HALMASHAURI PWANI YATENGA MILIONI 300 KUANZISHA MFUKO WA KUWAINUA KIUCHUMI BODABODA
>> Fedha za mfuko huo hazihusiani na mfuko wa asilimia 10
Na Gustaphu Haule, Pwani
HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha imetenga Tsh.Milioni 300 kwa ajili ya kuanzisha mfuko wa kuwainua kiuchumi maafisa usafirishaji (Bodaboda).
Mbali na kutenga fedha hizo lakini kwasasa Manispaa hiyo imeanza kwa kuwapatia maafisa usafirishaji hao Viakisi Mwanga (reflector) ili waweze kuzitumia katika kazi zao za kila siku.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge watatu kutoka kushoto akiwakabidhi maafisa usafirishaji (bodaboda) Viakisi Mwanga zaidi ya 1000 katika hafla iliyofanyika Disemba 08/2025 katika eneo la Kibaha Mall Manispaa ya Kibaha.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge , ameyasema hayo Desemba 08/2025 wakati akizungumza kwenye mkutano wake na maafisa wasafirishaji wa Manispaa ya Kibaha uliofanyika katika soko la Kibaha Mall.
Mkutano huo uliandaliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kupitia mkurugenzi wake Dkt.Rogers Shemwelekwa huku Jeshi la Polisi na taasisi nyingine ikiwemo Nida, na Latra walikuwa ni wadau muhimu wa kutoa elimu mbalimbali.
Maafisa usafirishaji ( Boda boda) wa Manispaa ya Kibaha wakimsikiliza Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge katika mkutano uliofanyika Disemba 08/2025 katika eneo la Kibaha Mall.
Mkutano huo uliwashirikisha zaidi ya maafisa wasafirishaji 1000 ambapo Kunenge amesema mfuko huo utatumika kuwainua kiuchumi na kwamba watatakiwa kurejesha kwa wakati ili wengine nao waweze kunufaika.
Amesema fedha za mfuko huo hazihusiani na fedha za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa kundi la Vijana,Wanawake na wenye Ulemavu kwani fedha hizo ni maalum kwa bodaboda tu.
"Ndani ya siku 100 za Dkt.Samia Suluhu Hassan alisema atatenga Sh.bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha maafisa usafirishaji na tayari kazi hiyo imeanza na kwa upande wa Manispaa ya Kibaha imeanza kutenga milioni 300 kiasi ambacho kinaweza kuongezeka kulingana na uhitaji lakini ukipata rudisha ili wengine nao waweze kupata," amesema.
Amesema kundi la maafisa usafirishaji ni muhimu katika kujenga uchumi wa nchi lakini pia wamekuwa wakifanya kazi vizuri kwa ajili ya kuwasafirisha watu kutoka eneo moja kwenda eneo lingine kirahisi zaidi.
Kunenge amesema kutokana na umuhimu huo lazima wawe makini ikiwa pamoja na kuepuka kutumika vibaya na watu wasiokuwa na nia njema ya kutaka kuharibu amani na utulivu wa nchi .
Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza na maafisa usafirishaji wa Manispaa ya Kibaha katika mkutano uliofanyika Disemba 08/2025 katika eneo la Kibaha Mall.
Ameongeza kuwa kundi hilo ni muhimu pia katika jamii na wanayonafasi kubwa ya kuwabaini watu ambao hawana nia njema na nchi yetu na kamwe wasiruhusu watu kuharibu amani yetu na kwamba yeyote wanayemuona ameingia katika kazi yao na wanamtilia mashaka ni vyema wakamfichua haraka kwa kutoa taarifa katika vyombo vya dola.
Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Pwani Edson Mwakihaba amesema maafisa usafirishaji hao wanapewa elimu ya usalama barabarani ili waweze kuzingatia sheria zilizopo.
Mwakihaba amesema wameanza utaratibu wa kutoa mafunzo kwa Wilaya ya Kisarawe na sasa wanaendelea Manispaa ya Kibaha na maeneo mengine watayafikia ili kila anayefanya biashara hiyo ya boda boda awe na ufahamu wa sheria za usalama barabarani.
Naye Ramadhani Maulid afisa usafirishaji kutoka Kata ya Misugusugu ambaye alikuwa mshiriki wa mkutano huo ameishukuru Serikali kwa kuanzisha utaratibu huo huku akiahidi kufuata maagizo ya Mkuu wa mkoa katika kusaidia kuwafichua watu wenye nia mbaya na Taifa.
Hata hivyo,zaidi ya maafisa usafirishaji 1100 wa Manispaa ya Kibaha wamepatiwa viakisi mwanga na mafunzo ya sheria za usalama barabarani mafunzo ya ulinzi na usalama yatakayowasaidia pindi wawapo kwenye kazi zao.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akiwakabidhi Viakisi Mwanga maafisa usafirishaji wa Manispaa ya Kibaha na kwanza kushoto ni Naibu Meya wa Manispaa Aziza Mruma na wapili kutoka kushoto ni Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nickas.
Vyombo vya usafiri vinavyotumiwa na maafisa usafirishaji wa Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani






Post a Comment