HEADER AD

HEADER AD

DED KIBAHA AAGIZA MRADI URUDIWE BAADA YA KUBAINI KUJENGWA CHINI YA KIWANGO


>>Halmashauri ya Kibaha imetoa Tsh. Milioni 420 za mapato ya ndani kwa ajili ya ukarabati wa barabara

>> Kila kata imepewa Tsh. Milioni 30 ukarabati wa barabara

Na Gustaphu Haule, Pwani 

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa ameonesha kutoridhishwa na utekelezaji wa mradi wa uchongaji wa barabara .

Miradi hiyo ni katika Mitaa ya Machinjioni na Kilimahewa, Kata ya Tangini ambapo ameagiza  kazi hiyo irudiwe mara moja ili barabara hizo ziwe katika kiwango kinachokidhi malengo ya serikali.

       Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa akikagua baadhi ya barabara katika Kata ya Tangini Novemba 13/2025.

Dkt. Shemwelekwa ametoa agizo hilo Novemba 13/2025 katika ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Kata ya Tangini ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi inayoendelea katika maeneo ya Kata mbalimbali ya Manispaa ya Kibaha.

Amesema  barabara hizo ambazo zinagharimu Tsh. Milioni 30 kupitia mapato ya ndani ya Manispaa hiyo hazijachongwa kwa ubora unaotakiwa na hivyo hazijakidhi lengo la serikali la kutatua kero za wananchi.

“Ndugu viongozi, nimekagua mradi huu wa barabara na niseme wazi sijaridhishwa na kazi iliyofanyika, lengo la serikali ni kutatua kero za wananchi .

" lakini kwa hali hii sioni kama tatizo limepatiwa suluhisho kwahiyo naagiza mtendaji wa kata kuhakikisha barabara hizi zinachongwa upya  na nitarejea tena kukagua utekelezaji wake,” amesema Dkt. Shemwelekwa.

Mkurugenzi huyo amewataka wananchi pamoja na viongozi wa ngazi ya kata na mitaa kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika ipasavyo kwa malengo yaliyokusudiwa.

        Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mailimoja" B" Shauri Yombayomba ( mwenye Tshirt rangi nyekundu) akimuelekeza jambo mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa alipokuwa akikagua baadhi ya barabara za Mitaa huo juzi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Shemwelekwa ameidhinisha ujenzi wa makaravati mawili eneo la shule ya msingi Mamlaka na kivuko cha Kwa kwembe katika maeneo yenye changamoto za mifereji ya maji ili kupunguza kero zinazowakabili wananchi.

Manispaa ya Kibaha imetoa jumla ya Tsh. Milioni 420 kutoka chanzo cha  mapato ya ndani kwa ajili ya kutengeneza barabara za mitaa ambapo kila kata imepatiwa Tsh. Milioni 30 ili kutatua changamoto za miundombinu kwa wananchi wake.

     Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa ( kushoto) akikagua barabara za Kata ya Tangini  katika ziara aliyoifanya Novemba 13/2025.


No comments