>>Inadaiwa chanzo cha mauaji mme alitaka ahusike kuhesabu kwenye tathmini na siyo mke wake
>>Nyumba ya Marehemu ni miongoni mwa nyumba zinazotarajiwa kufanyiwa uthamini kupisha ujenzi wa uwanja wa ndege .
>>Polisi yamshikilia Meneja TARURA mme wa marehemu
DIMA Online, Serengeti
SIMANZI , Majonzi vyatawala kwa wana familia, ndugu, jamaa, marafiki na majirani kutokana na kitendo cha kikatili cha mauaji aliyotendewa Rhoda Jonathan mwenye umri wa miaka (44) .
Rhoda alikuwa mke wa Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) mkoa wa Kagera , Mhandisi Wilson Charles.
Makazi ya Rhoda na familia yake ni katika Kitongoji cha Burunga, Kata ya Uwanja wa Ndege wilayani Serengeti, mkoani Mara .
Nyumbani kwa marehemu Rhoda Jonathani katika Kitongoji cha Burunga, kata ya Uwanja wa Ndege , wilayani Serengeti.
Rhoda alivamiwa nyumbani kwake na watu ambao hawakutambuliwa majina yao wala sura zao . Mmoja akiwa na panga lililonolewa aliingia chumbani mwa Rhoda na kumfanyia unyama hadi kuondoa uhai wake .
Imeelezwa kwamba wauwaji walitekeleza tukio hilo la kinyama kati ya saa moja na saa mbili usiku, siku ya alhamis , tarehe 23, 2025, na kumkatakata kwa mapanga katika sehemu mbalimbali za mwili huku kiganja chake cha mkono kikikutwa chini ya sakafu na mwili pembeni mwa kitanda.
Polisi walifika nyumbani na kuukagua mwili wa marehemu, kisha kuubeba na kuupeleka kuuhifadhi katika chumba cha kuhifadhia maiti, hospitali ya wilaya ya Serengeti . Mwili umehifadhi hadi sasa ukisubiri taratibu zingine kwa ajili ya mazishi.
Ni majonzi yasiyoweza kuzuilika kwani ukiutazama mwili wa marehemu Rhoda hautoweza kurudia kuutizama zaidi na zaidi kwani umejaa majeraha makubwa.
Sehemu za mwili wake ni majeraha, amekatwa na kuondolewa kiganja cha mkono wake wa kulia, katika mkono huo amekatwa na kuondolewa nyama sehemu ya mkono.
Mkono wa kushoto nao umekatwa na kuondolewa nyama sehemu ya mkono huo. Kifuani na kwenye matiti kumekatwakatwa na kuondolewa nyama sehemu ya maeneo hayo na majeraha mengine katika sehemu za mwili wake.
Chanzo cha Mauaji
Habari zinasema kwamba fidia ujenzi wa uwanja wa ndege Serengeti huenda ikawa chanzo cha kifo cha Rhoda .
Inasemekana kwamba mme wa Rhoda alitaka yeye ndiye ahesabu mali kwenye tathmini na siyo mke wake, licha ya kumtelekeza kwa zaidi ya miaka mitano.
Inaelezwa kwamba mke alipinga mmewe kuhesabu kwenye tathmini bali yeye ndiye ahusike kuhesabu, kwani mme ana mke zaidi ya mmoja na kila mke amemjengea nyumba yake jambo lililopelekea kutoelewana kwa wanandoa hao.
Marehemu Rhoda Jonathani enzi ya uhai wake.
Kitongoji cha Burunga anakoishi marehemu ni miongoni mwa vitongoji ambavyo wananchi wanatarajia kufanyiwa tathmini na serikali kwa ajili ya kulipwa fidia ili kupisha maeneo hayo kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege.
Inaelezwa kwamba mme wa marehemu , Wilson Charles alimnunulia mkewe uwanja na kumjengea nyumba. Hata hivyo mke aliendeleza nyumba hiyo kwa kujenga uzio na nyumba nyingine .
Inaelezwa kwamba Rhoda alikataa na kudai mmewe akipata fidia hatoweza kumpatia jambo lililoibua mgogoro kati yao na kwamba huwenda ikawa ndio chanzo kilichopelekea kifo chake.
Utata kifo cha Rhoda
John Jonathani Mobe mkazi wa Kijiji cha Nyangoto - Nyamongo ni kaka wa marehemu anasema mdogo wake kabla ya kuuawa alimpigia simu kumjulisha kwamba kuna zoezi la tathmini linataka kufanyika ili walipwe fidia kupisha ujenzi wa uwanja wa ndege.
John Jonathani Mobe mkazi wa Kijiji cha Nyangoto - Nyamongo kaka wa marehemu akizungumza.
