KHADIJA RUNGWE AWAOMBA WANANCHI WASIANGALIE CHAMA WACHAGUE MTU AMBAYE ATAWALETEA MAENDELEO

Na Gustaphu Haule, Pwani
MGOMBEA wa ubunge wa Jimbo la Kibaha Mjini kupitia tiketi ya Chama Cha Ukombozi wa Umma ( CHAUMMA) Khadija Rungwe, amewaomba wananchi kuacha mazoea ya kuchagua chama na badala yake wachague mtu ambaye anaweza kuwaletea maendeleo.
Amesema yeye ni kiongozi makini na mwenye nguvu ambaye anaweza kuwatumikia Wananchi wa Jimbo la Kibaha Mjini kwahiyo ifikapo Oktoba 29,2025 wakampigie kura ili aweze kuwa mbunge wao.
Khadija ametoa kauli hiyo Oktoba, 11, 2025 wakati akizungumza na Wananchi wa Mtaa wa kwa Mfipa Kata ya Kibaha Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni ya mgombea wa udiwani wa Kata hiyo Hamo Machapula.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kibaha Mjini kupitia tiketi ya Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Khadija Hashim Rungwe akisalimiana na Wananchi mara baada ya kumaliza mkutano wake wa kampeni uliofanyika Oktoba 11,2025 katika eneo la Kwa Mfipa Kata ya Kibaha Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.Amesema yeye hawezi kuwa mbunge wa kusinzia wala kupiga makofi lakini atakwenda bungeni kwa ajili ya kuwasemea wananchi wa Jimbo la Kibaha Mjini pamoja na kuhakikisha anatatua changamoto zilizopo.
Amesema kuwa anatambua Jimbo la Kibaha Mjini lina changamoto nyingi lakini pia Kibaha ni sehemu ambayo imejaaliwa ardhi na kila kitu kinachohitajika kuifanya Kibaha hiwe na maendeleo.
Khadija amesema kuwa Kibaha ina barabara kubwa inayotumika kupita kwenda mikoa mbalimbali na hata nchi za jirani na kwamba hiyo pekee tayari ni fursa lakini viongozi waliopo madarakani wameshindwa kuwasimamia Wananchi wake.
Amesema afya hairidhishi ,hospitali hazitoshi na madawa hakuna kwani mwananchi akiumwa anapata wasiwasi kwasababu hana uhakika kama akifika hospitali anaweza kulipia vipimo na kupata dawa.
Mgombea ubunge Jimbo la Kibaha Mjini kupitia Chama Cha Ukombozi wa Umma( CHAUMMA ) Khadija Hashim Rungwe akimuunga mkono mmoja wa wafanyabiashara wa viazi na mihogo wa eneo la kwa Mfipa.Kuhusu suala la elimu Khadija amesema kuwa michango imekuwa mingi shuleni,walimu hawatoshi, mazingira ya wanafunzi hayafurahishi na elimu inayotolewa haina kiwango.
Amesema ifike mahali Wananchi waseme inatosha na wamchague yeye kuwa mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini ili aende akasimamie vizuri elimu kwakuwa ndio msingi wa kesho ili watoto wapate elimu na waweze kujitafutia fursa za kimaendeleo.
Amesema kuwa wafanyabiashara wengi mitaji yao haikui na wengine biashara zao zinakufa na hivyo kukosa maendeleo lakini maendeleo yanatokana na viongozi kuwa makini .
"Khadija Hashim Rungwe ( Mtoto wa mzee wa Ubwabwa) ni kiongozi makini nitumeni mimi nikawe kilanja wenu kwakuwa tukiwa na uwakilishi makini kutoka kwangu na diwani Hamo basi tutafika mbali na maendeleo yatapatikana,"amesema Khadija.
Amesema changamoto zipo nyingi ikiwepo ajira,vijana wanahangaika kupata ajira kwahiyo ataenda kuwatetea vijana ili waweze kuajirika kwakuwa viwanda vipo vingi na hakuna sababu ya maisha kudidimia.
Mwenyekiti wa Chama Cha Ukombozi wa Umma( CHAUMMA) Mkoa wa Pwani Weston Sinkonde kushoto akimnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Kibaha Mjini kupitia chama hicho Khadija Hashim Rungwe ( katikati) na wa kwanza Kulia ni mgombea udiwani Kata ya Kibaha Hamo Machapula.Amesema wamchague ili waache kuwa watu wa kulalamika kwani nguvu ipo mikononi mwao na wachague mtu wanayemtaka sio kuchagua mtu kwa kulazimishwa au nguvu ya pesa.
Amesema kama Wananchi wanataka mabadiliko ya kweli siku ya Oktoba 29 wananchi watoke kwenda kupiga kura na wala wasisuse kwakuwa kususia uchaguzi ni sawa na kukataa mabadiliko ya kimaendeleo.
Mgombea wa udiwani wa Kata ya Kibaha kupitia tiketi ya Chaumma Hamo Machapula amewaomba Wananchi wamchague yeye kuwa diwani ili awe mwakilishi wao kwakuwa anajua Kata ya Kibaha inachangamoto nyingi ikiwemo elimu,afya,maji ,umeme na barabara.
Mwenyekiti wa Chama Cha Ukombozi wa Umma ( CHAUMMA) Mkoa wa Pwani Weston Sinkonde akimnadi mgombea wa udiwani wa Kata ya Kibaha Hamo Machapula katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika Oktoba 11 ,2025 kwa Mfipa katika Manispaa ya Kibaha.Machapula ameseema wamchague ili kuboresha elimu hususani ujenzi wa madarasa katika Shule zilizopo pamoja na kuhakikisha anajenga Shule mpya katika maeneo ambayo hayana shule ili kuepusha wanafunzi kutembea umbali mrefu.
Amesema kuwa atazisimamia barabara za Mitaa hususani Mtaa wa Simbani na Mwendapole ili zijengwe na kupitika muda wote lakini pia atakwenda kusukuma ajenda ya mikopo ya asilimia 10 .
Amesema mikopo hiyo kwasasa haiwafikii walengwa kwakuwa hakuna mtu wa kusukuma ajenda hiyo katika Halmashauri na badala yake fedha zinazotengwa zinarudishwa lakini mtu pekee wa kufanyakazi hiyo ni yeye endapo watamchagua.
Hata hivyo Machapula amesema pia atakwenda kusukuma ajenda ya ushuru mdogomdogo kuhakikisha Wananchi wake hawateseki na ushuru kwani Tanzania ni tajiri na ina migodi mikubwa ambayo inatoa pesa nyingi na hakuna sababu ya kuwasumbua wafanyabiashara wadogo.




Post a Comment