HEADER AD

HEADER AD

MITUNGI YA GESI YAWAFIKIA WANANCHI BABATI KWA BEI YA RUZUKU


Na Mwandishi wetu , Babati

WANANCHI wa Kata ya Ayalagaya, wilaya ya Babati, mkoani Manyara, wamenufaika na mradi wa mitungi ya gesi aina ya Manjis Logistics Limited kwa kuinunua kwa bei ya ruzuku ya Tsh. 17,500 ambapo jumla ya mitungi ya gesi 3,255 itasambazwa na kuuzwa kwa wananchi wilayani Babati.

Diwani wa Kata ya Ayalagaya , Sabil John amekabidhi mitungi hiyo Desemba, 04, 2025 , kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Babati.


 "Kinachofanyika leo ni kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia  katika kutunza mazingira na afya za wananchi" amesema Sabil.

Sabil amesema, lengo la mradi huo unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ni kuendeleza juhudi za utunzaji wa mazingira na afya za wananchi kwa kuhakikisha wananchi wanapata elimu na hamasa ya kutosha na kufanya mabadiliko katika matumizi ya nishati ya kupikia.

Ameongeza kuwa, mradi huo utabadilisha mtazamo wa wananchi katika matumizi nishati ya kupikia kutoka kutumia kuni na mkaa mwingi na kuanza kutumia gesi.

"Mradi huu utasambazwa na kuuza mitungi ya gesi 3,255 wilaya nzima ya Babati na kata zake zote ambapo kwa mtungi mmoja mwananchi atanunua kwa bei ya ruzuku ya asilimia Hamsini (50%) ya TZS 35,000 mbayo ni sawa na TZS 17,500 tu" amesema .

Mkazi wa Kijiji cha Dereda kati , katika kata hiyo, Barbina Koreyami ameipongeza serikali kwa kufikisha mitungi hiyo ya gesi wilayani humo kwa bei nafuu na kuahidi kwenda kuwahamasisha wananchi wenzake kutumia majiko ya gesi .

" Hapo mwanzo nilikuwa nikitumia sana kuni na mkaa, ila baada ya kupata mtungi huu nimehamasika zaidi kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.

" Nitakuwa wa kwanza kuhamasisha wenzangu kutumia nishati safi hasa  mama lishe wenzangu na wengine" amesema Barbina.

Naye, Mtendaji kata wa Ayalagaya Ndugu Onesmo Lohay , ametoa wito kwa wananchi wa kata ya Ayalagaya kutumia fursa hiyo ya upatikanaji wa mitungi kama nyenzo ya kuachana kabisa na matumizi ya nishati zisizo salama za kupikia ili kutunza afya  na mazingira.











No comments