HEADER AD

HEADER AD

KANISA LA WASABATO NYAMONGO LATOA MSAADA WA VIFAA WEZESHI KWA WENYE MAHITAJI MAALUM, MILIONI 4 ZACHANGWA

>>  Wenye uhitaji maalum wapewa Baiskeli magodoro, sabuni, magongo Biblia, nguo, miwani 

>>Chinga muuza nguo aguswa atoa Milioni moja

>> Happy Francis, Kelvin Mroni, Mchungaji Doto watia neno

Na Mwandishi Wetu, Nyamongo 

KANISA la Waadventista Wasabato Nyamongo Kati, limetoa msaada wa vifaa wezeshi huku zaidi ya Tsh. Milioni 4 zikichangwa na waumini pamoja na wadau mbalimbali ili kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum ndani ya kanisa .

Vifaa wezeshi vilivyotolewa ni pamoja na Baiskeli 6 kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa miguu, magodoro, Sabuni, Magongo ya kisasa, Biblia, Sabuni, Nguo na fedha , vilivyotolewa siku ya jumamosi, Desemba, 27,2025 wakati wa ibada kanisani hapo .

        Magodoro na nguo zilizotolewa na Kanisa la Waadventista Wasabato Nyamongo kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum wakati wa ibada maalum ya watu wenye mahitaji maalum iliyofanyika Desemba, 27,2026.

Mchungaji wa kanisa la Waadventista Wasabato mtaa wa Kewanja, Doto Shija amesema kwamba kanisa la Wasabato Nyamongo kati kupitia kitengo maalum cha mahitaji maalum, ilitenga Sabato maalum kwa ajili ya watu wenye uhitaji na kuweza kutoa pesa na vifaa wezeshi.

          Mchungaji wa kanisa la Waadventista Wasabato mtaa wa Kewanja, Doto Shija akizungumza .

" Leo ni Sabato maalum ya watu wenye uhitaji maalum .Tumewakabidhi vifaa wezeshi Baiskeli kwa wale wenye changamoto ya kutotembea , miwani kwa ajili ya wenye ulemavu wa macho, biblia za kawaida na za maudhui ya sauti, Magongo ya kisasa, sabuni, pamoja na nguo.

"Kanisani tuna kitengo cha mahitaji maalum. Kupitia mratibu wa kitengo cha mahitaji maalum, namshukuru Bhoke Orindo mwenye ulemavu wa macho amesaidia kufanikisha zoezi hili kwa kutafuta wadau ambao wamewezesha upatikanaji wa vifaa wezeshi na fedha kwa ajili ya kutunisha mfuko kitengo cha mahitaji maalum.

Mgeni rasmi katika harambee ya kuchangia huduma wezeshi , Happy Francis ametoa msaada wa baiskeli moja na Tsh. 500,000 ambapo katika harambee kiasi cha pesa zaidi ya Milioni nne zimechangwa na waumini pamoja na wadau mbalimbali .

           Happy Francis akizungumza na waumini akiwa mgeni rasmi siku maalum ya watu wenye mahitaji maalum kanisa la Waadventista Wasabato Nyamongo.

" Natoa wito kwa watu wengine wawasaidie wenye uhitaji . Naomba wenye uwezo wawe wanamtafuta Bhoke na kumpatia misaada akiwa kama kiongozi wa kitengo cha wahitaji kanisani ili aweze kuwasaidia wenzake wenye uhitaji maalum.

Kelvin Mroni muumini wa kanisa la Roman Katoriki aliyekuwa mgeni mwalikwa, ametoa msaada wa baiskeli  moja na Pesa tasilimu Tsh. 200,000 huku akiahidi kutoa Tsh. 800,000 ndani ya wiki hii pamoja na kununua baiskeli 10 za watu wenye ulemavu wa miguu atakazo kabidhi kanisa hilo Juni, 2026.

    Kelvin Mroni muumini wa kanisa la Roman Katoriki Nyamongo akimkabidhi Magongo mwalimu Mekaus wa shule ya msingi Magufuli ya mahitaji maalum wakati alipoalikwa kushiriki ibada maalum ya watu wenye ulemavu kanisa la Nyamongo SDA .

Amewaomba waumini wa dini zote kuwasaidia watu wenye uhitaji kama njia ya kudumisha upendo kwa binadamu.

" Nimefika hapa kwa mwaliko wa Bhoke, nimesoma nae darasa moja ,nimemchangia Baiskeli ya Tsh. 500,000 , nimekuja na laki mbili kumuunga Bhoke lakini baada ya kufika hapa nimejisikia huzuni ,natoa laki mbili . Naahidi baada ya ibada hii Bhoke aje achukue Tsh. 800,000 ikamilike Milioni moja" amesema Kevin.

Ameongeza " Bhoke ni mlemavu wa macho anayetembea kwa msaada, mwendo wake sio mrefu ni mtu wa kukaa ndani lakini bado anawakumbuka Binadamu wanaoishi nje ya mazingira yake" amesema Kevin.

      Kevin Mroni akiteta jambo na Bhoke Orindo ambaye ni mratibu wa kitengo cha mahitaji maalum kanisa la Nyamongo SDA

Ametoa wito kwa jamii kutowatenga na kuwabagua watu wenye ulemavu wa viungo na badala yake wawasaidie mahitaji yao " Tuwasaidie wahitaji kwasababu hawana nyenzo . Kama Mungu anasema yeye ni upendo basi tupendane sisi kwa sisi tusibaguane kwa tofauti zetu za dini " amesema Kevin.

Yusuph Tambana muuza nguo (Chinga) amechanga Tsh. 1,000,000 na kusema  "  Nilinusurika kufa kwenye ajali ya gari , lakini kaka yangu alipigwa risasi wakati wa maandamano alipokuwa ameenda Dar es Salaam kununua mzigo wa biashara.

Yusuph Tambana muuza nguo (Chinga) aliyevaa Sweta akilia wakati akizungumza baada ya kuguswa na ibada ya watu Wasioona ambapo alichangia Tsh. Milioni moja Kitengo cha mahitaji maalum kanisa la Waadventista Wasabato Nyamongo Kati.

" Mimi na familia yangu tumekubaliana kuchangia Milioni moja maana huwenda na mimi leo ningekuwa mlemavu . Ningetamani nichangie Milioni 20 lakini kulingana na uwezo nachangia sh. 1,000,000. 

Bhoke Makabala mkazi wa Kijiji cha mjini kati amelishukuru kanisa la SDA Nyamongo kwa kumpatia msaada wa miwani na jozi moja ya kitenge.

          Mkazi wa Kijiji cha mjini kati, Bhoke Makabala mwenye tatizo la macho akishukuru baada ya kupata miwani ya macho na vitenge kutoka kanisa la Nyamongo SDA.

" Namshukuru sana Mungu kwa kuniwezesha kufika hapa nashukuru msaada huu wa miwani itanisaidia sana maana nina changamoto ya macho sioni vizuri nilikuwa nikitembea najikwaa kwasababu ya kutoona vizuri " amesema Bhoke Makabala.

Mratibu wa huduma wezeshi kwa watu wenye ulemavu Nyamongo SDA , ambaye pia ni mwanachama wa Chama chama Wasioona (TLB) wilaya ya Tarime, Bhoke Orindo ameushukuru uongozi wa kanisa hilo akiwemo mchungaji Shija, Wazee wa kanisa, wakuu wa huduma kanisani , kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha kanisa hilo linatenga siku maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu .

" Nawashukuru wadau wote waliotusapoti kwasababu kabla ya harambee hii tuliomba michango tukapata milioni nne zilizotumika kununua vifaa wezeshi. 

" Leo hapa kanisani tumeweza kuchangiwa zaidi ya Milioni nne nawashukuru waumini na viongozi wa dini kwa ushirikiano wenu hadi kufanikisha hili jambo muhimu la ibada ya wenye ulemavu " amesema Bhoke.

      Mratibu wa huduma wezeshi kwa watu wenye ulemavu Nyamongo SDA , ambaye pia ni mwanachama wa Chamachama Wasioona (TLB) wilaya ya Tarime, Bhoke Orindo (aliyesimama katikati )

Katika ibada hiyo wameshiriki waumini wa kanisa hilo, baadhi ya watu wenye ulemavu kutoka madhehebu mbalimbali kutoka wilaya ya Tarime, Musoma na Serengeti pamoja na mwimbaji maarufu mwenye ulemavu wa macho kutoka mkoani Mwanza John Julius (J J)  .




























No comments