" Alinipigia simu akanieleza kwamba kuna tathmini inataka kufanyika ila yeye haelewani na mme wake . Rhoda alisema kwamba mme wake amemwambia asifanye chochote kwakuwa mji ni wake .
" Siku moja kabla ya kifo cha mdogo wangu alikuwa hapa Nyamongo kwenye harusi . Mdogo wangu alipigiwa simu na mtu asiyemfahamu kwamba anatakiwa akasaini fomu ya uthamini. Akaondoka akaenda kwake, usiku akavamiwa nyumbani wakamuua.
" Tulipofuatilia kama kuna uthamini tuligundua ilikuwa ni uongo na wala hakumfahamu aliyempigia alikuwa ni nani. Hivyo kutokana na ugomvi wa ndoa ya mdogo wangu inatupa mashaka juu ya kifo chake huwenda mmewe anajua kinachoendelea" amesema John .
" Ndoa yao imekuwa na shida kwa muda mrefu mmewe alimtelekeza kwa zaidi ya miaka mitano, amekuwa akiishi mwenyewe na watoto wake ,sisi ndugu zake ndio tulikuwa tunamsaidia.
Mkazi wa Kitongoji cha Burunga, Kata ya Uwanja wa Ndege , Sesilia Matinde anasema kwamba waliotekeleza mauaji walifika nyumbani kwake kabla ya kwenda nyumbani kwa Rhoda kufanya mauaji.
Mkazi wa Kitongoji cha Burunga, Kata ya Uwanja wa Ndege , Sesilia Matinde akizungumza.
" Huwenda mimi ndio ningekufa , kwasababu wale waliomuua mama Agata walianzia nyumbani kwangu , mimi nikiwa kwenye shughuli zangu nyumbani nilimwacha msichana wa kazi.
" Msichana wangu wa kazi aitwae Ester aliniambia unajua hao watu walianzia hapa nyumbani walikuwa watatu ,walikuja wakiwa kwenye pikipiki mmoja akiwa ameshikilia panga, wakaniuliza hapa ni kwa nani? nikawaambia ni kwa mama Rhoda.
" Mmoja akapiga simu akisema Bosi tuko kwa mama Rhoda ,yule mtu kwenye simu akamwambia sio hapo nenda kwa Rhoda huyo ni mama Rhoda, nenda kwa Rhoda yaani kwa Injinia Wilson ,wakaondoka.
" Muda sio mrefu tukapata taarifa kuwa Rhoda ameuawa. Rhoda alikuwa jirani yetu mwema sana ,mimi ni mkazi wa kwanza kwenye hiki Kitongoji sijawahi kuona tukio kama hili, tunaomba serikali iwakamate waliohusika ili kitendo hiki kisiwe endelevu" anasema Sesilia.
Ndoa ya Rhoda na mmewe
Kumekuwepo na sintofahamu kuhusu ndoa ya Rhoda na mmewe Eng. Wilson . Baadhi wanasema kwamba Rhoda si mke halali wa Wilson kwamba walishaachana miaka 10 iliyopita hivyo si mke halali .
Wengine wanasema kwamba Marehemu Rhoda alikuwa mke halali wa Eng. Wilson isipokuwa walitofautiana, na kwamba si kweli wameachana kwa zaidi ya miaka kumi kwani mtoto wa mwisho ana umri wa miaka saba na tangu watengane Rhoda hakuwahi kuzaa mtoto mwingine nje ya ndoa.
Ester Jonathan Mobe ni mama mzazi wa marehemu anasema kwamba mwanae ni mke halali wa Eng. Wilson,walifunga ndoa na hawakuwahi kuachana kwa talaka wala mme kumshika ugoni mkewe.
Ester Jonathan Mobe ni mama mzazi wa Rhoda Jonathan.
" Nani anayesema kwamba mwanangu si mke halali? Wilson alikuwa na mke wa kwanza ambaye waliachana kwa Talaka , alimuoa mwanangu kwa ndoa ya kidini. Rhoda na Wilson walifunga ndoa mwezi Desemba, 2005 katika Kanisa la Waadventista Wasabato, Nyangoto hapa Nyamongo.
" Rhoda na mmewe wameishi hapo Serengeti kwenye mji wao tangu mwaka 2009 . Rhoda hajaachana na mme wake isipokuwa mme wake alimtelekeza, akawa hampatii matumizi ,kaka zake ndio wamekuwa wakimsaidia hata kumsomeshea watoto " amesema Ester.
Telesia Chacha Maginga ambaye ni dada wa mme wa Rhoda anasema kwamba anamtambua Rhoda kama mke wa kaka yake na kwamba hawajaachana ni wanandoa.
