RC PWANI AKABIDHI MAGARI 12, MITAMBO ,BOTI JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI
Na Gustaphu Haule, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amekabidhi mitambo ,magari 12 na boti moja kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji la mkoa huo yenye thamani ya Tsh. Bilioni 7.9.
RC amekabidhi vifaa hivyo Oktoba 24/2025 kwa kamanda wa kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa mkoa wa Pwani Jenifa Shirima katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Pwani iliyopo Manispaa ya Kibaha.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akikagua baadhi ya mitambo ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika hafla hiyo.Hafla hiyo imehudhuriwa na watendaji wengine mbalimbali akiwemo Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Pili Mnyema, Sekretarieti ya Mkoa wa Pwani pamoja na askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji la Mkoa huo.
Akizungumza kabla ya kukabidhi vifaa hivyo Kunenge ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha vitendea kazi vya vyombo vya ulinzi na usalama hususani Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Kamanda wa kikosi cha Zimamoto na Uokoaji wa Mkoa wa Pwani Jenifa Shirima (mwenye sare Kulia) akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mitambo , magari na boti moja katika hafla iliyofanyika Oktoba 24/2025 katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ( Katikati) na kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Pili Mnyema.Amesema upatikanaji wa magari na boti hizo utaimarisha uwezo wa Jeshi hilo katika kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuokoa maisha na mali za wananchi wakati wa majanga ya moto na maafa ya majini.
“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika vifaa vya uokoaji na uboreshaji huu utasaidia kuongeza ufanisi katika kazi za zimamoto na kuimarisha usalama wa wananchi wetu", amesema Kunenge.
Aidha, Kunenge amelipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji la Mkoa wa Pwani kwa kazi nzuri ya kupambana na matukio ya moto na majanga mbalimbali ambapo amesema upatikanaji wa vifaa itawaongezea ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Pwani, Jenifa Shirima, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kulipa jeshi hilo kipaumbele katika upatikanaji wa rasilimali na vifaa muhimu.
Kamanda wa Kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa Mkoa wa Jenifa Shirima akimuelezea Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge matumizi ya boti jipya katika hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo iliyofanyika Oktoba 24/2025.Amesema magari na boti vilivyokabidhiwa vitasaidia kwa kiasi kikubwa katika majukumu ya uokoaji, ikiwemo usafirishaji wa wagonjwa, kudhibiti moto, na kutoa huduma za haraka katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani.
“Vifaa hivi vitasaidia kuongeza kasi ya majibu wakati wa dharura na kupunguza madhara yanayosababishwa na majanga ya moto na ajali hivyo tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhimu wa kuboresha huduma za zimamoto nchini,” amesema Kamanda Shirima.
Hatahivyo makabidhiano hayo ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuhakikisha taasisi za ulinzi na usalama zinakuwa na vifaa vya kisasa vinavyowezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Baadhi ya magari na mitambo kama inavyoonekana pichani
Kamanda wa Kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa Mkoa wa Pwani Jenifa Shirima akimuongoza Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge kukagua mitambo na magari mapya ya Jeshi hilo katika hafla iliyofanyika Oktoba 24/2025 katika viwanja vya Mkuu wa mkoa wa Pwani.






Post a Comment