HEADER AD

HEADER AD

WAINUE WAVULANA


NI waraka kwa wazazi, na watoto wa kiume,

Ya kwamba mnayo kazi, ili wao wasimame,

Kazi yenyewe malezi, hizi nyakati zisome,

Wainue wavulana, sawa nao wasichana. 


Maisha ya siku hizi, sisi sote tujipime,

Nani wapata malezi, wa kike na wa kiume?

Nani wafundishwa kazi, ili kesho wasimame?

Wainue wavulana, sawa nao wasichana.


Kimataifa ni wazi, machapisho tuyasome,

Msimamo uko wazi, si kificho tuusome,

Wahitajio malezi, watoto gani tuseme,

Wainue wavulana, sawa nao wasichana.


Watoto yao malezi, ilo sawa tuiseme,

Chini mitano ni wazi, wanasemwa wasizame,

Baada ya hapo wazi, wa kike si wa kiume,

Wainue wavulana, sawa nao wasichana.


Yale mambo ya uzazi, si watoto wa kiume,

Msisitizo ni wazi, wale wapigiwa shime,

Lafanyika waziwazi, wala hilo lisikome,

Wainue wavulana, sawa nao wasichana.


Wavulana wameachwa, acha namba wazisome,

Siyo wao wameachwa, hili budi tuliseme,

Ni kizazi kimeachwa, ili mwishowe kikome,

Wainue wavulana, sawa nao wasichana.


Majukumu familia, yao wote tuyaseme,

Miaka inapotimia, chansi zao wasimame,

Kutumikia dunia, kama hasa wanaume,

Wainue wavulana, sawa nao wasichana.


Kwamba jinsi wanakua, wale nini wanaume,

Nini wapaswa kujua, familia isimame,

Nini waweza fukua, waishi na wasizame,

Wainue wavulana, sawa nao wasichana.


Nafasi yao ni ipi, hasa hasa wanaume,

Yakiwasibu ni wapi, nao waende waseme?

Ni vipi nao wakopi, na kufanya wajitume,

Wainue wavulana, sawa nao wasichana.


Dunia hii ni yetu, wa kike na wa kiume,

Hivyo ni wajibu wetu, wote hao wasimame,

Ya kwamba kizazi chetu, kidumu na kisizame,

Wainue wavulana, sawa nao wasichana.


Mtumzi wa shairi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments