CCM PWANI WATOA TAMKO LA KUUNGA MKONO HOTUBA YA RAIS SAMIA
Na Gustaphu Haule, Pwani
CHAMA Cha Mapinduzi ( CCM) Mkoa wa Pwani kimetoa tamko la kuunga mkono hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Disemba 02/2025 wakati akizungumza na wazee wa Jijini Dar es Salaam.
Chama hicho kimesema kuwa hotuba ya Rais Dkt .Samia imegusa masuala muhimu yanayohusu Taifa na imetoa dira ,matumaini na mwelekeo mpya kwa maendeleo ya Taifa.
Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Pwani David Mramba ametoa tamko hilo Disemba 5/2025 katika mkutano wake na Waandishi wa habari uliofanyika kwenye ofisi ya CCM Mkoa wa Pwani.
Katika mkutano huo,Mramba amesema kuwa CCM Mkoa wa Pwani inaunga mkono hotuba hiyo katika mambo mbalimbali ambayo yana muelekeo na maslahi ya Taifa.
Mramba amesema hotuba hiyo imeonyesha kuimarisha amani na Muungano kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo na hotuba hiyo imekuwa na dhamira ya dhati ya kuendeleza maridhiano,umoja na kudumisha Muungano wa Taifa .
Mramba amesema kuwa jambo la pili ni kuwa hotuba ya Rais Samia imechochea uchumi na fursa za maendeleo ambapo CCM Mkoa wa Pwani wanapongeza Kwakuwa Rais amekuwa ni dhamira ya kuendeleza mageuzi ya kiuchumi,kukuza uwekezaji, kuimarisha miundombinu na kutengeneza ajira kwa vijana na Wanawake.
Mramba amesema hotuba imeonyesha namna ambavyo Serikali imejipanga kusimamia utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa ambapo CCM wanaunga mkono suala la kuendelea vita dhidi ya rushwa, ubadhilifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Amesema ni kuhusu kuimarisha huduma za jamii ambapo CCM wamepongeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuimarisha sekta ya afya, kuboresha elimu,kutoa wigo mpana wa upatikanaji wa maji Safi na kuhakikisha huduma bora za kijamii kwa wazee,vijana na makundi maalum.
Mramba amesema kuwa jambo la tano hotuba ya Rais Samia imejikita katika suala la ushirikiano na ushirikishwaji wa wazee kwani Rais ameonyesha utayari wake katika kusikiliza ushauri wa wazee,kuthamini mchango wao na kuwatambua kama nguzo muhimu ya hekima na utulivu wa Taifa.
Amesema CCM mkoa wa Pwani kwa kauli moja wanathibitisha kuunga mkono hotuba ya Rais Samia kwasababu kuu nne ikiwemo kwani inaweka muelekeo sahihi wa Taifa,inajenga matumaini kwa Watanzania, inasisitiza mshikamano,pamoja na kuweka msingi wa maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vya baadae.
Ameongeza kusema CCM mkoa wa Pwani kinampongeza Rais Samia kwa uongozi wake mahiri,hekima ,na wakijasiri kwa kuonesha uzalendo wa kweli katika kulipigania Taifa.
Hata hivyo,Mramba amesema chama hicho kimeahidi kushirikiana na Serikali katika kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa kwa manufaa na maslahi ya Taifa la Tanzania.


Post a Comment