HEADER AD

HEADER AD

DED KIBAHA AWATAKA WANANCHI KUTUNZA MIUNDOMBINU YA MIRADI YA MAENDELEO



Na Gustaphu Haule, Pwani 

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa,amewataka wananchi wa Manispaa hiyo kuhakikisha wanatunza miundombinu ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

Dkt.Shemwelekwa ametoa wito huo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo katika Kata ya Mbwawa iliyofanyika Novemba 12/2025 ambapo amesisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika kuilinda na kuitunza miradi inayotekelezwa kwa manufaa yao.



Amesema halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imetoa Tsh. Milioni 420 kwa ajili ya kutengeneza barabara zenye lengo la kuboresha huduma kwa wananchi lakini changamoto kubwa imekuwa wananchi kutokutunza barabara hizo mara baada ya kufunguliwa.

Shemwelekwa ameongeza kuwa ni muhimu kwa wananchi kutambua kwamba miradi ya serikali ni matokeo ya kodi zao hivyo ni wajibu wao kuilinda na kuitunza kuhakikisha inadumu kwa muda mrefu.

“Kama leo tumefungua barabara basi mwaka ujao tuweke kifusi na kuendelea kuboresha zaidi ili tuendelee kupiga hatua za kimaendeleo ,"amesisitiza Shemwelekwa.

Wananchi wa Kata ya Mbwawa wamempongeza Dkt. Shemwelekwa kwa utendaji wake na kasi ya kusimamia maendeleo, wakisema kuwa anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kutatua changamoto zinazowakabili.

Mkurugenzi huyo ameahidi kuendelea kumpa ushirikiano ili kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inafanikiwa na kuleta manufaa kwa jamii.
      Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa (Kulia) akiwa katika ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo katika Kata ya Mbwawa.

      Ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha katika Kata ya Mbwawa iliyofanyika Novemba 12/2025.

     Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa akiongoza timu ya wataalamu kukagua miradi ya maendeleo Kata ya Mbwawa.


No comments