HEADER AD

HEADER AD

SAA 24 - ZIKUJENGE ZIBOMOE

WALE wamefanikiwa, na wasiofanikiwa,

Muda wao uko sawa, na Mungu wamegawiwa,

Kile kinaangaliwa, jinsi unavyotumiwa,

Saa ishirina nne, zikujenge zibomoe.


Wengine hufanikiwa, kwa muda waliopewa,

Kufanya ya uelewa, sasa ndio wapepewa,

Si pesa wanagawiwa, na keki kuandaliwa,

Saa ishirina nne, zikujenge zibomoe.


Ratiba yaandaliwa, vizuri yashikiliwa,

Mipango inapitiwa, mchakato yafanyiwa,

Mbinu zinaibuliwa, za malengo kufikiwa,

Saa ishirina nne, zikujenge zibomoe.


Tasema wamejaliwa, tena wamebarikiwa,

Kama wanadondoshewa, vile wanafanikiwa,

Kumbe yanaandaliwa, nao si ya kupangiwa,

Saa ishirina nne, zikujenge zibomoe.


Saa hizo umepewa, kama vile amepewa,

Ni vipi zinatumiwa, hesabu itatolewa,

Huko ni kufanikiwa, au kutofanikiwa,

Saa ishirina nne, zikujenge zibomoe.


Kazi umeshapangiwa, na afya umejaliwa,

Kila mara wapitiwa, himizwa wasumbuliwa,

Hapo utatobolewa, useme hujajaliwa,

Saa ishirina nne, zikujenge zibomoe.


Talanta umepatiwa, vile ulivyojaliwa,

Na akili umepewa, zatakiwa kutumiwa,

Metulia kama ziwa, mawimbi unapepewa,

Saa ishirina nne, zikujenge zibomoe.


Habari twasimuliwa, za waliofanikiwa,

Si kwamba walizaliwa, tayari wafanikiwa,

Nao walikamuliwa, hamu hawakuishiwa,

Saa ishirina nne, zikujenge zibomoe.


Maisha umepatiwa, hata afya mejaliwa,

Hakuna wa kuchelewa, hili ukilielewa,

Anza huwezi zuiwa, mwisho utafanikiwa,

Saa ishirina nne, zikujenge zibomoe.


Yule amefanikiwa, nini alichojaliwa,

Wewe hujafanikiwa, wapi unapozibiwa,

Mungu muda amegawa, kwetu sote sawa sawa,

Saa ishirina nne, zikujenge zibomoe.


Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments