HEADER AD

HEADER AD

KOSA KUBWA USIPIME

UKIMWITA mwanaume, kwamba yeye mwanamke,

 Kosa kubwa usipime, sitake akasirike, 

Kwa haraka ujitume, kama radhi umtake, 

Uumbaji wake Mungu, usifanyiwe mzaha.


Hivyo hivyo mwanamke, alivyo usimcheke,

Eti mwite dume jike, ufikirie acheke,

Hiyo radhi umtake, asamehe aridhike,

Uumbaji wake Mungu, usifanyiwe mzaha.


Wapo watu niwasute, na mwisho mwisho wafike,

Kuleta habari tete, wengine wakasirike,

Neno baya lisipite, na kinywani lisitoke,

Uumbaji wake Mungu, usifanyiwe mzaha.


Mwanaume ajipenda, akivalia atoke,

Apate wa kumpenda, pete kwao zivalike,

Tena Mungu akipenda, wazae wana wacheke,

Uumbaji wake Mungu, usifanyiwe mzaha.


Ukimwona vile alivyo, sifanye akasirike,

Umdharau alivyo, kulingana mwanamke,

Hayo maneno ya hivyo, na kwako yasisikike,

Uumbaji wake Mungu, usifanyiwe mzaha.


Yeye kaumbwa alivyo, mapenzi ya Mungu wake,

Nawe meumbwa ulivyo, pia ni mapenzi yake,

Mheshimu hivyo hivyo, mabaya usitamke,

Uumbaji wake Mungu, usifanyiwe mzaha.


Chuki unayoiunda, kudharau mwanamke,

Mwanaume kumponda, ya kwamba ni mwanamke,

Mke hawezi kupenda, kwamba yeye teketeke,

Uumbaji wake Mungu, usifanyiwe mzaha.


Au huyo mwanamke, ukimwita dume jike,

Mume adharaulike, duni yeye aoneke,

Sio mambo utapike, na kwa watu yasikike,

Uumbaji wake Mungu, usifanyiwe mzaha.


Mtu na aheshimike, hii na ifahamike,

Uumbaji siyo wake, amefanya Mungu wake,

Hebu umwache atoke, sifanye aghabike,

Uumbaji wake Mungu, usifanyiwe mzaha.


Ila nawe mwanaume, kuishi ka mwanamke,

Mke kuwa kama mume, kwenye jamii itoke,

Kila mtu ajitume, kwa Mungu asiumbuke,

Uumbaji wake Mungu, usifanyiwe mzaha.

Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments