MWILI WA RHODA ALIYEUAWA KWA MAPANGA WAENDELEA KUSOTA MOCHWARI , NDUGU WAGOMA KUZIKA
>>Familia ya marehemu yadai mme ambaye ni Meneja TARURA amehusika mauaji ya ndugu yao , hivyo hawawezi kumzika kirahisi
>> Ndugu upande wa marehemu wajitenga ,msiba waketi mara mbili nyumbani kwao marehemu Nyamongo na nyumbani kwa mume wa marehemu Serengeti
DIMA Online, Serengeti
MWILI wa marehemu Rhoda Jonathani, mkazi wa Kitongoji cha Burunga , Kata ya Uwanja wa Ndege wilayani Serengeti, mkoa wa Mara , aliyeuawa kwa kukatwakatwa kwa mapanga umeendelea kusota katika chumba cha kuhifadhia maiti , katika hospitali ya wilaya ya Serengeti.
Familia ya marehemu imesema haiwezi kuzika hadi pale serikali itakapotoa taarifa ya awali ya uchunguzi juu ya mauaji ya ndugu yao huku wakimuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingilia kati haki ipatikane na wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria .
Ni siku ya tano tangu mwili huo ulipohifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti . Tukio la mauaji lilitokea, Oktoba, 23, 2025, baada ya watu ambao hawakutambuliwa majina yao , waliruka ukuta na kuingia chumbani kwake kisha kumkatakata mapanga katika sehemu mbalimbali za mwili wake huku kiganja cha mkono wake kikikutwa chini ya sakafu.
Marehemu alikuwa mke wa Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) mkoa wa Kagera , Mhandisi Wilson Charles ambaye wamefanikiwa kupata watoto watatu ,kati yao wa kike wawili na mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka saba ambaye ni mlemavu wa viungo.
Rhoda Jonathan enzi ya uhai wake akiwa nyumbani kwake Kitongoji cha Burunga, kata ya Uwanja wa Ndege wilayani Serengeti.
Imeelezwa kwamba sababu ya mwili huo kuendelea kusota chumba cha kuhifadhia maiti bila kuzikwa ni baada ya ndugu wa marehemu kugoma mwili kuzikwa wakiitaka serikali iingilie kati ili haki ya ndugu yao ipatikane baada ya kufanyiwa kitendo cha kikatili.
Ndugu wa marehemu wanamtuhumu mme wa marehemu Eng. Wilson kwa madai kuwa anahusika kwa mauaji ya ndugu yao huku wakiiomba serikali kuwasaka wahusika wote na kuwachukukia hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Kufuatia tukio hilo la mauaji familia ya marehemu imejitenga na familia ya Eng. Wilson ambapo kila familia imeweka msiba nyumbani kwao . Familia ya marehemu msiba upo nyumabani kwao Kijiji cha Nyangoto -Nyamongo na familia ya Wilson msiba upo nyumbani kwake Kitongoji cha Burunga, Kata ya Uwanja wa Ndege ,wilayani Serengeti.
Mpaka sasa haijaeleweka mwili wa marehemu utazikwa lini ambapo hadi sasa ni siku ya tano mwili wa marehemu ukiendelea kusota chumba cha kuhifadhia maiti .
Ndugu wa marehemu
John Jonathan kaka wa marehemu amesema wanataka serikali iwapatie taarifa ya uchunguzi , lakini pia ndugu wa marehemu wanataka kuona hatua zinachukuliwa kwa watuhumiwa waliohusika na mauaji.
" Kinachotushangaza, siku marehemu ameuawa shemeji hakutupatia taarifa ya kifo cha mke wake. Mida ya saa moja usiku mke wa mdogo wangu alimpigia simu wifi yake kumuuliza kama amefika salama maana siku hiyo alikuwa hapa Nyamongo kwenye harusi.
"Wakati akiongea nae kwa simu ghafla akasikia mdogo wangu anapiga kelele akisema wifi nimekufa. Wifi yake akampigia simu mme wake akamwambia kwamba alikuwa anaongea na simu na wifi yake lakini ghafla alisikia akipiga yowe na kisha akasikia anakoroma, baada ya hapo simu yake ilikuwa kimya bila mtu kusema chochote.
" Wanafamilia tulilazimika kufunga safari
muda huo huo kutoka Nyamongo hadi wilayani Serengeti ,tulifika mida ya saa sita usiku. Tulikuta mdogo wetu ameshakufa na yuko chumba cha kuhifadhia maiti .
" Mtu wa mochari alisema muda umeenda sana hatuwezi kumuona, ilibidi tuende nyumbani kwa marehemu tukalala pale, mpaka kunakucha hatukumuona mme wa marehemu.
" Tulienda mochari tukakaa pale masaa saba lakini mmewe hakujitokeza hospitali . Tulijiuliza sana kwanini ndugu yetu kafa na hajatupatia taarifa?na kwanini haonekani hospitali wala msibani wakati mkewe ameuawa " amesema John.
John ameongeza kusema" Muda wote tumekaa pale hospitali tukisubiri uchunguzi wa mwili , hakuna ndugu wa upande wa mwanaume wala mme wake aliyeonekana hospitali . Wakati sisi tulitegemea wao ndio watupokee .
" Cha kushangaza licha ya mwanaume kutoonekana hospitali mwanaume akapanga mazishi yafanyike jumapili . Sisi tulisema hawezi kuzikwa bila kupata taarifa ya awali ya serikali juu ya kifo chake .
Ndugu wa marehemu wamesema wanasubiri majibu ya serikali , lakini wanataka kuona serikali itachukua hatua gani huku wakiiomba serikali ya Mara na Rais Samia, kufanya uchunguzi ikiwemo kuichunguza simu ya marehemu ambayo ilitumika katika mawasiliano .
" Wakati mdogo wangu hajaondoka kwenda kwake Serengeti,alipigiwa simu na mtu akimwambia anahitajika Serengeti kwenda kusaini fomu za uthamini na siku hiyo hiyo saa moja usiku baada ya kufika kwake aliuawa.
" Tunaomba serikali ichunguze simu ya marehemu ili kutambua ni nani aliyempigia simu. Lakini pia wale wahalifu walimuua kwa kutumia panga na kisha kulitelekeza pembeni mwa barabarani likiwa na damu. Polisi walilichukua kwa uchunguzi zaidii. Tunaomba vifaa hivyo vichunguzwe" amesema John.
Sara Harun Sultan dada wa marehemu amesema " mdogo wangu alikuwa kwenye harusi huku Nyamongo , aliondoka siku ya alhamis kwenda kwake Serengeti na usiku wa siku hiyo aliuawa.
"Nilijiuliza kwanini shemeji hakutupatia taarifa ya msiba wa mdogo wangu mpaka tunapewa taarifa na watu wengine ! Hata kama wanandoa hamna maelewano likitokea tatizo mnajulisha ndugu.
" Nilijiuliza kwanini hakukuwa na ndugu yeyote wa mwanaume pale hospitali zaidi ya kuwepo tu ndugu wa upande wa marehemu ? " .Tunaiomba serikali , Rais Samia waliitazame suala hili kwa jicho pana " amesema Sarah.
Victoria Paul amesema " Marehemu ni wifi yangu , ni dada yake na mme wangu. Wifi ni mtu aliyependa sana kuzungumza kwa simu . Nilimpigia simu kujua kama amefika salama , wakati tunaongea na simu nilisikia kama anaongea na mtu baadae kidogo nikasikia anapiga yowe mara mbili kama vile ananigwa .
" Alisema wifi yangu nimekufa , nikaendelea kuomba kwenye simu nikadhani au ameshikwa na mapepo ?niliendelea kumuita wifi lakini sikusikia sauti yake tena .
Nilipiga simu tena na tena iliita bila kupokelewa ndipo nikampigia simu mme wangu na kumueleza , naye akawapigia simu ndugu zake kisha wakaenda Serengeti wakakuta wifi ameuawa" amesema Victoria.
Dada wa mme wa marehemu
Telesia Chacha Maginga ni dada wa mme wa Rhoda ameziomba familia zote upande wa mme na upande wa mke kuondoa tofauti zao na kuacha hasira waweze kuzika mwili wa marehemu huku taratibu zingine za kiuchunguzi zikiendelea .
DIMA Online, imemtafuta kwa jina ya simu Mganga mkuu hospitali ya wilaya ya Serengeti, Lusubilo Adam kufahamu kama mwili umefanyiwa uchunguzi na taratibu zingine lakini simu yake iliita bila kupokelewa, alipotafutwa mara kadhaa simu yake haikuwa hewani.
Hatua zilizochukuliwa na serikali
Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Anjelina Lubella amesema serikali inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo .
Jeshi la Polisi linamshikilia kwa mahojiano , Wilson Mwita Charles mwenye umri wa miaka (53) mkazi wa Kitongoji cha Burunga, kata ya Uwanja wa Ndege wilayani Serengeti kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Rhoda Jomathani.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mara, Pius Lutumo , amesema Tarehe , 23, Oktoba, 2025 ,majira ya saa 1: 00 usiku huko Kitongoji cha Burunga, Rhoda Jonathan (42) aliuawa kwa kukatwakatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake .
" Aliuawa baada ya mtu/watu kuruka ukuta wa nyumba yake na kutekeleza mauaji hayo. Jeshi la Polisi bado linaendelea na uchunguzi " amesema Kamanda Pius .
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Polisi kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia uchunguzi .
Kwa undani wa habari hii rejea habari zilizoropotiwa kupitia chombo hiki cha habari , Agosti, 26, 2025, Agosti ,27, 2025 na Agosti 28, 2025 .







Post a Comment