Telesia Chacha Maginga ambaye ni dada wa mme wa Rhoda akizungumza.
"Mimi naishi hapa Burunga wifi ni jirani yangu siku ya tukio niliitwa nikaambiwa wifi yangu ameuawa . Kaka yangu hakuwa ameachana na wifi alikuwa anakuja na kwenda mara ya mwisho kumuona kaka hapa kwakwe ni mwaka jana .
" Kaka amezaa na Rhoda watoto watatu . Siwezi kujua kama walikuwa na ugomvi nachofahamu mimi walikuwa ni wanandoa na hata uwanja kaka ndio alinunua na nyumba ndio alimjengea" anasema Telesia.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Burunga, Kata ya Uwanja wa Ndege, James Makuru Marwa, anasema kwamba yeye ni mkazi katika Kitongoji hicho kwa zaidi ya miaka 20 na kwamba anatambua Rhoda na Eng. Wilson walikuwa wanandoa.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Burunga, Kata ya Uwanja wa Ndege, James Makuru Marwa
" Sisi hapa kwenye Kitongoji tunatambua Rhoda na Eng. Wilson ni wanandoa ,yaani mtu akitaka kwenda nyumbani kwake ukiuliza kwa Eng. Wilson unaletwa hadi hapa kwa mama Agata (Rhoda).
" Siwezi kujua mambo ya ndoa yao ila nachokifahamu mimi kwenye kitongoji chetu nina miaka kati ya tano au sita sijawahi kumuona tena Eng. Wilson hapa kwenye Kitongoji chetu.
Mwenyekiti agusia zoezi la uthamini
Mwenyekiti anasema suala la uthamini lipo isipokuwa bado tathmini haijaanza kwenye kitongoji chake na kwamba nyumba ya Eng. Wilson na mkewe ni miongoni mwa nyumba zitakazofanyiwa uthamini.
" Suala la kuhamisha watu kwa ajili ya kupisha ujenzi wa uwanja wa Ndege lipo na tathmini imeanza tangu juzi imeanzia kwenye kitongoji jirani cha Kyambahi . Siku ya Alhamis tarehe, 16,2025 watu wa uthamini walinichukua tukazunguka nao kwenye maeneo wanasema hapa pako ndani ama hapa pako nje na nyumba ya Marehemu ipo ndani itatasminiwa
" Siku ya jumanne, tarehe 21october, 2025 tulikaa mkutano wa wananchi kuzungumzia jambo lililopo mbele yetu la tathmini, siku ya alhamis tarehe , 23 ndio huyu mama aliuwawa, yaani inasikitisha sana" anasema Mwenyekiti.
Wasemavyo ndugu wa mme
DIMA online imezungumza na baadhi ya ndugu wa mme kama wanafahamu chochote juu ya tukio hilo la mauaji lakini wamesema hawafahamu chochote . Kijana mmoja wa kiume ambaye ni kijana mkubwa wa mme wa Rhoda anasema ;
" Mimi ni kijana mkubwa wa Wilson ila sifahamu chochote kwasababu mimi nimefika muda sio mrefe , labda uongee na yule mzee ndio msemaji wa familia" anasema kijana mkubwa wa Eng. Wilson.
Ndugu mwingine wa mme naye anasema " Nami nimefika muda sio mrefu ,sijui chochote labda uzungumze na wenyeji wa hapa" anasema ".
Serikali yamshikilia Meneja TARURA
DIMA Online imewasiliana na mkuu wa wilaya ya Serengeti, Anjelina Lubella nakuthibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba tukio hilo lipo kwenye uchunguzi , uchunguzi ukikamilika atatoa taarifa.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mara, Pius Lutumo amesema Jeshi la Polisi linamshikilia Wilson Mwita Charles mwenye umri wa miaka (53) Mkazi wa Kitongoji cha Burunga ,kata ya Uwanja wa Ndege wilayani Serengeti kwa tuhuma za mauaji ya Rhoda Jonathani .
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mara, Pius Lutumo kizungumza.
" Tarehe 23, Oktoba, 2025 majiara ya saa moja usiku huko Kitongoji cha Burunga, Rhoda Jonathani (42) aliuwawa kwa kukatwa katwa na kitu chenye ncha Kali sehemu mbalimbali za mwili wake . Baada ya mtu/watu kuruka ukuta wa nyumba yake na kutekeleza mauaji hayo.
Kamanda Pius amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Polisi kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia u
Serikali ya Tanzania ilitenga zaidi ya Tsh. Bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wilayani Serengeti.
Februari , 27, 2025 , Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ilitilia saini na kampuni ya Saba Engineering mkataba wa kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wilayani Serengeti.
Taarifa ya Polisi
Post a Comment