MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA KIBAHA VIJIJINI AWAHIMIZA VIJANA KUDUMISHA AMANI

Na Gustaphu Haule, Pwani
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Hamoud Jumaa ( Mzee wa Sambusa)amewasisitiza vijana waliopo katika Jimbo hilo kuhakikisha wanailinda amani kwani ndio silaha inayoinua uchumi nchini.
Amesema bila uwepo wa amani watu hawawezi kufanya shughuli za kiuchumi hivyo ni vyema amani iliyopo ikazidi kudumishwa kizazi hadi kizazi.
Jumaa ametoa wito huo wakati akizungumza na Wananchi pamoja na wanachama wa CCM katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika Oktoba 18,2025 katika Kata ya Kilangalanga iliyopo Kibaha Vijijini.
Hamoud Jumaa apokea zawadi kutoka kwa wanachama wa CCM wa Kata ya Kilangalanga alipokwenda kufanya mkutano wa kampeni kwa ajili ya kuomba kura ili wamchague Oktoba 29 mwaka huu.
Amesema baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alifanya kazi kubwa ya kuiunganisha Tanzania kuwa kitu kimoja licha ya kuwa ndani ya nchi hiyo kuna makabila mengi.
Jumaa amesema jambo kubwa ambalo Mwalimu Nyerere alifanikiwa ni kutengeneza amani ya nchi ambapo kila Mtanzania anao Uhuru wa kufanyakazi na kuishi sehemu yoyote hapa nchini bila kusumbuliwa.
Amesema kutokana na umuhimu wa amani hapa nchini vijana wanatakiwa kuendelea kushikamana kuhakikisha amani iliyopo inalindwa kwa gharama yoyote na wasijiingize katika makundi ya watu ambao hawaitakii mema nchi.
WanaCCM wakimsikiliza mgombea ubunge Hamoud Jumaa hayupo pichani katika mkutano wa kampeni uliofanyika Oktoba 18 Kata ya Kilangalanga.
"Vijana nawaomba itunzeni amani iliyopo na kuitunza amani ni pamoja na kwenda kupiga kura siku ya Oktoba 29 bila kuingia katika mkumbo wa watu wachache ambao hawaitakii mema nchi yetu na ikifika siku ya kupiga kura nendenj mkapige kura na mrudi nyumbani kuendelea na shughuli zenu za kiuchumi,"amesema Jumaa.
Jumaa amewaomba wananchi wa Kata ya Kilangalanga Oktoba , 29 wakafanye maamuzi ya msingi ya kwenda kumchagua mgombea wa urais wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) Dkt.Samia Suluhu Hassan, mbunge Hamoud Jumaa pamoja na diwani Mwajuma Denge.
Amesema CCM itashinda kwakuwa inawachama wengi zaidi ya milioni 13 lakini hakiwezi kushinda kwa kujiamini kwa Kulala kitandani na hapo watakuwa wamefanya makosa kwani kinachotakiwa ni kutoka kwa ajili ya kuwashawishi wananchi wakichague Chama Cha Mapinduzi.
Amesema kuwa CCM ni chama sahihi ambacho kinaleta maendeleo ya nchi na ni chama ambacho kimetufikisha hapa tulipo na kitaendelea kuleta maendeleo zaidi kwakuwa ilani yake inaeleweka.
Amesema yapo mambo anataka kuyafanya akichaguliwa kubwa mbunge wa Jimbo hilo kwani anafahamu changamoto za akina mama, wafugaji ,barabara ,elimu ,afya ,umeme ,maji na vijana.
Hamoud Jumaa akabidhiwa upinde na vijana wa Kata ya Kilangalanga ikiwa ni ishara ya ulinzi kipindi akiwa katika utekelezaji wa majukumu yake.
Amesema na jambo la kwanza ni kuhakikisha vijana wanapata ajira na kuwaelimisha vijana kutambua fursa zilizopo katika maeneo yao na hata kuwasaidia katika kupata elimu.
"Nimejipanga kuhakikisha vijana wanasaidiwa kwa vitendo lakini nahitaji kusaidia akina mama hususani kupata mikopo na kupata elimu ya ujasiriamali kwani wakati nikiwa mbunge nilikuwa nafanya mambo hayo na sasa mkinichagua nitafanya tena kama awali",amesema Jumaa
"Ndugu zangu naomba mtuamini maana tumekuja kufanya mambo mazuri na sasa tunakwenda kujenga kituo cha biashara pamoja na kusimamia shughuli za maendeleo ili Wananchi wetu wapate maendeleo,"amesema Jumaa wakati akiomba kura Kilangalanga.
Hata hivyo, pamoja na mambo mengine Jumaa ameahidi kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa uzio katika Shule ya Sekondari Kilangalanga ambapo aliuanzisha akiwa mbunge na sasa akiingia atakwenda kupambana kuhakikisha anakamilisha ujenzi huo.
Naye mgombea wa udiwani wa Kata ya Kilangalanga Mwajuma Denge amesema kuwa CCM imefanya mambo makubwa miaka mitano iliyopita kwani wamepokea kiasi cha Sh. Bilioni 1.5 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ndani ya Kata hiyo.
Denge amesema kuwa fedha hizo zimetumika kujenga madarasa katika shule zote pamoja na kujenga matundu ya vyoo, ujenzi wa Zahanati ya Disunyara na jengo la mama na mtoto pamoja na nyumba ya afisa Kilimo wa Kata hiyo.
Hamoud Jumaa apewa zawadi na wanachama wa CCM Kilangalanga.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini kupitia tiketi ya CCM Hamoud Jumaa akiwa katika Kata ya Kilangalanga.






Post a Comment