili nasisitizia,
Lazima kutafutana, kule mwenza kafikia,
Kama mwaheshimiana, kutafutana muhimu.
Kama hajakutafuta, wala usijechukia,
Wewe unamtafuta, mbali kijisafiria,
Elimu umeshapata, kazi anza ifanyia,
Kama mwaheshimiana, kutafutana muhimu.
Kama hamtafutani, hili linaniingia,
Kuombeana sioni, jinale kujitajia,
Nasema huo uhuni, ni bora ukafifia,
Kama mwaheshimiana, kutafutana muhimu.
Vipi watu wapendana, vema ukaangalia,
Hali wanajualiana, huku wanafurahia,
Au wote wauchuna, jioni kusubiria,
Kama mwaheshimiana, kutafutana muhimu.
Siyo kulaumiana, hali kama wapitia,
Simufifi hujaona, mwenza kikufwatilia,
Muda kujirudi sana, kibao mgeuzia,
Kama mwaheshimiana, kutafutana muhimu.
Sasa ulipo anzia, simu ukimpigia,
Lengo hasa kumwambia, safari lipofikia,
Nawe utamsikia, jibu akikupatia,
Kama mwaheshimiana, kutafutana muhimu.
Usijekusubiria, kwamba atakupigia,
Wewe kazini ingia, kimpigiapigia,
Yako yatamuingia, ataanza kupigia,
Kama mwaheshimiana, kutafutana muhimu.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment