HEADER AD

HEADER AD

MABALOZI WAKAGUA MIRADI YA MAENDELEO INAYOTEKELEZWA NA SHIRIKA LA ELIMU

Na Gustaphu Haule, Pwani 

MABALOZI wanne wa nchi za Nordic wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania  wamefanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Shirika la Elimu Kibaha lililopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

Ziara ya Mabalozi hao imefanyika Oktoba 10,2025  katika Shirika hilo ikiwa ni sehemu ya kuendeleza ushirikiano kati ya nchi za Nordic na Serikali ya Tanzania kwakuwa ndio nchi ambazo zilianzisha kwa pamoja Shirika la Elimu Kibaha chini ya Hayyat Julius Kambarage Nyerere.

Mabalozi waliotembelea Shirika hilo na nchi zao kuwa ni balozi Tone Tinnes kutoka nchi ya( Norway), Balozi Jesper Kammersgaad kutoka nchi ya (Denmark),Balozi Charlotta ozaki Macias kutoka nchini (Sweden) na Balozi Theresa Zitting kutoka nchini (Finland).

        Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha Robert Shilingi ( katikati) akiwa katika picha ya pamoja na mabalozi wa nchi za Nordic na baadhi ya watumishi wa Shirika hilo.

Wakiwa katika Shirika la Elimu Kibaha mabalozi hao walipokea taarifa mbalimbali za miradi ya maendeleo kutoka kwa Mkurugenzi wa Shirika hilo Robert Shilingi na kisha kutembelea miradi mitano muhimu hususani katika elimu.

Miongoni mwa miradi waliyoitembelea ni Shule ya msingi Tumbi, Shule ya vipaji ya Sekondari Kibaha ( Kibaha Boys),Chuo cha ufundi cha maendeleo ya Wananchi ( FDC),Shule ya Sekondari ya wasichana Tumbi na Shule ya Sekondari ya Kata ya Tumbi.

Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha Robert Shilingi amesema kuwa Shirika hilo lilianza mwaka 1963 kwa ushirikiano wa nchi nne za Nordic chini ya Hayyat Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo wakati huo lilikuwa likiitwa Nordic Tanganyika Project na lilizinduliwa rasmi mwaka 1964.

Shilingi amesema kuwa malengo ya kuanzisha Shirika hilo lilikuwa ni kupambana na mambo makubwa  matatu ikiwemo kupiga vita Ujinga,Maradhi na Umaskini ambapo kwa kiasi kikubwa ilikuwa ndoto ya Hayyat Julius Kambarage Nyerere.

Amesema mwaka 1970 jina lilibadilika kutoka Nordic Tanganyika Project na kuitwa Kibaha Education Centre (KEC) Shirika la Elimu Kibaha kituo ambacho hadi sasa kinasimamiwa na ofisi ya Rais Tamisemi.

Shilingi asema mafanikio ya kituo hicho ni makubwa kwani awali walianza na shule moja ya Msingi na Shule moja ya Sekondari lakini kwasasa wanashule za Sekondari tatu na maendeleo yake yapo vizuri.

      Mabalozi wa nchi za Nordic wakimsikiliza mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Tumbi kuhusu suala la utafiti wa masuala ya Kilimo na uzalishaji wa mazao mbalimbali ya bustani.

Amesema  kwasasa anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt .Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kulisaidia Shirika hilo kwani amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya Shirika hilo .

Amesema amefurahishwa na  ujio wa Mabalozi hao kwakuwa  ni sehemu ya kuzidi kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na nchi za Nordic hususani katika kuhakikisha ndoto za waanzilishi wa shirika hilo zinatimia.

Kwa upande wake balozi wa Sweden nchi Tanzania Charlotta ozaki Macias amesema lengo la kufanya ziara hiyo ni kwajili ya kukagua maendeleo ya Shirika hilo na hatua lilipofikia tangu kuanzisha kwake.

Macias amesema kuwa  nchi za Nordic zinafurahi kuona malengo ya uanzishwaji wa Shirika hilo yanazidi kuimarika kwakuwa hali ya sasa tofauti na wakati ambao shirika hilo lilianzishwa.

Amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuweza kulisimamia vizuri Shirika hilo hususani katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya elimu na kwamba wao wataendelea kulisaidia Shirika hilo ili kusudi liweze kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

Hata hivyo,amesema nchi Nordic zinatamani kuona Shirika hilo linazidi kuimarika zaidi na kwamba nchi za Nordic zitaendeleza ushirikiano na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha malengo ya kuanzisha Shirika hilo yanakuwa endelevu.

Mabalozi wa nchi za Nordic ikiwemo Norway, Sweden, Denmark na Finland katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kikao na watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha kilichofanyika Oktoba 10,2025 Kibaha Pwani.


No comments