HEADER AD

HEADER AD

SERIKALI KUWAFIKISHA MAHAKAMANI WALIOHUSIKA MAUAJI YA MKE WA MENEJA TARURA


>> Hatimaye mwili wazikwa baada ya kugomewa na ndugu wa marehemu kwa siku 14

>>DC Serengeti asema Serikali haitawavumilia wote waliohusika na mauaji

DC Tarime ahimiza amani

DIMA Online, Serengeti 

SERIKALI imewahakikishia waombolezaji na familia ya marehemu Rhoda Jonathani , mwenye umri wa miaka (42), aliyeuawa kwa kukatwakatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake, kuwa itahakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wote waliohusika na mauaji na kuwafikisha mahakamani.

Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Anjelina Lubella ameyasema hayo wakati akizungumza na waombolezaji kwenye mazishi ya Marehemu Rhoda Jonathan, yaliyofanyika Novemba, 06, 2025 katika Kanisa la Waadventista Wasabato Matare mjini Mugumu.

   Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Anjelina Lubella akizungumza wakati wa ibada ya mazishi ya Marehemu Rhoda Jonathani yaliyofanyika Katia Kanisa la Matare SDA wilayani Serengeti.

DC Anjelina amekemea vitendo hivyo vya kikatili na kusema kuwa serikali haitawavumilia wote waliohusika na mauaji ya marehemu Rhoda na kwamba watu kadhaa wanashikiliwa kwa tuhuma za mauaji.

" Poleni sana , sisi kama serikali tunawahakikishia hatua za kisheria zitachukuliwa didhi ya wote waliohusika. Mmeshaona hatua za awali zimeanza kufanyika.

      Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Anjelina Lubella , akiaga mwili wa marehemu Rhoda Jonathani aliyeuawa kwa kukatwakatwa mapanga nyumbani kwake, katikati ni mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele

" RPC alituambia uchunguzi umeanza na kuna baadhi ya watu wameshakamatwa. Tunaombeni mtuamini kama serikali tufanye kazi yetu. Uchunguzi utakapokamilishwa na vyombo vya kisheria waliohusika wote watafikishwa mahakamani na mtaendelea kuhabarishwa" amesema DC Serengeti .

Ameitaka jamii kuachana na vitendo vya kikatili yakiwemo mauaji . " Kumekuwepo na stori nyingi sana , hawa wanasema imetokea hivi imetokea hivi. Mimi kama kiongozi wa serikali ninawaomba sana sana sana tumuachie Mungu.

  Mwili wa marehemu Rhoda Jonathani ukitolewa Mochwari, wilayani Serengeti kwa na kuingizwa kwenye gari kwa ajili ya maziko.

" Sisi kama serikali tunalaani kitendo hicho kilichofanyika kwa mwanamama mwenzetu ni cha kikatili sana hakuna mtu anayekipenda ni kibaya sana na tunalaani sana.

" Tunaomba jamii tuache vitendo kama hivi sio vizuri vinauzunisha . Tunaona Bi. Rhoda ameacha mtoto mdogo aliyehitaji msaada wake wa karibu . Leo hii tumekatisha uhai wake nani atakayemwangalia mtoto! Tunawapa pole sana na tunazidi kuwaombea maana faraja inatoka kwa Mungu " amesema DC Anjelina.

Naye mkuu wa wilaya ya Tarime , Meja Edward Gowele amewaomba waumini, waombolezaji na wananchi kwa ujumla kuendelea kuhimiza amani ya wilaya hizo.

     Mkuu wa wilaya ya Tarime , Meja Edward Gowele akiaga mwili wa marehemu Rhoda Jonathan, aliyeuawa kwa kukatwakatwa mapanga nyumbani kwake wilayani Serengeti.

" Nimeona nishiriki nanyi , kazi zetu zinategemea maombi yenu. Niwaombe waombolezaji , waumini na wananchi kwa ujumla tuendelee kuhimiza amani, haina haja ya kuelezea wote tunajua msiba ulivyotokea " amesema DC Gowele.

Katibu mkuu Jimbo la Kaskazini kanisa la Waadventista Wasabato, Mchungaji Baraka Nchama, amewaomba waumini na waombolezaji kutubu dhambi kwani bila hivyo ukimtendea mwenzio vibaya na wewe utatendewa hivyo hivyo.


     Katibu mkuu Jimbo la Kaskazini kanisa la Waadventista Wasabato, Mchungaji Baraka Nchama( mwenye suti nyeusi) , mkuu wa wilaya ya Tarime , Meja Edward Gowele kushoto na mkuu wa wilaya ya Serengeti, Anjelina Lubella wakitoa pole kwa wafiwa.

" Waliomwaga damu za watu hawatatoboa  kwa Mungu kwani Mungu kupitia wanasheria wake wameshatoa hukumu " amesema mchungaji.

Pia, amekemea uongo kwamba ni mbaya unachongamisha na unatenganisha watu.

Awali Jeshi la Polisi mkoa wa Mara, lilithibitisha kuwashikilia kwa mahojiano watu kadhaa akiwemo mume wa marehemu, Mhandisi Wilson Mwita Charles mwenye umri wa miaka (53) mkazi wa Kitongoji cha Burunga, kata ya Uwanja wa Ndege wilayani Serengeti kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mkewe Rhoda Jonathani.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mara, Pius Lutumo, alisema Tarehe , 23, Oktoba, 2025 ,majira ya saa 1: 00 usiku huko Kitongoji cha Burunga, Rhoda Jonathan (42) aliuawa kwa kukatwakatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake .

      Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mara, Pius Lutumo.

" Aliuawa baada ya mtu/watu kuruka ukuta wa nyumba yake na kutekeleza mauaji hayo. Jeshi la Polisi bado linaendelea na uchunguzi " amesema Kamanda Pius.

Pia jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Polisi kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia uchunguzi.

      Washiriki wa kanisa la Waadventista Wasabato kanisa la Misituni na waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa marehemu Rhoda Jonathan wakiupeleka kuhifadhi kwenye makabuli yaliyopo kanisa la Matare SDA wilayani Serengeti.

Mwili wazikwa baada ya kusota siku 14

Hatimaye mwili wa marehemu Rhoda Jonathani , uliosota Mochwari siku 14 umezikwa katika makaburi ya kanisa la Waadventista Wasabato Matare, wilayani Serengeti .
 
Mwili wa marehemu Rhoda Jonathani ukishushwa kwenye nyumba yake ya milele ,kwenye makabuli ya kanisa la Matare SDA wilayani Serengeti.

Rhoda aliuawa kwa kukatwakatwa kwa mapanga na kiganja cha mkono wake wa kulia kukutwa kimedondoka sakafuni, akiwa na majeraha makubwa kifuani , mkononi na sehemu mbalimbali za mwili wake.

Awali familia ya marehemu ilisema haiwezi kuzika hadi pale serikali itakapotoa taarifa ya awali ya uchunguzi juu ya mauaji ya ndugu yao huku wakimuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingilia kati haki ipatikane na wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria .

         Mwili wa marehemu Rhoda Jonathani ukutolewa Mochwari wilayani Serengeti kwa ajili ya maziko.

Ndugu wa marehemu walimtuhumu mme wa marehemu Eng. Wilson kwa madai kuwa anahusika na mauaji ya ndugu yao ambapo chanzo kilitajwa kuwa ni fidia ya ardhi kupisha ujenzi wa uwanja wa ndege.

Familia ya marehemu ilieleza kuwa,  mme alimkatalia marehemu kuhusika chochote katika tathmini isipokuwa yeye tu licha ya kumtelekeza kwa zaidi ya miaka mitano ambapo mke alikuwa amefanya uendelezaji wa nyumba ambayo alijengewa na mmewe jambo lililoibua migogoro baina yao na kupelekea mauaji ya Rhoda.

Kufuatia tukio hilo la mauaji familia ya marehemu ilijiitenga na familia ya Eng. Wilson mme wa marehemu ambapo kila familia iliweka msiba nyumbani kwao .

       Waombolezaji wakiwa msibani nyumbani kwa marehemu Rhoda Jonathani Kitongoji cha Burunga wilayani Serengeti.

Familia ya marehemu msiba upo nyumabani kwao Kijiji cha Nyangoto -Nyamongo na familia ya mme wa marehemu msiba upo nyumbani  kwa marehemu Kitongoji cha Burunga, Kata ya Uwanja wa Ndege ,wilayani Serengeti ambako ni nyumbani kwa Wilson na mkewe.

Waombolezaji wamkumbuka Rhoda 

Waombolezaji wakiwa katika mazishi wameeleza wasifu wa marehemu na kusema kuwa alikuwa mtu mwema na aliyejituma katika kazi za kumtumikia Mungu .

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Burunga , James Makuru Marwa amesema wana Burunga wamepata msiba mkubwa anamuomba Mungu awatie nguvu katika kipindi hiki kigumu.

      Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kanisani, kata ya Matare , Abeid Nyangi.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kanisani, kata ya Matare , Abeid Nyangi amesema amemfahamu Rhoda tangu mwaka 2008 na kwamba amesikitika Marehemu Rhoda alivyouawa kinyama.

" Tuna masikitiko sana naomba Mungu awe mfariji wetu , mwenyezi Mungu ameamua apunzike hatuna namna " amesema" Mwenyekiti.

Akieleza historia ya Marehemu , Steven Kigwasho Paul ambaye ni mshiriki wa kanisa la waadventista Wasabato la Misitu alikokuwa akiabudu Rhoda, amesema Rhoda ni miongoni mwa waanzilishi wa kanisa la Misitu akiwa mshiriki namba 14.

        Ndugu wa marehemu Rhoda Jonathani waliotoka Nyamongo alikozaliwa Rhoda wakiwa kwenye majonzi baada ya kuwasili nyumbani kwa marehemu Kitongoji cha Burunga,wilayani Serengeti.

Amesema katika utumishi wake kanisani amewahi kuwa mhazini wa kanisa, Katibu wa huduma , mkuu wa Huduma, Mjumbe wa Baraza la kanisa na kwamba amekuwa na mchango mkubwa kanisani.

" Alisaidia kupatikana kwa samani na vyombo vya kuendesha kanisa , amekuwa msaada kwa wajane , watoto wenye ulemavu . Kanisa limepoteza nguzo muhimu" amesema Steven.

 Kaka wa marehemu , John Jonathani amesema familia ya marehemu inawashukuru wananchi, waumini majirani, na viongozi wa serikali kushiriki bega kwa bega katika msiba wa mdogo wake .

      Ester Jonathani  Mobe mama wa Marehemu Rhoda Jonathani akiaga mwili wa mwanae aliyeuawa kwa kukatwa mapanga nyumbani kwake .

"Nina washukuru sana wote kujumuika katika msiba huu, tunashukuru kanisa kwa kutoa eneo ili kumzika Rhoda. Upande wa mme hawakuhudhulia msiba huu. Msiba uligawanyika, kwa upande wa mme wamefanyia msiba Serengeti na kwa upande wa Marehemu wamefanyia msiba Nyamongo -Tarime.

"Leo siku ya madhishi tuliona Rhoda azikwe hapa kanisani kwasababu kule kwake eneo lile litafanyiwa uthamini kwa ajili ya kupisha ujenzi wa uwanja wa ndege. Rhoda ni mdogo wangu ni mtoto wa tatu kutoka mwisho.

        Nyumba ya marehemu Rhoda Jonathan na mmewe Mhandisi Wilson Charles katika Kitongoji cha Burunga, kata ya Uwanja wa Ndege,wilayani Serengeti.

" Rhoda alikuwa ni kiunganishi kwenye familia . Siku mbili kabla ya kifo chake alinipigia simu kwamba wanataka kufanyiwa tathmini lakini hajui kama atapata haki yake kwasababu mme wake alimzuia asifanye chochote na baada ya hapo aliuawa" amesema John.

Musa Jonathan amesema Marehemu Rhoda alikuwa anampenda Mungu " Aliniambia kaka yangu naomba ufanye kazi ya Mungu na upende familia yako . Muda tunaoishi ni mfupi sana , kupitia msiba huu naomba kila mtu atafakari maisha yake " amesema Musa.

Mazishi hayo alihudhuliwa na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali ambapo wakuu hao wa wilaya ya Serengeti na Tarime walishuhudia wakati mwili wa marehemu ukishushwa kwenye nyumba yake ya milele hadi mwisho wa mazishi licha ya mvua kubwa kunyesha.

Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (kushoto) pamoja na mkuu wa wilaya ya Serengeti Anjelina Lubella wakitoa salamu za pole wakati wa ibada ya mazishi ya Marehemu Rhoda Jonathani iliyofanyika kanisa la Matare SDA wilayani Serengeti, Novemba, 06, 2025.

       Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (kushoto) pamoja na mkuu wa wilaya ya Serengeti Anjelina Lubella wakiwa kwenye ibada ya mazishi ya Marehemu Rhoda Jonathani iliyofanyika kanisa la Matare SDA wilayani Serengeti, Novemba, 06, 2025.

           Sehemu ya waombolezaji wakiwa kwenye ibada ya mazishi ya Rhoda Jonathan katika kanisa la Matare, wilayani Serengeti.

              Watoto wa marehemu wakitolewa ndani ya nyumba yao wakisindikizwa kwenda kwenye eneo la waombolezaji.


No comments