DKT. MAPANA AWASHAURI VIJANA KAGERA KUTUMIA MITANDAO YA KIJAMII KUTANGAZA MAFANIKIO YAO
Na Alodia Dominick, Bukoba
NAIBU katibu mkuu ofisi ya Rais maendeleo ya vijana Dkt. Kedmon Mapana, amewashauri vijana wa mkoa wa Kagera kutumia mitandao ya kijamii kutangaza mafanikio yao wanayoyapata kutokana na mikopo ya asilimia kumi ya Halmashauri ili na wengine waweze kujitokeza na kutumia fursa hiyo kujiajiri.
Dkt. Mapana ametoa ushauri huo jana wakati akitoa salaam za Wizara hiyo ambapo amemwakilisha Waziri wa Wizara hiyo Joel Nanauka katika uzinduzi wa mpango wa uwezeshaji vijana wa mkoa wa Kagera katika tamasha la Ijuka Omuka (kumbuka nyumbani) linaloendelea mjini Bukoba.
Mpango huo uliozinduliwa unatarajiwa kuwawezesha vijana kupata ajira kupitia sekta ya kilimo, ufugaji,kongani ambazo zimeundwa kutokana na maagizo ya mkuu wa mkoa huo Hajati Fatma Mwassa.
Naye Mkuu wa mkoa wa Kagera Khajat Fatma Mwassa ameiomba Serikali kupitia wizara ya maendeleo ya vijana kusaidia vijana wa mkoa huo kunufaika na fursa zinazojitokeza hapa nchini na nje ya nchi ikiwemo mafunzo ,makongamano na mashindano ili kuwasaidia kufanya makubwa zaidi katika sekta ya ajira.
Hajat Mwassa katika taarifa yake amebainisha fursa zilizotengenezwa na serikali kwa vijana wa Kagera katika kupambana na changamoto ya upatikanaji wa ajira kwa vijana.
Mwassa amesema, serikali ya mkoa huo itahakikisha Halmashauri zote nane za mkoa huo zinazalisha ajira 2000 za vijana kila mwaka kupitia sekta ya kilimo, ufugaji, karakana na mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Serikali.
Rwiza Venanti ni mwenyekiti wa Kongani ya vijana wa Manispaa ya Bukoba ambayo ina vikundi sita vya vijana vinavyounda kongani hiyo amesema, uanzishwaji wa kongani manispaa ya Bukoba umekuwa kichocheo cha ukuaji wa shughuli za kiuchumi kwa vijana wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za ufundi.
Amesema kupitia asilimia kumi ya Serikali kikundi chake kimeweza kukopeshwa kiasi cha shilingi milioni 300 ambapo wameanzisha miradi mbalimbali ya kuwainua kiuchumi.
Ametoa wito kwa vijana kuwa wanyenyekevu na kujifunza kwa uaminifu na ubunifu ili waweze kutumia vipaji vyao na kuvionyesha adharani na jamii iweze kuwaamini na njia hiyo itawafanya kuwa taa na kutimiza malengo na sera ya serikali.

Post a Comment