HEADER AD

HEADER AD

MALEZI KIINGEREZA!

MALEZI Kiingereza, ndiyo ya kwetu malezi,

Na pesa twaziongeza, huku twapiga mluzi,

Nyumbani ni malegeza, tumejitoa uzazi,

Haya malezi mengine, ndiyo chaisha kizazi.

Shule tunajiongeza, kusaka hadi Zambezi,

Aseme Kiingereza, hata kile hatuwezi,

Hapo tunajipongeza, kwamba tumefanya kazi,

Haya malezi mengine, ndiyo chaisha kizazi.

Jinsi tunawadekeza, kwa yetu haya malezi,

Wajiburuzaburuza, hata hawafanyi kazi,

Hilo si la kutukwaza, ni ya kisasa malezi,

Haya malezi mengine, ndiyo chaisha kizazi.

Nyumbani twabembeleza, hawafanyi yote kazi,

Kazi ni kuwachokoza, wajibu wa kijakazi,

Wenyewe kuchezacheza, vile bado wanafunzi,

Haya malezi mengine, ndiyo chaisha kizazi.

Lugha imetupumbaza, eti hayo ni malezi,

Watoto watutatiza, kwa kuyakosa malezi,

Macho bado yachomoza, shule nzuri utatuzi,

Haya malezi mengine, ndiyo kizazi chaisha.

Mila twaziangamiza, wazione upuuzi,

Ndizo zilizotukuza, twaeleweka wazazi,

Wenyewe wajiongeza, hata za kigeni kozi,

Haya malezi mengine, ndiyo kizazi chaisha.

Lugha yetu yapendeza, tujue tuwe wajuzi,

Sawa na Kiingereza, zote zinafanya kazi,

Elimu wakiongeza, tusiyaache malezi,

Haya malezi mengine, ndiyo kizazi chaisha.

Familia kuiweza, vema kuwapa malezi,

Tuache wabembeleza, kwa yetu haya malezi,

Waweze kujitokeza, wawe wazuri wazazi,

Haya malezi mengine, ndiyo kizazi chaisha.

Elimu kuwabatiza, ile njema ni malezi,

Lakini kuwadekeza, hayo wala si malezi,

Ndivyo tunawapoteza, na kumaliza kizazi,

Haya malezi mengine, ndiyo kizazi chaisha.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments